Jaji Francis Mtungi akifungua mkutano wa wadau wa siasa wa uimarishaji demokrasia ya vyama vingi.
Dk. Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam ambaye amebobea katika masuala ya siasa amewataka wadau wa siasa na wananchi kwa ujumla kuzuia uvunjifu wa amani kuelekea uchaguzi mkuu kwa kufuata Sheria na kutobeza mamlaka.
Dk Bana alisema hayo jana akijibu swali la msimamizi wa mdahalo wenye lengo la kuimarisha demokrasia ya vyama vingi ulioandaliwa na Msajili wa Vyama vya siasa kwa ufadhili wa UNDP, Profesa Bernadetta Killian.
Profesa Killian alitaka kujua baada ya maelezo ya awali ya Dk Bana juu ya mtazamo wake kuhusu ukuaji wa demokrasia ya vyama vingi nchini Tanzania , nini kinastahili kufanya kuepuka uvunjifu wa amani hasa katika muda huu ambapo viashiria vipo.
Dk Bana alisema kama watu hawatafuata utamaduni wa vyama vingi, utamaduni wa kufuata sheria na kutobeza mamlaka, taifa litaingia katika machafuko.