Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri
James, amewataka viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, hususan idara ya
elimu sekondari, uhandisi na manunuzi, kusimamia kwa umakini na weledi miradi
ya serikali ili kuhakikisha inaleta manufaa kwa wananchi.
RC James alitoa kauli hiyo jana
baada ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo,
ikiwemo ujenzi wa mabweni mawili ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita katika
Shule ya Sekondari Ifingo, Kata ya Kising’a, Tarafa ya Kilolo, kupitia mradi
kuboresha mazingira elimu sekondari (SEQUIP).
Katika ukaguzi huo, Mkuu wa Mkoa
hakuridhishwa na kasi ya utekelezaji pamoja na usimamizi wa mradi huo, baada ya
kubaini kuwa licha ya fedha kutolewa, bweni moja bado halijakamilika.
“Sijaridhishwa na usimamizi wa
ujenzi wa mabweni haya. Fedha hazijatumika ipasavyo na baadhi ya majengo
yamebaki magofu. Hatutamvumilia mtu yeyote atakayechezea fedha za serikali,”
alisisitiza RC James.
Amesema Wilaya ya Kilolo imekuwa
ya mwisho katika utekelezaji wa miradi ya kijamii kutokana na upungufu wa
usimamizi, ukosefu wa weledi katika uhandisi na manunuzi, hali inayosababisha
miradi mingi kuchelewa kukamilika huku wananchi wakikosa huduma stahiki.
“Kila mradi Kilolo unachunguzwa
na TAMISEMI, TAKUKURU, lakini bado changamoto ni kubwa. Huu ni uzembe
usiokubalika kwa kuwa wilaya hii ina uwezo wa kiuchumi wa kutosha,” aliongeza
kwa msisitizo.
Katika ziara hiyo, RC James
alikagua pia miradi mingine ikiwemo Kituo cha Afya Nyalumbu, Shule ya Wasichana
ya Mkoa wa Iringa (Lugalo Girls High School), Shule ya Sekondari Kilolo, Shule
ya Sekondari Lukosi na Kituo cha Afya Ruahambuyuni.
WITO KWA WANANCHI IRINGA
Wakati huohuo, Mkuu wa Mkoa wa
Iringa aliwataka wananchi wa Kata ya Magulilwa, Tarafa ya Mlolo, Wilaya ya
Iringa, kulinda na kutunza miundombinu ya Kituo cha Afya Mlanda ili kiweze kutoa
huduma bora kwa muda mrefu.
Alisema mafanikio ya miradi ya
maendeleo yanategemea sio tu serikali na wataalamu, bali pia ushirikiano wa
wananchi katika kuitunza na kuilinda.
“Kituo hiki ni cha wananchi wote.
Ni wajibu wetu kukilinda dhidi ya uharibifu wa aina yoyote. Tunahitaji
usimamizi madhubuti kutoka kwa wataalamu na ushirikiano kutoka kwa jamii,”
alisema RC James.
Aidha, aliwataka wataalamu wa
halmashauri zote kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu,
sambamba na kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana kwenye kila mradi
unaotekelezwa.
Ziara hiyo ni sehemu ya mikakati
ya Serikali ya Mkoa wa Iringa katika kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa
miradi ya maendeleo na kuhakikisha huduma za msingi kama elimu na afya
zinawafikia wananchi kwa ubora unaostahili.
Mwisho
No comments:
Post a Comment