IRINGA: Kaimu Balozi wa Marekani Dk Inmi Patterson amepongeza juhudi zinazofanywa na serikali ya Tanzania katika kushughulikia masuala ya udamavu na utapiamlo vinavyoathari wananchi wengi nchini .
Balozi huyo alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa ghala jipya la Mama Seki sambamba na mashine ya kusaga unga wa mahindi wa lishe bora iliyotolewa kwa msaada wa serikali ya marekani kupitia mradi wa NAFAKA, ikiwa sehemu ya ziara yako mkoani Iringa.
Dk Patterson alisema kuwa Tanzania ina aslimia 34 ya wakazi wake wanaoishi na udumavu na utapiamlo huku wilaya za Iringa, Njombe na Songwe zote zikiwa na viwango vya utapiamlo kwa zaidi ya asilimia 40.
Alisema kuwa juhudi zaidi zinahitajika katika kuboresha masuala ya elimu bora na lishe bora ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa na serikali ya kupunguza matatizo ya udumavu na utapiamlo nchini.
Alisema kuwa ukosefu wa lishe unamfanya mtu asiweze kufikia malengo yake kwa vile udumavu huathiri mwili na akili.
Dk Patterson pia aliongeza kuwa watoto wenye lishe duni hawafanyi vizuri shuleni, kitu amabcho kina punguza fursa na hatima ya ajira siku za mbeleni.
“Ninayo furaha kwa kuwa sehemu ya mafaniko ya Mama Seki katika kuzindua mashine ya kuzalisha unga wa mahindi bora unaopatikana katika Mkoa wa Iringa na katika maeneo yote ya nyanda za juu kusini. Biashara ya Mama Seki inasaidia juhudi za serikali katika kushughulikia masuala ya udumavu na utapiamlo yanayoiathari nchi hii…,” alisema kaimu balozi wa marekani.
Alisisitiza kuwa watu wazima wenye lishe duni hawawezi kufanya kazi, kuchangia katika uchumi wa ndani, na kutoa huduma kwa famila zao.
“Wamama wenye lishe duni wana uwezekano mkubwa wa kupata watoto wenye uzito mdogo, ambao pia wana hatari kubwa ya kuathirika kimwili na akiakili, ” alisema Dk Patterson.
Alisema kuwa uwepo wa ghala jipya la Mama Seki na kiwanda cha kuzalisha wa bidhaa bora na lishe kunaonesha ufanisi wa ushirikiano kati ya serikali mbili za Tanzania na Marekani kutambua na kuunga mkono biashara za wanawake ili kuboresha nafasi zao za kiuchumi.
Naye, Ritha Sekilovele, Mkurugezi wa Kampuni ya ‘Super Seki Investment’ alitoa shukrani kwa mradi wa USAID NAFAKA kwa kuweza kumsaidia mambo mengi ambayo kimsingi ndiyo wameweza kumfikisha hapo.
Alisema kuwa mradi huo umempatia mashine mbili za kurutubisha unga wa mahindi zenye thamani ya shilingi milioni 22,840,000/- ambazo zinasaidia kusindika unga ulioogezwa virutubishi kama mpamgo wa serikali ulivyo lenga kupunguza utapiamlo na udumavu katika Mkoa wa Iringa.
Alisema kuwa alianza shughuli za kusindika unga wa mahindi miaka 25 iliyopita akiwa na mtaji mdogo, lakini kupitia mradi wa NAFAKA kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita ameongeza mara mbili uzalishaji wake kufikia tani 15 za unga kwa siku, ambapo asilimia 15 ya uzalishaji wake hutumia kuzalisha unga bora wa mahindi.
Sekilovele (Mama Seki) alisema kuwa mradi huo pia umemsaidia kumuunganisha na wanunuzi wa bidhaa zake ndani na nje ya nchi kwa mfano wameweza kumkutanisha na wanunuzi wa huko Kenya na ataanza kuuza bidhaa hizo pindi tu majibu ya samuli za vibali vya ubora wa bidhaa vitakapotoka.
Pia masoko ya unga ulioongezwa virutubishi yameongezeka na kuuza ndani ya Mkoa wa Iringa na nje ya mkoa kama vile Morogoro, Kilombero, Lindi na Mtwara.
Hata hivyo, Mama Seki alisema kuwa zipo changamoto anazokukatanazo katika shughuli za usindikaji ikiwemo vifaa vya kuhifadhia malighafi (mahindi) ambavyo imekuwa changamoto kwake, kwani saa zingine mahindi yanaharibika kulingana na hali halisi ya mazingira anayotunzia.
Alisema kuwa changamoto nyingine ni umeme kwenye jengo lake jipya ni mdogo ambao unauwezo wa kuendesha mashine moja tu, hivyo kushindwa kusaga kwa wakati na kuweza kuhudumia masoko yake.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya Iringa Richard Kasesela kwa niba Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Hapi, aliipongeza serikali ya Marekani kwa kuunga juhudi za serikali ya Tanzania katika sera ya uchumi wa viwanda.
Alisema kuwa uzinduzi wa ghala jipya na mashine za kusindika unga wa mahindi linaonesha ufanisi wa ushirikiano kati ya serikali hizo mbili kutambua, na kuunga mkono biashara za wanawake ili kuboresha nafasi zao za kiuchumi.
DC Kasesela alisema kuwa mafanikio ya Mama Seki ni mfano wa hatua kubwa katika uwezeshaji wa wanawake, afya ya jamii na ukuaji wa sekta ya kilimo kwa kufanya kazi kwa pamoja kati ya serikali zote mbili.
Kuhusu tatizo la umeme, alisema kuwa serikali ya Mkoa wa Iringa itahakikisha kuwa tatizo hilo la umeme kuwa mdogo katika jengo jipya linapatiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo ili kiwanda hicho kiweze kuendesha mashine zote mbili na kusaga unga kwa wakati.