BAADHI ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa mjini Iringa katika Jimbo la Iringa Mjini, kesho wameahidi kuanza kurudisha kadi za chama hicho katika ofisi za matwi yao ikiwa ni matokeo ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho kumuengua katika kinyang’anyiro cha ubunge, Fredrick Mwakalebela aliyeshinda kura za maoni za chama hicho katika jimbo la Iringa Mjini.
Katika kura hizo, Mwakalebela alimshinda kwa kura 3, 897 na mpinzani wake wa karibu Bi.Monica Mbega aliyepata kura 2,989.
NEC imemuengua Mwakalebela katika mbio hizo za kuusaka ubunge katika jimbo hilo kumeelezwa kuhusishwa na kashfa ya rushwa inayomkabili.
Baada ya kupata taarifa za kuwepo kwa baadhi ya wanachama walioapa kurudisha kadi za chama hicho na kumuunga mkono mgombea wa Chama cha demokrasia na Maendeleo (Chadema), mwandishi wa habari hii jana alitembelea baadhi ya matawi ya chama hicho mjini hapa na kushuhudia makundi ya wanaCCM wakijipanga na kuendelea kuwashawishi wenzao kesho kuzirudisha kadi za CCM katika ofisi za matawi yao.
Matawi hayo ni pamoja na Kichanngani, Kihesa, Wilolesi, Soko Kuu la Mjini Iringa, Mshindo na Igumbilo.
Baadhi ya wanaCCM hao walisema maamuzi ya NEC yamemtoa kafara Mwakalebela ambaye taarifa zilizopo zinaonesha kwamba hakuwahi kukamatwa akitoa rushwa katika kinyang;anyiro hicho cha kura za maoni.
“Taarifa za Takukuru zinadai kwamba kwa kupitia mke wake ambaye naye hakukamatwa akifanya hivyo, Mwakalebela alitoa rushwa ya Sh 100,000 kwa wanachama 22 wa kijiji cha Mgongo, waliokuwa wamekusanyika nyumbani kwa Gwido Sanga wakimsikiliza wakati akitangaza nia ya kuwania ubunge katika jimbo hilo,” alisema David Butinini wa tawi la Mtwivila.
Naye Julie Sawani wa tawi la Kichangani, alisema wakati Mwakalebela akienguliwa kwa madai hayo ya rushwa, inashangaza kuona NEC hiyo hiyo imeyapitisha majina ya Basil Mramba na Andrew Chenge ambao wanatuhuma kubwa za rushwa.
Alli Mduba wa tawi la Kihesa alisema uamuzi wa CCM wa kuwataka wanachama wote washiriki katika kura hizo umekiwezesha chama hicho kujua wagombea wanaokubalika katika mbio hizo za uongozi, hata hivyo akasema maamuzi yaliyofanywa na NEC dhidi ya Mwakalebela majibu yake watayapata Oktoba 31, siku ya Uchaguzi Mkuu.
Mohamed Kassim wa wilolesi alisema, kesho jumatatu wanachama watarudisha kadi zao za CCM katika ofisi ya tawi katika tukio ambalo pia watalitumia kumtangaza rasmi mgombea watakayemuunga mkono.
Naye Edgar Sanga wa Igumbilo alisema wanaCCM watamaliza jazba zao za mgombea wao kuenguliwa kwa kumpigia kampeni na kura mgombea wa Chadema. Mchungaji Peter Msigwa.
“Mwakalebela ndiye aliyekuwa chaguo letu vijana, na wananchi wote wa jimbo la Iringa Mjini bila kujali rangi, itikadi, dini na makabila yao, tumesikitishwa na uamuzi wa NEC,” alisema mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Anna Michael wa tawi la Miyomboni.
Sunday, 15 August 2010
…VIGOGO………….1
ALIYEKUWA mshindi wa pili katika kura za maoni za Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Njombe Kaskazini, Alatanga Nyagawa huenda akatimkia CHADEMA ikiwa ni hatua mojawapo ya kupinga maamuzi ya vikao vya juu vya chama hicho yaliyomteua Deo Sanga (Jah People) kuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo.
Katika kura hizo, Jah people alipata kura 6,313 dhidi ya kura 2,313 alizopata Nyagawa huku mbunge mkongwe aliyemaliza muda wake Jackson Makweta akipata kura 1,671.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, Nyagawa alisema yeye pamoja na wanaCCM wengine 11 waliokuwa wakiwania kushinda kura za maoni za jimbo hilo, walipinga matokeo yaliyompa ushindi Jah People kwa madai kwamba yalitawaliwa na mazingira ya hila na rushwa.
Nyagawa alisema tofauti na matarajio yake vikao vya juu vya CCM vimetupilia malalamiko yao ambayo yana ushahidi wa kutosha.
Nyagawa alisema kutokana na kasoro hizo hayuko tayari kuunga mkono ushindi na uteuzi wa Jah People kuwania ubunge katika jimbo hilo.
Alipoulizwa wapi hatma yake ya kisiasa itakuwa baada ya malalamiko yao dhidi ya Sanga kutupiliwa mbali, Nyagawa alisema anaendelea kupokea ushauri kutoka kwa wanaCCM na wapiga kura wengine wa jimbo hilo la Njombe.
Hata hivyo vyanzo vyetu vya habari kutoka katika jimbo hilo vimethibitisha kwamba baadhi ya wanaCCM wanaendelea na jitihada kumshawishi Nyagawa agombee jimbo hilo kwa kupitia Chadema.
Mmoja kati ya vyanzo hivyo alilidokeza gazeti hili kwamba maoni ya haraka yanaendelea kukusanywa kutoka katika kata zote za jimbo hili ili kupata ushauri zaidi kuhusiana na ushawishi huo wa kumtaka Nyagawa agombee kwa chama hicho.
Wakati hali ya kisiasa katika jimbo hilo ikiwa na mtazamo huo, wapiga kura wa jimbo la Njombe Magharibi nao wamesema wanataka sauti zao zisikike katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu na hivyo kwa hamu kubwa wanasubiri kujua hatma ya kisiasa ya aliyekuwa mshindi wa kura za maoni za chama hicho, Thomas Nyimbo.
Licha ya kuongoza katika kura za maoni Nyimbo na mbunge aliyemaliza muda wake Yono Kevela ambaye katika kinyang’anyiro hicho alishika nafasi ya pili, NEC iliwatupilia mbali na nafasi ya kuliwania jimbo hilo ilikwenda kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) mkoa wa Dodoma, Greyson Lwenge.
Katika kura hizo Nyimbo alipata kura 6,795 dhidi ya kura 3,434 alizopata Kevela na 2,971 alizopata Lwenge katika kinyang’anyiro hicho kilichokuwa na wagombea 13
UBALOZI WA UNITED ARAB EMIRATES NCHINI WATOA MSAADA KWA WAISLAM
UBALOZI wa United Arab Emirates (UAE) nchini kupitia kwa Balozi wake Maala llah Mubarak Suweid umetoa msaada kwa waislamu kupitia taasisi ya Dhi nureyn Islamic Foundation yenye makao yake makuu – mkoani Iringa.
Msaada huo ambao umetolewa na taasisi mbili za nchini UAE ambazo ni : Sheikh Khalifa Bin Zaid Al Nahyan Foundation for humanitarian aid na Red Crescent Society of UAE , misaada hiyo ni kwa jili ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ambao waislamu hufunga na kuzidisha kufanya mema kwa ajili ya kujikurubisha kwa mwenyezimungu.
Akizungumzia kuhusu msaada huo, Mwenyekiti Mtendaji wa Taasisi ya Dhi Nureyn Sheikh Said Ahmed Abri, amemshukuru balozi Maala llah na ubalozi mzima wa UAE kwa msaada huo, na amemuomba afikishe salamu na shukrani za waislamu kwa uongozi mzima wa uae na watu wake.
Msaada uliotolewa unafikia shilingi milioni hamsini (50,000,000) ambazo ni :
35,000,000 fedha taslimu kwa ajili ya programu za ufuturishaji na bosks 500 za tende zenye jumla ya kg 6,000 zenye thamani ya shilingi milioni 15,000,000/=.
Misaada hiyo tayari imekwisha sambazwa kwa walengwa kupitia misikiti zaidi ya 50 katika mikoa ya Iringa, Singida, Mbeya, Kilimanjaro na Dar es salaam.
.
Subscribe to:
Posts (Atom)
WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...
Na Friday Simbaya, Mufindi Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...
-
KIKUNDI cha Upendo ni kikundi cha kina mama 20 walioamua kujiunga kwa pamoja na kuanz...
-
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini MIEMBE hulimwa karibu katika nchi zote zilizoko kwenye ukanda wa joto, na hasa tropiki. Nchini ...
-
Habari ndugu msomaji wetu wa blog, Natumaini unaendelea vyema. Leo tutaanza kujifunza kilimo cha bora cha nyanya, na tutaanza kufahamu vit...