Na Friday Simbaya, Songea
Halmashauri ya Wilaya ya Songea,
Mkoa wa Ruvuma katika Idara ya Elimu ya Msingi ina jumla ya wanafunzi 3770 wasiojua kusoma,
kuandika na kuhesabu (K.K.K.), imefahamika.
Hayo yalibainika wakati wa mkutano wa kutathmini elimu na matokeo ya
mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi na daras la nne mwaka 2013 uliofanyika hapa
Peramiho hivi karibuni .
Akisoma taarifa yake ya
utekelezaji kwa wadau wa elimu mbalimbali waliohudhuria kikao hicho cha siku
moja, Afisa Elimu Taaluma, Wilaya ya Songea, Vincent Chimoto alisema kuwa wapo
wanafunzi wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu katika shule za msingi mwaka
2013 wapatao 3770 darasa la I-VII.
Afisa huyo wa elimu taaluma
pia aliwaagiza walimu kuchukuwa jitihada za makusudi kwa kutenga muda wa ziada
na kuwa na ratiba ya kuwafundisha wanafunzi hao ili wajue stadi za K.K.K.
Aidha, alisema kuwa Halmashauri
ya Wilaya ya Songea inazo jumla ya shule za msingi 96, kati ya hizo shule zenye
darasa la saba ni 89.
“ Wilaya ina jumla ya wanafunzi
wapatao 32,592 kati ya hao wavulana ni 16,010 na wasichana 16,582,” alifafanua.
Alisema wilaya ina jumla ya
walimu 721, mahitaji ni 911 hivyo upungufu ni walimu 190.
“Katika mgao wa walimu wapya
mwaka 2013 tulipata walimu 96, lakini walioripoti ni 87 na ambao walisafirishwa
hadi katika vituo vyao vya kazi,” aliongeza.
Awali akifungua kikao hicho cha
wadau wa elimu, Mkuu wa Wilaya ya Songea, Joseph Mkilikiti aliwataka wadau kuchukua hatua za makusudi kwa kuweka nguvu ya pamoja kuinua sekta ya
elimu wilayani hususani elimu ya msingi.
Alisema kuwa elimu ya msingi
ndio kila kitu ni kama msingi wa nyumba. Msingi wa nyumba unapokosewa hakika
nyumba hiyo haiwezi kuwa imara tena.
MATOKEO YA MTIHANI
Mtihani wa kuhitimu elimu ya
msingi ulifanyika nchini kote kuanzia tarehe 10-11/9/2013. Wilaya ilikuwa na
jumla ya shule za msingi zipatazo 89 zenye wahitimu wapatao 3738 kati yao
wavulana ni 1680 na wasichana ni 2058 waliosajiliwa kufanya mtihani.
Matokeo ya mtihani
yanaonesha kuwa wilaya ina wastani wa ufaulu wa asilimia 42.5 ukilinganisha na
ule wa mwaka 2012 ambao ni asilimia 30. Katika matokeo ya kimkoa, wilaya ni ya
pili kwa kupata wastani wa ufaulu asiliamia 42.5.
CHANGAMOTO ZINAZOKABILI
UTOAJI TAALUMA
Upungufu wa walimu
unaotokana na walimu wengi kustaafu na wengine kufariki dunia, mfano wastaafu
2010/2011 walimu 28, 2011/2012 walimu 26, 2013/2014 walimu 37. Jumla yao ni 91
na waliofariki dunia ni walimu 13.
Utoaji chakula kwa wanafunzi
bado ni tatizo, msisitizo unahitajika wa pamoja ili kufikia malengo ya shule
zote kutoa chakula. Mwaka 2013 shule 48 kati ya 96 zinatoa chakula.
Utoro wa rejareja wa walimu
na wanafunzi huchangia kushusha taaluma. Kwa upande wa walimu mada katika
masomo hazimaliziki na kwa upande wa wanafuzi kukosa baadhi ya mada.
Baadhi ya walimu kutokuwa na
moyo wa kujituma kuwafundisha wanafunzi hususani wanafunzi wasiojua K.K.K. na
wanajiandaa kufanya mitihani ya taifa darasa la nne na la saba.