Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda amewataka wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam kutunza mazingira hasa sehemu zenye mazalia ya mbu ili kuepukana na ugonjwa wa mabusha na matende.Makonda ametoa wito huo siku ya leo.
Kata ya Buguruni wakati akizindua kampeni ya uhamasishaji unywaji dawa na kufanyiwa upasuaji kwa magonjwa yasiyopewa kipaumbele ambayo ni Matende, Mabusha, Kichocho, Minyoo na Usubi, ambapo takwimu zinaonesha wakazi wa Dar es Salaam wamekuwa wakisumbuliwa na magonjwa ya minyoo, matende na mabusha.
Makonda ameeleza ni vyema wakazi wa Dar es Salaam wakaitumia fursa hiyo ya kampeni itakayodumu kwa siku tano kuanzia siku ya leo mpaka Oktoba 30, kwani kujitokeza kwao kwa wingi kupimwa na kunywa dawa kutaisaidia serikali kuinua nguvu kazi itakayochochea ukuaji wa uchumi kwani watu wakiugua maradhi hayo bila ya kupata tiba au kuwa na kinga mapema hupoteza nguvu kazi.
Makonda ameongeza kuwa takribani ya watu 6400 wamegundulika na mabusha hivyo ni vyema wakawahi mapema na wengine wajitokeze kwa wingi kuizidi idadi ya wananchi milioni 3.9 waliojitokeza mwaka 2009.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Grace Maghembe amewataka wakazi hao kutosikiliza upotoshaji wa kuwa wakitumia dawa hizo hawatakuwa na uwezo wa kupata watoto na badala yake wajitokeze kwa wingi kwani dawa hizo ni salama, huku akisisitiza kuwa kwa zoezi la unywaji wa dawa litaishia Oktoba 30 huku upasuaji ukiendelea mpaka mwezi Desemba ambapo tayari upasuaji kwa watu wenye mabusha unaendelea kwa kituo kilichopo Pugu na zaidi ya watu 76 wamepatiwa matibabu katika kituo hicho, ambapo hapo baadae wataongeza vituo vingi zaidi kwa maeneo mengine.