Na Friday Simbaya, Songea
Paroko Msaidizi wa Parokia ya Peramiho katika Jimbo Kuu la Songea,
Padre Benedict OSB ametoa rai kwa wazazi wa Peramiho na kwingineko kuwaelekeza
watoto katika masomo kwa sababu elimu ni mwanga wa maisha.
Alisema kuwa wazazi na walezi wanapaswa kuwasomesha watoto
wao ili kuwaandalia maisha mazuri kwa baadaye yenye faraja.
Paroko huyu aliyasema haya jana wakati wa Ibada ya Misa
Takatifu ya mazishi ya marehemu Barnabas Jacob Mkuwa (91), ambaye alikuwa baba
mzazi wa Mbunge wa Viti Maalum, Rais wa Vicoba Tanzania na Mjumbe wa Bunge
Maalum la Katiba, Devote Mkuwa Likokola.
Misa hiyo iliyofanyika nyumbani kwa marehemu Mtaa wa Madukani,
Peramiho wilayani Songea, mkoani Ruvuma iliongozwa na mapadre saba, akiwemo Padre Lucius OSB aliyeongoza madhehebu yote ya Misa.
Alisema kuwa kuna baadhi ya wazazi wanakwepa majukumu ya
kuwalea watoto wao katika maadili mema ikiwa pamoja na kuwapatia elimu, afya,
mavazi na malezi. “Watoto ni zawadi kwenu, simameni imara katika malezi ili
baadaye wawe faraja kwenu,”aliongeza paroko huyo.
‘Wazazi na walezi popote duniani wanatambua kuwa hakuna
jukumu zito kama la kulea watoto. Ni kazi ngumu ambayo haina likizo. Wazazi
makini huwalea watoto wao kwa kuwapatia elimu, afya, mavazi na malezi,’alisema
paroko huyo.
Alitoa mfano wa marehemu Barnabas Jacobo Mkuwa walifanya kazi
vizuri ya malezi kwa kuwasomesha watoto
wake wote, ndiyo maana aliishi maisha marefu yenye faraja kwa sababu ya
kuwapatia elimu watoto wake.
Aliongeza kuwa wazazi wa jana, leo na kesho wakumbuke kuwa
kazi ya malezi ni jukumu la uhai wote, hivyo basi wazazi wakumbuke kuwa samaki
mkunje angali mbichi, kwa sababu jinsi watakavyo walea watoto wangali wadogo
ndivyo watakavyofarijika zaidi baadaye na kuyaona matunda mema ya watoto wao.
Kwa upande wake Fr. Lucius OSB ambaye pia Priori Mstaafu wa
Abasia ya Peramiho kwa niaba ya jamii ya Abasia ya Peramiho alitoa shukurani kwa ukoo wa familia ya Mkuwa kwa kutoa mchango
mkubwa kwa kuendeleza umissionari hapa Peramiho tangu kuanzishwa kwake miaka
114.
Alisema kuwa ukoo wa Mkuwa ulikuwa bega kwa bega kwa kuhakikisha
maendeleo ya Abasia ya Peramiho kwa hakikisha kuwa umisionari hapa Peramiho unakuwa na kusimama imara.
Wakati huohuo, wabunge wa Mkoa wa Ruvuma kwa kupitia
mwenyekiti wa wabunge wa Mkoa wa Ruvuma, Jenister Mhagama wametoa rambirambi ya
shilingi laki tisa (900,000/-) kwa mbunge mwenzao, Devote Likokola kwa kufiwa
na baba yake mzazi.
Marehemu Barnabas Mkuwa alizaliwa tarehe 23.04.1923 hapa Peramiho,
ameacha watoto saba wote wakike, wajukuu 36 na vitukuu 31. Alifariki dunia
tarehe 13.03. 2014 katika Hospitali ya Mtakatifu Joseph Peramiho kwa ugonjwa
shinikizo la damu na kuzikwa katika makaburi ya Namihoro Peramiho.
Marehemu Barnabas alibatizwa tarehe 27.04.1923, alipata
Kumunio ya Kwanza tarehe 25.06.1931. Kipaimara tarehe 28.05.1934 na alifunga
ndoa na Isabella Mukaranga ambaye pia ni marehemu mnamo tarehe 10.06.1943 katika
Kanisa la Peramiho.
Alianza kazi ya ualimu mwaka 1942 na kustaafu mwaka 1978 ambapo wakati wa uhai wake alifundisha
shule mbalimabli za msingi zikiwemo Likuyufusi, Ndilima, Namabengo, Lilambo, Parangu,
Mtyangimbole, Tukuyu, Liganga, Lipaya na Peramiho zote za Mkoa wa Ruvuma.
Mwisho