Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Wilaya ya
Ludewa mkoani Iringa Bi. Georgina Bundala ameitaka Halmashauri ya Wilaya hiyo
kutunga sheria ndogondogo (by laws) ili kujipatia mapato kupitia watafiti na
wachimba madini wanaoingia wilayani humo kila kukicha.
Bi Georgina aliyasema
hayo jana ofisini kwake alipotembelewa
na mwandishi aliyotaka kujua ni nini mchango wa watafiti na wachimba madini
waliopo katika maeneo mbalimbali wilayani mwake kwa wilaya yake.
Bundala alisema
anashangaa kuona Baraza la Madiwani chini ya wabunge wawili wasomi na
wanasheria kunyamaza kimya bila kuibua mjadala kuhusu kutunga sheria ndogondogo
zitakazoingizia halmashauri yao kipato.
“Halmashuri ya Wilaya
ya Ludewa inaweza kujiongezea kipato kupitia watafiti na wachimbaji madini
waliopo katika maeneo mbalimbali kwa kutunga sheria ndogondogo zitakazo wabana
wadau hao,” alisema mkuu huyo.
Naye Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa Bw. Matei Kongo alipotakiwa na Nipashe kujibu
kwanini Baraza lake limekaa kimya katika suala zima la kutunga sheria ndogondogo
zikiwemo za kuingiza mapato kupitia watafiti na wachimba madini alisema
mchakato huo ulishafanyika na kuwasilishwa kwa waziri mwenye dhamana.
Bw. Kongo alisema siyo
sheria za madini tu zilizopelekwa kwa waziri kwa ajili ya kusainiwa bali zipo
na zingine zinazohusu masuala mengine muhimu labda mkuu wa wilaya hajawahi
kuziona.
Alto Liholelu ni
mwanasheria wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa akizungumza kwa njia ya simu
akiwa Dar es salaam, alisema tayari
waziri ameshasaini na kinachosubiriwa kuchapishwa kwenye gazeti la serikali ili
zianze kutumika.
“Mbali na makampuni
ya madini kulipa ada na ushuru mwingine kila mwaka makampuni hayo yatatakiwa
kutoa huduma mbalimbali za kijamii kama vile maji, elimu na afya,”alisema
mwanasheria huyo.
Bw. Liholelu alisema
mchakato huo ulifanyika mwaka jana na kwamba sheria zilizokwishatungwa na
kupitishwa na Baraza la madiwani ni pamoja na sheria ya ada na ushuru na mfuko
wa elimu.
Alizitaja sheria zingine
zinazotaraji kupitishwa na halmashauri kuwa ni pamoja na sheria ya kilimo na
kwamba sheria hii itadhibiti masoko ya mazao ya kilimo kwa kila kijiji kuwa na
kituo kimoja cha kuuzia na kununua badala ya walanguzi kufuata mazao shambani.