Tuesday, 5 November 2013

SHULE YA PERAMIHO INAONGOZA KIWILAYA

Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Peramiho, Jane Mkuwa. (Picha na Friday Simbaya)


Na Friday Simbaya, Songea
Shule ya Msingi Peramiho, Wilaya  Songea Vijijini mkoani Ruvuma,  imepanda na kushika nafasi ya kwanza kiwilaya kutoka nafasi ya pili mwaka jana kati ya  ya shule 89, imefahamika.
Akiongea  na MWENGE, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Peramiho,  Jane Mkuwa leo ofisini kwake alisema shule yake imepanda nafasi ya kwanza kiwilaya kati ya shule 89 ukilinganisha na mwaka jana ambapo shule hiyo ilishika nafasi ya pili.
Aidha, shule hiyo imekuwa  ya sita kimkoa kati ya shule 719 na nafasi ya 428 kitaifa kati ya jumla ya shule 15,656. Shule hiyo  ina jumla ya walimu 20 wakiwemo  walimu wa kike  kumi na tano na wakiume wa  tano.
Alisema kuwa watahiniwa waliofanya  mtihani wa kumaliza darasa la saba kwa mwaka 2013  walikuwa 33 na wote  wamefaulu, sawa na asilimia 100 ya ufaulu. Wanafunzi waliopata alama za juu kuliko wengine ni wanafunzi wawili tu, ambao ni Eberhat Selestini Komba na Faraja Elias Katulu waliopata wastani wa daraja la ‘A’.
“Tangu nimekuwa Mwalimu Mkuu katika  shule hii mwaka 2010 nikitokea Shule ya Msingi Mapinduzi, Wilaya ya Songea vijijini, mkoani Ruvuma, shule yangu imekuwa na mafanyikio makubwa. Mafanikio yote haya ni     kutokana na ushirikiano mzuri wa walimu,” alisema mwalimu mkuu.

Aliongeza kuwa mwaka 2010 na 2011 shule hiyo ilikamata nafasi ya nne kwa miaka miwili  mfululizo  kwa ufaulu wa asilimia 66. Mwaka 2012 na 2013 shule hiyo imefaulisha kwa asilimia 100, ambapo mwaka jana ilishika nafasi ya pili na mwaka huu imekamata nafasi ya kwanza mtawalia kiwiliaya.
“Ufaulu umepanda kutoka asilimia 66 mwaka 2010/2011 hadi asilimia 100 mwaka 2012/2013, ” aliongeza mkuu huyo.
Changamoto kubwa inayokabili shule ni pamoja na wazazi na walezi kusuasua kuchagia chakula shuleni kunakopelekea shuleni, kwani wanafunzi wanalazimika kwenda majumbani kula chakula na hatimaye kukosa masomo.
"Wito wangu kwa wazazi na walezi wachangie chakula cha wanafunzi ili waweze kula shuleni mchana hapa hapa, kuliko kwenda nyumbani ili kupunguza utoro na kuongeza mahudhurio kwa wanafunzi darasani," aliseam mwalimu mkuu huyo.

Wakati huohuo, imeelezwa kuwa ufaulu wa mtihani wa kumaliza darasa la saba kwa mwaka 2013 umepanda kwa masomo yote kwa asilimia 19.89 ikilinganishwa na ilivyokuwa kwa mwaka uliopita. Kwamba, wakati mwaka jana wahitimu waliopata asilimia 100 walikuwa asilimia 30.72, mwaka huu wameongezeka kuwa asilimia 50.61.
Pia, somo ambalo watahiniwa hao wamefaulu zaidi katika mtihani wao ni  Kiswahili ambapo ufaulu ni  asilimia 69.06 huku wakiwa wamefeli zaidi kwenye somo la Hisabati ambalo ufaulu upo chini kwa asilimia 28.62.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dk. Charles Msonde alisema wanafunzi 427,606 walifanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2013 huku kiwango cha udanganyifu kikizidi kudhibitiwa hivyo kupungua.
Alisema NECTA imefuta matokeo yote ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa watahiniwa 13, ambao walibainika kufanya udanganyifu kwenye mtihani au kurudia pasipo ruhusa ya Baraza. Watahiniwa waliofutiwa mwaka jana ni 293.
Alisema kati ya wanafunzi hao, 844,938 waliofanya mtihani huo wamepata alama zaidi ya 100 katika alama 250: ”Idadi hiyo ni sawa na asilimia 50.61. Kati yao wasichana walikuwa 208,227 (sawa na asilimia 46.68) na wavulana 219,379 sawa na asilimia 55.01,” alisema.
Dk. Msonde alisema katika ufanyaji wa mtihani huo, pia walikuwepo watu wenye ulemavu, ambapo wasichana walikuwa 219 na wavulana 257.
Alisema matokeo hayo yatapelekwa maeneo yote husika ili mchakato wa upangaji shule ukifanyika kwa watahiniwa wote waliofaulu mtihani huo wa kumaliza elimu ya msingi.
Kuhusu usahihishaji mitihani, Dk. Msonde alisema ili kujiridhisha na usahihi wa zoezi la usahihishaji wa kutumia mfumo wa kompyuta (Optical Mark Reader - OMR), sampuli za karatasi 20,795 za majibu ya watahiniwa wa shule 200 kutoka wilaya 48 zilichukuliwa kutoka shule za mikoa tisa ya (Iringa, Kagera, Shinyanga, Manyara, Njombe, Mbeya, Morogoro, Katavi na Tanga) na kusahihishwa kwa mkono: ”Ulinganifu baina ya alama za watahiniwa zilizopatikana kwa kusahihishwa kwa mkono na zile zilizotokana na usahihishaji wa mfumo wa kompyuta ulifanyika na kubaini kompyuta ilikuwa sahihi,”alisema.
Amesema makosa yaliyojitokeza katika karatasi zilizosahihishwa kwa mkono ni kuweka pata pale ambapo kuna kosa ama kuweka kosa pale ambapo kuna pata, makosa ambayo kwenye usahihishaji wa kutumia kompyuta hayakuwepo. Source: http://www.wavuti.com

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...