Mmoja wa wafanyakazi wa benki ya Maendeleo ya Wakulima, Geofrey Mtawa akizungumza na moja ya wadau waliotembelea banda lao katika maonyesho ya Nanenane.
Na Mwandishi wetu
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania inashiriki maonesho ya kilimo ya Nanenane kitaifa kwa mara ya kwanza mkoani Lindi mwaka huu kwa lengo la kutambulisha huduma zake kwa wadau wake wakuu, wakulima.
Katika maonesho hayo yaliyofunguliwa rasmi jana jumanne na Waziri Mkuu Mh. Mizengo Kayanza Peter Pinda, benki hiyo inatoa elimu na kujitambulisha kwa wakulima kwa kuwaelezea huduma zake zenye lengo la kuanzisha mtizamo mpya wa kukiendeleza kilimo kupitia kushirikisha wadau mbali mbali, kuangalia kila mnyororo wa thamani kwa ukamilifu wake, pamoja na kuwa na ubunifu katika kuchangia kifedha kwenye miradi ya muda mrefu, ya kati na muda mfupi kwenye sekta ya kilimo.
Akifungua maonesho hayo Waziri Mkuu Mh. Pinda, alisema kuwa Nanenane ni shamba darasa kwa wakulima kwa kuwa kupitia maonesho hayo wakulima watajifunza mbinu mbalimbali zenye kuongeza tija katika kilimo chao, na pia kujifunza wapi wanaweza kupata msaada kwa ajili ya kuinua kilimo chao sambamba na kujua namna wanavyoweza kutumia zana za kisasa ili kuongeza tija katika kilimo.