Thursday, 5 May 2016

TRA YAWAANDALIA ZAWADI NONO WAANDISHI WA HABARI WALIOSHINDA TUZO YA UANDISHI WA KODI NA MAKUSANYO YA MAPATO


Pichani ni Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Bw. Richard Kayombo, kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TRA (Kushoto) akimkabidhi tuzo pamoja na cheti mshindi wa kwanza wa tuzo ya Uandishi wa habari za Kodi na Makusanyo ya Mapato ya Serikali kwa mwaka 2015 Bi. Valeria Mwalongo katika sherehe za kutunuku waandishi bora wa mwaka zilizofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam tarehe 29 Aprili 2016

Mshindi wa pili wa tuzo ya Uandishi wa habari za Kodi na Makusanyo ya Mapato ya Serikali mwaka 2015 Bw. Nuru Hassan (kulia) akipokea cheti kutoka kwa Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Bw. Richard Kayombo (kushoto) aliyemuwakilisha Kamishna Mkuu wa TRA katika sherehe zilizofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam tarehe 29 Aprili 2016


Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tuzo za Umahiri katika Uandishi wa Habari, ambazo hutolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT), waandishi wawili wameshinda tuzo ya Uandishi wa Kodi na Makusanyo ya Mapato ya Serikali kwa mwaka 2015,


Waandishi hao wawili, Valeria Mwalongo, mwandishi wa Redio Tumaini aliyeshika nafasi ya kwanza na Bw. Nuru Hassan kutoka Afya Redio aliyeshika nafasi ya pili katika kinyang’anyiro hicho ni washiriki na washindi wa kwanza kupata tuzo hiyo ambayo imeingizwa kwa mara ya kwanza kwa kazi za mwaka 2015.


Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kutoka TRA Bw. Richard Kayombo alitoa tuzo hiyo kwa waandishi hao kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TRA katika Ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam ambako sherehe za kutunuku Zawadi zilifanyika.


Kutokana na ushindi huo Bw. Richard Kayombo amesema TRA itatoa donge nono kwa waandishi wa habari watakaoshiriki na kushinda katika kundi la uandishi wa habari za kodi na ukusanyaji wa mapato. Mshindi wa kwanza wa 2015 Bi. Valeria Mwalongo atajipatia kompyuta mpakato na wapili Bw. Nuru Hassan atajipatia simu aina ya Samsung mbali na kupata tuzo na vyeti kutoka MCT.


“Mamlaka ya Mapato Tanzania imedhamiria kuwajengea uwezo zaidi wanahabari kwa kuwaelimisha juu ya masuala ya kodi kwa kushirikiana na MCT ambao waowatawajengea uwezo juu ya uandishi bora kwaajili ya kuchochea ushindani zaidi katika kundi hili mwaka ujao kwa kazi ambazo zitaandikwa katika mwaka huu wa 2016.” Alisema Bw. Kayombo


MCT ilianzisha kundi la tuzo za uandishi wa habari za kodi na ukusanyaji mapato baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania kuomba kundi hili liingizwe katika tuzo hizo kwa kuzingatia kwamba waandishi na watangazaji wa habari wanaweza kushiriki kwa kuandika masuala ambayo yataongeza ridhaa ya kulipa kodi kwa hiari.


Sehemu ya barua ya TRA kwa MCT inasema, “TRA inatekeleza majukumu mbalimbali na mojawapo ni kuihabarisha jamii kupitia vyombo mbalimbali. TRA pekee haiwezi kufanikisha jukumu hili bila kuwashirikisha wadau ndio maana inaiomba MCT kuanzisha kundi la tuzo ya uandishi wa masuala ya kodi”


Tuzo ya kundi la uandishi wa Kodi na ukusanyaji mapato ya serikali ilijumuisha habari mbalimbali za masuala ya kodi, masuala ya ukusanyaji wa kodi, umuhimu na matumizi ya kodi hasa katika kugharimia huduma za jamii, nidhamu ya ukusanyaji na utumiaji, mianya ya upotevu wa mapato, njia za kuongeza wigo wa kodi. Nia ni kuongeza uhiari wa ulipaji kodi kwa ili kukuza mapato ya serikali


MCT ilizindua uwasilishaji wa kazi za wanahabari tarehe 12 Februari 2016 kwa makundi 22 yaliyojumuisha uandishi wa habari za Uchumi na Biashara, Michezo na Utamaduni, Mazingira, Watoto, Virusi vya Ukimwi na Ukimwi, Utawala Bora, Jinsia, Sayansi na Teknolojia, Afya ya Uzazi, Uandishi wa Uchunguzi, Elimu, Utalii na Uhifadhi, walemavu, Mpiga picha bora wa magazeti, Mpiga picha bora, Mchoraji kibonzo bora, Afya ya Uzazi kwa Vijana, Gesi, petrol, Utafiti wa Madini pamoja na habari za kodi na ukusanyaji mapato.


TRA inatoa wito kwa waandishi wote kujitokeza kwa wingi zaidi kuwania kinyang’anyiro hiki katika mashindano ya mwaka ujao ili kuendelea kupaza sauti juu ya masuala mbalimbali yahusuyo kodi na kujishindia zawadi mbalimbali zitakazotolewa kwa kipindi hicho.
“Pamoja Tunajenga Taifa Letu”

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...