KIKUNDI cha Upendo ni kikundi cha kina mama 20 walioamua
kujiunga kwa pamoja na kuanzisha mradi wa kupika pombe aina ya Wanzuki kwa ajili ya kuwezeshana
wenyewe kwa wenyewe. Kikundi hiki cha Upendo kipo katika Mtaa wa Lipinyapinya,
Peramiho ‘B’ Wilaya Songea mkoani Ruvuma.
Kinywaji baridi cha wanzuki hutengenzwa kwa kutumia maji, majani ya chai, sukari na amila na kusindikwa kwenye chupa mbalimbali zikiwemo za soda, bia na maji.
Mweyekiti wa Kikundi
cha Upendo Bi. Asumpta Luoga
alisema kuwa kikundi hiki kilianza tarehe
5 May, 2011 kikiwa na wanachama wachache
kwa mboga za majani hasa Chinese, na kwa sasa kina jumla ya wanachama 20.
“Tulianza kwa kuuza Chinese baada ya kuona kuwa mtaji
umekuwa kidogo tukaachana na biashara hiyo na kubuni biashara nyingine japo tulianza kutengeneza pombe ya kiyenyeji aina ya Wanzuki” alisema Bi. Luoga.
Pombe hii ya Wanzuki malighafi yake ni pamoja na maji, sukari, majani ya chai na amila kwa kupika mchanganiko huo kwenye moto na baada yapo kusindikwa kwenye chapa mbalimbali zikiwemo za soda, bia na makopo ya maji.
Ingawa kiwango cha alcohol bado hakijafahamika sawa sawa, pombe
hii kali kipimo chake ni kikombe cha robo lita na
kinauzwa kwa bei ya Shilingi 200/- kwa chupa.
Aidha, mwenyekiti huyo alisema kuwa kikundi chao kinaundwa na
makundi matatu muhimu kama vile waathirika wa Ukimwi, Wajane na Yatima. Alisema kuwa kinywaji baridi
aina ya Wanzuki hupikwa kwa pamoja na baada ya mauzo kupatikana mwanachama wanamtoa kwa kumpa
katika Shilingi 25,000/- hadi Shilingi 30,000/- kila baada ya siku nne. Mzinguko huu wakipeana pesa unaendelea hadi kila moja anapata mgao wake.
“Huwa tunamtoa mwanachama mmoja kwa kumpa kiasi cha 25,000/- hadi 30,000/-
kutegemea na biashara ili aweze kununua vyombo vya nyumbani na mauzo yakiwa zaidi huwa tunaweka kwenye akiba ili kutunisha mfuko. Kwa kweli kamradi ketu haka huwa kanatusaidia kidogo kidogo
kuliko kukaa tu ukilinganisha maisha kuwa magumu bila kufanya biashara hautaweza kuishi,” alisema Bi. Luoga.
Kwa upande wa Katibu wa Kikundi hicho Bi. Anitha Komba
alisema kuwa pamoja na kuwepo baadhi ya mafanikio pia kuna changamoto
mbalimbali wanazokumbana nazo kama kikundi ikiwa ni pamoja na upungufu wa vifaa kama vile madumu ya maji, chupa, viti
vya kukalia wateja, meza, radio, majiko ya kisasa na mabanda.
Alisema kikundi kinahitaji vitu kama hivyo ili viweze
kuwasaidia katika shughuli zao, kama vile majiko ya kisasa yaliyokuwa rafiki wa
mazingira ili wapunguze matumizi ya kuni, wanahitaji mabanda kwa ajili ya kuuzia biashara hiyo na radio kwa
muziki na burudani kwa wateja n.k.
“Hatuna sehemu maalum ya kuuzia biashara yetu kwa hiyo tunalazimika kupeleka kwenye vilabu vya pombe vya watu wengine lakini nasi tungekuwa na sehemu
yetu maalum tunaweza kufanya biashara yetu kwa uhuru kuliko hivi sasa
tunahangaika sehemu ya kuuzia,” alisema Katibu wa kikundi.
Aidha, Katibu huyo aliwataja wanachama kuwa ni pamoja na Agata
Mbano, Brandina Mbawala, Fausta Haule, Amina Pili, Maria Ngonyani, Jisela
Chale, Salome Nyoni na Osmundi Kayombo.
Wengine ni Rose Nyoni, Agnes Ndauka, Aifosia Mbano, Evans
Mbano, Romana Mbilo, Mage Kayombo, Avena Mahundi, Charles Ponela na Sebestian
Nyoni.
Naye Mweka Hazina wa Kikundi cha Upendo, Bi. Joyce Kunguru
alisema kuwa mpaka sasa kikundi kina akiba ya shilingi 25,000/- tu, na wanaomba wafadhili mbalimbali wajitokeze ili waweze kuwasaidia ili waweze
kupanua biashara yao pamoja na kuongeza wanachama.
“Tunaomba wafadhili waweze kusikia kilio chetu kwa kutusaidia
katika kutuwezesha ili tuweze kuongeza mtaji wetu na hatimaye tuweze kuongeza
wanachama wengi zaidi. Kama unavyojua mwanamke ni nguzo kuu katika familia na mzalishaji mkuu pia, kwa
hiyo akiwezeshwa anaweza kupunguza umaskini wa kipato,” alisema Bi. Kunguru.