Haya ni maneno ya Jackline Masisa (17), aliyekatiza masomo akiwa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Mondo wilayani Kishapu, baada ya kupewa mimba na mwalimu wa shule jirani na mahali alikokuwa anapata huduma ya masomo ya ziada au tuisheni.
“Akimaliza kunifundisha, alikuwa ananishikashika na kunivua nguo, kisha kunilaza…” anaendelea kusimulia Jackline, akimueleza mwalimu huyo mwenye umri wa miaka 30 (jina linahifadhiwa).
Anasema mwalimu huyo alimshawishi kuingia katika masomo ya ziada, yaani tuisheni, lakini baada ya muda wakageukia mapenzi.
Jackline anakiri alizamishwa katika mapenzi na mwalimu wake kwa ushawishi wa ‘posho’ ya Sh. 5000 na matokeo yake, hivi sasa ana mtoto mwenye miaka miwili analelewa na wazazi wake, baada ya mwalimu aliyempa mimba kumkana.
Ilikuwaje baada ya wazazi kugundua yu mja mzito? Kwanza anaanza kusema namna alivyoingia katika maisha mapya ya ujauzito.
Bila ya kujitambua ana hali gani wakati huo , Jackline anasimulia, huku akionyesha ishara ya aibu kwa kuangalia chini na kung’ata vidole. Anatamka: “Nilianza kujisikia vibaya, sikujua ni nini. Kumbe nina mimba...”
Anasema katika mazungumzo shuleni, aliwasikia wenzake shuleni wakimhisi huenda ana mimba na akaamua kwenda kununua vipimo vya kugundua mimba.
Jackline anasema aligundua namna ya kubaini mimba kwa msaada wa maarifa aliyopewa na wasichana wenzake shuleni.
Kwa mujibu wa Jackline, wakati huo uhusiano wake na mwanaume wake- mwalimu, ulishaishia katika mazingira ya kutatanisha. (Huenda mwalimu aligundua mabadiliko)
Anasema wakati wote shuleni kwao hawakugundua chochote, bali nyumbani wazazi wake, hasa mama yake alimgundua kwa mabadiliko yake kiafya na ukubwa wa tumbo.
Jackline ambaye ni mzito wa kuzungumzia sakata hilo, anakumbuka tukio la mama yake kubaini hali yake, kwamba alimgombeza sana, huku baba yake alibaki kimya hadi leo kuhusdiana na sakata hiyo.
Huo ndio ukawa mwisho wa safari yake kwenda shule na baba yake ameendelea kubaki kimya kuhusiana na sakata hilo, lakini katika familia baadhi ya ndugu zake walionyesha chuki dhidi yake kutokana na kitendo hicho.
Jackline anfafanua: “Kwa kuwa sikuwa na mbadala kwamba niende wapi, nilikaa tu nyumbani hadi nikajifungua. Mpaka sasa mama anamlea mwanangu, kwa kuwa mimi nipo shule ya bweni,”
Kwa sasa Jackline baada ya kujifungua, anasoma kidato cha pili kwenye shule iliyo chini ya asasi ya Agape, iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga, ambayo ni mahsusi kwa wasichana waliopoteza fursa za masomo yao.
Kulingana na mila za jamii ya mkoa wa Shinyanga, kama zilivyo jamiii nyingi za Kiafrika, mtoto hupatiwa jina la pili (ubini) la baba yake.
Licha ya kuwapo mila hizo, Jackline ambaye anasema hakumtaja baba wa mtoto kwa wazazi wake, bila ya kutoa sababu za kumficha mzazi wake, anafafanua kuhusu majina ya binti yake kwa kauli:
“Jina la ubini wangu ni Masisa, mwanangu wamempa ubini wa baba yangu, kutokana na mwanaume aliyenipa mimba kutoonekana na malezi ni ya wazazi wangu tu.”
Jackline ni miongoni mwa wasichana 8,000 wanaopata ujauzito kila mwaka nchini. Kati yao wamo wanafunzi wa shule za sekondari 5,000 na shule za msingi 3,000.
Ripoti ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, inaeleza juhudi za serikali katika kuondoa tatizo hilo kwa kutumia mbinu mbalimbali.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), mwanzoni mwa mwaka huu, lilisema Tanzania ni miongoni mwa vinara wa ndoa za utotoni.
UNFPA inataja mikoa inayoongoza kwa ndoa za utotoni ni Shinyanga, Tabora, Mara, Dodoma, Lindi, Mbeya, Morogoro, Singida, Manyara, Mtwara, Pwani, Arusha, Kilimanjaro, Kigoma, Dar es Salaam na Iringa.
Takwimu za UNFPA zinaonyesha kuna watoto 13,822 waliozaliwa kati ya mwaka 2005 na 2010, ifikapo mwaka 2030 watakuwa wameolewa wakiwa na umri wa chini ya miaka 18, iwapo kasi iliyopo haitadhibitiwa.
Hayo yanatokea huku kukiwapo vigezo vya kijamii na kisheria katika kukabiliana na hali hiyo. Miongoni mwake ni Sheria ya Mtoto na Sheria ya Makosa ya Kujamiiana, ambazo zinamlinda msichana.
Mbali na hiyo, kuna kampeni na harakati za kuwalinda wasichana zinazofanyika kupitia nyenzo mbalimbali kama vile vyombo vya habari na vikundi vya kijamii.
Shinyanga ambayo ni mkoa anakotoka Jackline, kumeshamiri matukio hayo, huku mzazi huyo mwenye mtoto wa miaka miwili aking’aka kwa lugha kali ya majuto akisema:
“Hatua kali zaidi zichukuliwe dhidi ya mafataki wanaowakatisha masomo watoto wa kike, kwani wanadumaza mchango wa wanawake katika maendeleo ya nchi yao.”
Kulingana na mila, desturi za waafrika wengi ikiwamo Tanzania, jina la pili la mtoto akishazaliwa huitwa ubini wa baba.
Lakini hii ni tofauti na kwake Jackline kwani wazazi wake wamempa mtoto wake ubini wa baba yake na kumuita Ritha Masisa.
“Jina la ubini wangu ni Masisa, mwanangu wamempa ubini wa baba yangu kutokana na mwanaume aliyenipa mimba kutoonekana na malezi ni ya wazazi wangu tu,” anasema.
OFISA ELIMU MKOA
Ofisa Elimu Taaluma Sekondari mkoani Shinyanga, James Malima, anasema mkakati uliopo sasa katika shule za sekondari ni kuwapima mimba kila baada ya miezi mitatu wanafunzi wa kike.
Pia anasema kuna mkakati wakuwekwa vituo vya ushauri kuhusu afya ya uzazi, vitakavyowasaidia wanafunzi wajitambue, mara baada ya kupevuka.
Kauli ya Agape
Mkurugenzi Mkuu wa asasi ya Agape iliyopo mkoani Shinyanga, John Myola, ambaye taasisi yake inajishughulisha na kutoa elimu kwa wasichana waliokatizwa masomo, anasema changamoto kubwa na sababu ya kuendelea kwa mimba hizo ni kukithiri kwa rushwa, vyombo vya maamuzi ikiwamo mahakama kushindwa kutoa maamuzi haraka.
Anasema ukosefu wa wanasheria wa kutafsiri sheria kwa familia za waathiriwa wa mimba pamoja na ushirikiano mdogo wa jamii uliopo katika jamii katika kukomesha tatizo hili.
Anasema wazazi, walezi baadhi yao hawathamini elimu kwa mtoto wa kike na kuona kuwa mtoto wa kike ni wa kuolewa tu na kwamba mwaka 2014 katika shule ya sekondari Kituli, iliyopo wilaya ya Shinyanga wanafunzi 14 waliozeshwa.
UTATA WA SHERIA
Sheria, sera na matamko kadhaa zinaliwekwa ili kulinda watoto na haki yao, ikiwa ni pamoja na kupata elimu, hasa kwa upande wa mtoto wa kike bado anakabiliwa na kadhia nyingi, ikiwamo kupata mimba katika umri mdogo.
Hilo linafanya ndoto yake ya kupata elimu kwa kiwango cha juu ifutike. Inaelezwa kuwa matokeo ya ulegevu katika usimamizi wa sheria, sera na matamko ya serikali, ni tatizo.
Mathalan, Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 ambayo pamoja na inatoa ulinzi kwa taasisi ya ndoa, kwa miaka takriban 45 imekuwa na mapungufu ya kuruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa umri chini ya miaka 18.
Taasisi ya Msichana Initiative ilifungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Shauri Namba Tano ya mwaka 2016 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikihoji uhalali wa kikatiba wa kifungu cha 13 na 17 cha Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971.
Hicho ndicho kifungu cha sheria hiyo, inayoidhinisha mtoto wa kike mwenye kati ya miaka 14 na 15 kuolewa kwa idhini ya mzazi au mahakama.
Mahakama Kuu iliamuru vifungu hivyo vifutwe, kwani vinakinzana naKatiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inayoruhusu kumuoza mtoto chini ya umri huo ni kuvunja sheria.
Hivi karibuni serikali imekata rufaa kupinga huku hiyo, lengo ni kwamba maamuzi ya mwisho yafanywe na mahakama ya juu zaidi ambayo ni Mahakama Kuu ya Rufaa, ili kusiwapo mahakama nyingine ya kuhoji uamuzi huo.
“Kinachofanyika ni utaratibu wa kawaida ambao utaiwezesha serikali kuwa na uamuzi kutoka katika chombo cha juu kabisa cha mahakama nchini,” anasema Dk. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Sheria na Katiba.
Kuna wakati, wanaharakati na vyama vya kutetea utu wa mwanamke, ikiwamo Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), walishinikiza na kukatungwa Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ya Mwaka 1998.
Sheria hiyo ilirekebishwa mwaka 2002, kwa baadhi ya makosa kufafanuliwa zaidi katika Sheria ya Kanuni ya.
Kwa mfano kosa la kubaka lilifafanuliwa zaidi na suala ridhaa liliondolewa kabisa, kama kosa la kubaka litafanyika dhidi ya mtoto mwenye chini ya miaka 18.
Pia mwaka 2009, ilitungwa Sheria Mtoto, ambayo imejikita katika kumlinda mtoto dhidi ya vitendo vya ngono navinavyofana nayo.
Kimsingi, Sheria ya Mtoto inasimamia mambo mengi ya kitaifa yanayohusuhaki na ulinzi wa mtoto, ingawaje utekelezaji wake ni changamoto.
Ni sheria inayojumuisha mikataba ya kimataifa, ambayo Tanzania imeridhia inamakubaliano mbalimbali ya kimataifa yanayohusu haki za mtoto, vilevile kutoka Sera ya Taifa ya Watoto.
Muundo wa sheria hiyo umelenga kumpa mtoto kinga na haki. Vipengele vinajumuisha watoto kuhitaji matunzo nje ya makazi yao na wasiajiriwe.
Haki za mtoto katika Tanzania Bara zinalenga mengi, kama vile kulelewa na wazazi wake, kupewa jina, utaifa, na kupata mahitaji ya msingi kama vile chakula, malazi, mavazi, matibabu, kucheza na kuburudika.
Pia, kuna wajibu wa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi; wanapelekwa kwenye chanjo, huduma za afya, wanaandikishwa shuleni, wanafuatiliwa maendeleo ya shule, wanasikilizwa na kupewa miongozo na matunzo.
WANAHARAKATI
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi inayojishughulisha na Utetezi na Ulinzi wa Watoto ya Nexgen, Jacob Kahemele, anasema serikali inapaswa kutofumbia macho suala hiloili kudhibiti unyanyasaji, ukatili, ndoa za utotoni na ubakaji wa watoto nchini.
Anasema taarifa iliyotolewa katika Bunge la Bajeti mjini Dodoma mwaka huu na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Mwakyembe, kwamba tangu mwezi Januari mwaka huu, kuna kesi zaidi ya 2000 zilizoripotiwa kuhusu ubakaji na ukatili wa watoto.
Kahemele anawahimiza wadauwa haki za binadamu, watetezi wa haki za mtoto na viongozi wa serikali, kushinikiza hatua za kisheria zichukuliwe.
LHRC
Tathmini ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kipindi cha miezi sita mwaka huu, ni kwamba kuna kesi za ubakaji wa watoto 1,491 katika kipindi hicho.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Hellen Kijo-Bisimba, anasema haki za watoto zimekuwa zikikiukwa, licha ya kuwapo sheria mbalimbali. Ombi lake kwa serikali ni kwamba ichukue hatua haraka.
Mdau wa kimataifa, Mwalimu Brendan Callaghan kutoka Shule ya Watakatifu Wote ya Anglikana - Australia, anasema uzoefu wa nchi yao, kwamba wako makini katika kumlinda mtoto apate haki zake za msingi.
Anajigamba kuwa, Australia ni moja ya nchi zinazoongoza duniani katika kuweka mikakati, kanuni na sheria makini za kumlinda na kumtetea mtoto.
WIZARA YA AFYA
Waziri wa Afya Maedeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema wanaume wanaoendelea kuwapa mimba wasichana walio chini ya miaka 18, wajiandae kujaa kwenye Magereza, mara baada ya muswada wa marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971, kufikishwa bungeni Septemba mwaka huu na kufanyiwa marekebisho.
Aidha, anasema uamuzi uliotolewa Mahakama Kuu na kuamuru vifungu viwili vya 13 na 17 vya sheria hiyo, vifutwe kwa kuwa viko kinyume cha Katiba ambayo inatamka kuwa umri wa mtoto ni hadi miaka 18 na kuolewa katika umri huo, utawalinda watoto ambao wanakumbwa na masuala hayo.
Mwalimu anasema kuwa takwimu za elimu zinaonyesha kati ya wasichana 1000 waliopo shuleni kunazuia vifo vya uzazi vya wasichana wawili kila mwaka.
Anasema elimu ya watoto wa kike ni moja ya njia bora ya kupunguza umaskini katika mataifa yanayoendelea na matokeo hayo yanaweza kuonekana kwa watu, binafsi, famulia zao, na jamii kwa ujumla.
“Elimu inafaida ya kuchelewesha ndoa na ujauzito kwa wasichana wadogo, unaosababisha vifo vingi vya uzazi hususa kwa walio na umri kati ya miaka 15 hadi 18”.
“Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030 unyanyasaji na ukatili kwa mtoto wa kike unatokomezwa, ikiwamo ukeketaji, ndoa za utotoni na mimba,” anasema Mwalimu.
UNFPA
Aliyekuwa Mwakilishi Mkazi wa shirika la UNFPAhapa nchini, Dk. Natalia Kanem, anasema: “Ni muhimu kuwekeza kwa wasichana wadogo, hususan katika masuala ya utoaji taarifa sahihi kuhusu Afya ya Uzazi na kutoa huduma za Afya ya uzazi na Ukimwi, kwa kufanya hivyo itawawezesha wasicha kufikia malengo.”
Anaongeza kuwa UNFPA kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), wamefanya utafiti na kubaini mimba za utotoni zimeongezeka.
Ofisa Programu waMasuala ya Afya ya Uzazi kwa Vijana wa UNPA, Fatina Kiluvia, anasema wasichana wenye umri kati ya miaka 13 na 19, wana changamoto kubwa ya maisha.
Dk. Albina Chuwa, Mkurugenzi wa NBS, anasema asilimia 23 ya wasichana nchini hupata mimba, jambo linalorudisha nyuma uchumi na maendeleo ya nchi.
“Tunatarajia uchumi wa viwanda kama ilivyoazimia Serikali ya Awamu ya Tano. Lakini idadi hiyo, maana yake ni kwamba tutakosa wasomi ambao wangesaidia kukua uchumi kwa namna moja au nyingine,” anasema Dk. Chuwa. (SOURCE: NIPASHE)