Na Friday Simbaya,
Ludewa
IKIWA imebaki siku moja tu kuanza kwa mtihani wa Taifa wa Kidato cha nne nchini mwanafunzi Hosana Raaban wa Shule ya Sekondari Ulayasi Ludewa mkoani Iringa ametimuliwa shule baada ya kukamatwa na walimu wake akifanya mapenzi na mwanaume vichakani kinyume na sheria za shule.
Mwanafunzi Hosana Raaban (20) anayetoka katika Kijiji cha Ligumbilo katika Kata ya Mlangali alikutwa na mkasa huo Oktoba 2 mwaka huu katika vichaka vinavyoizunguka shule hiyo baada ya kuwatoroka walimu waliokuwa wakisubiri kwa vifaa vya mitihani shuleni hapo tayari kwa mtihani kesho yake.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bw Richard Chitundu akizungumza kwa njia ya simu alikiri kutokea kwa fumanizi hilo vichakani majira ya saa kumi na moja jioni na kukiri kosa na kutakiwa kufika kesho yake akiwa ama na mzazi au mlezi wake ili kupata ufumbuzi wa suala hilo, lakini mwanafunzi na wazazi wamekaidi agizo hilo.
Akielezea tukio lenyewe Bw Chitundu alisema Oktoba 2 mwaka huu majira ya saa kumi na moja wanafunzi na walimu wakiwa shuleni kusubiri vifaa na mitihani mwanaume mmoja alionekana kulandalanda maeneo ya shule na baada ya muda mfupi Hosana Raaban alitoweka na ndipo aliingia hofu na kuwatuma walimu watatu kufuatilia nyendo zake.
Alisema walimu hao walipanda juu ya mti na kushuhudia laivu wahusika wakikumbatiana na ndipo walishuka kama mwewe na kufanikiwa kuwatia mbaroni, lakini mwanaume alifanikiwa kuwatoka na kutokomea vichakani na hadi sasa hajakamatwa na mwanafunzi amekataa kumtaja.
“Mtoto alipohojiwa alisema ni kweli alikubaliana na mwanaume huyo ambaye hakumtaja jina ili waende kufanya mapenzi vichakani ili aweze kumpa simu yake ya mkononi aliyochukua,” alisema Bw Chitundu kwa masikitiko makubwa.
Chitundu alisema kufuatia tukio hilo wazazi wake walijulishwa na kuagizwa wafike kesho yake Oktoba 3, lakini walikaidi agizo hilo. Hata hivyo, binti Hosana hakujutia kitendo badala yake alionesha dharau kwa walimu kama vile ni haki yake kufanya alichokifanya.
Habari kutoka kwa wanafunzi wenzake zinasema siku ya kufa nyani miti yote huteleza na kwamba wao hawamshangai mwenzao kukamatwa siku moja kabla ya Mtihani wa Taifa kwani ni muda mrefu amekuwa akituhumiwa kuwa na mahusiano na waume za watu siku za nyuma, lakini hakuwahi kukamatwa.
Mmoja wa wanafunzi hao ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini alisema kuwa Hosana amefanya kitendo hicho makusudi kukwepa (paper) mtihani kwa sababu hata uwezo katika masomo alikuwa mvivu hakuwa na malengo wala nia na shule.
Akizungumza ofisini kwake Afisa Elimu wa Sekondari wilayani Ludewa Bw Emanuel Mlelwa alikiri kuipokea taarifa hiyo na kusema kuwa mwanafunzi Hosana Raaban baada ya kukamatwa na kosa hilo hakufukuzwa shule isipokuwa alitakiwa kufika siku ya pili na mzazi au mlezi wake lakini alikaidi.
“Katika hali ya kawaida na uungwana kama Hosana angefika kesho yake shuleni angeruhusiwa kufanya mtihani wake wa kuhitimu kidato cha nne sasa kwa kuwa hakurudi, basi hatuna jinsi inawezekana alifikwa na aibu,” alisema Bw Mlelwa.
Akitoa takwimu za watahiniwa wilayani kwake Bw Mlelwa alisema wanafunzi waliosajiriwa kwa wilaya nzima ni 1,682 wavulana wakiwa 916 huku 766 wakiwa wasichana tofauti na mwaka jana ambapo waliosajiriwa walikuwa 1,631 wavulana wakiwa 868 na wasichana wakiwa 763.
Bw Mlelwa hata hivyo kwa mwaka jana watahiniwa waliofanya mtihani walikuwa 1,565 wavulana wakiwa 829 na wasichana 735 sawa na asilimia 99 huku idadi ya waliokosa kufanya mtihani kwa sababu mbalimbali ikiwepo mimba, utoro na kufukuzwa ikifikia 66 wavulana 36 wasichana 30 sawa na asilimia 4.
Wilaya ya Ludewa ina shule za Sekondari kumi na tano (15) zilizofikia kidato cha nne 13 zikiwa za serikali na shule mbili zikiwa zinamilikiwa na Jumuia ya wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
MWISHO.