Mgombea Daudi Masasi aliyepata kura 21, agoma kusani matokeo kutokana na alichodai kuwa hajaridhishwa na mchako.
Mgombea Chiku Abwao aliyepata kura 25, akisani matokeo.
ALIYEKUWA Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chiku Abwao ameshinda kura za maoni za chama cha ACT Wazalendo ikiwa ni siku chache toka ajiunge na chama hicho.
Ushindi mwembamba wa kura 25 alizopata dhidi ya mgombea mwenzake Daudi Masasi aliyepata kura 21, umemuweka katika nafasi ya kuteuliwa na chama chake hicho kipya kuwania ubunge wa jimbo la Iringa Mjini katika Uchaguzi Mkuu wa baadaye mwaka huu.
Kabla ya kujiunga na ACT Wazalendo, Abwao alipania kugombea ubunge katika jimbo la Isimani kupitia Chadema, lakini kwa kile alichoita hila zilizokuwa zikifanywa dhidi yake na mbunge wa jimbo la Iringa Mjini anayemaliza muda wake, Mchungaji Peter Msigwa ndoto yake hiyo imekoma.
Kabla ya kushinda kura hizo za maoni Abwao alisema Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe anatarajia kuja mjini Iringa Jumapili Agosti 9 kwa lengo la kumtambulisha rasmi kwa wakazi wa mjini Iringa.
Alisema Kabwe atakayeambatana na aliyekuwa Mbunge wa Kasulu, Moses Machali na Afande Sele na viongozi wengine wa ACT atafanya mkutano mkubwa katika viwanja vya Mwembetogwa jumapili hiyo.
Wakati, aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Kalenga kupitia chadema Mwanahamisi Muyinga ameshinda kura za maoni za kugombea ubunge katika jimbo hilo kupitia chama cha ACT Wazalendo kwa kupata kura zaidi 20.
Mwanahamisi aliwashinda wagombea wenzako watatu na kutangazwa mshindi katika uchaguzi wa kura za maoni uliyofanyika leo.
Hata hivyo, Mwanahamisi wamewashukuru wajumbe kwa kumpingia kura pamoja na wale ambao hawakumpigia kura na kuwaomba washirikiane katika kuleta maendeleo katika jimbo la Kalenga.
Wakati huohuo, Mwanahamisi amesema atachukua fomu pia ya kuwania ubunge viti maalum kupitia chama hicho kupitia jimbo la kalenga.