Thursday, 17 November 2016

WANANCHI KILOLO WATAKA SERIKALI IWAPATIE CHETI CHA ARDHI YA KIJIJI






KILOLO: WANANCHI wa kijiji cha Mawala, kata ya Irole katika Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa wameitaka serikali wilayani humo kuharakisha upimaji wa maeneo ya ardhi ya kijiji chao pamoja kupatiwa cheti cha ardhi ya kijiji ili kupunguza migororo mbalimbali iliyopo kwa sasa.

Wakizungumuza jana katika mdahalo walisema serikali kwa kutumia sheria ya ardhi ya vijiji itenge maeneo kwa ajili ya wakulima na wafugaji hatua itakayosaidia makundi hayo kuepukana na migogoro kwa kuwa makundi yote mawili yanategemeana.

Mdahalo huo uliozungumzia namna ya kuondoa migogoro ya ardhi ya kijiji uliandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Grassroots
Oriented Development (TAGRODE) yenye makao yake makuu mjini Iringa kwa shirikiana na PELUM Tanzania.

Wakichangia mada, wakazi hao wa Kijiji cha Mawala walisema migogoro ya ardhi katika maeneo yao itakoma kama serikali itasimamia kwa nguvu zake zote utekelezaji wa sheria za ardhi hatua ambayo pia itaimarisha amani na utulivu na kuleta tija kwa jamii.

kijiji cha Mawala kina vitongoji viwili ambavyo Mawala ‘A’ na ‘B’ hakina cheti cha ardhi ya ardhi ya kijiji hivyo wameiomba serikali iwapatie cheti hicho ilikuweza kuondoa migogoro ya mipaka baina vijiji inavyopakana navyo.

Naye mratibu wa Shirika la TAGRODE, Dickson Mwalubandu alisema shirika hilo linaendesha midahalo hiyo katika vijiji vya Ikuka, Mbigili, Mawala, Mawambala na Masalali kwa wilaya ya kilolo na vijiji vya Usokami, Ugesa, Makungu, Magunguli na Isaula wilaya ya Mufindi kupitia mradi wake wa CEGO unaohusisha jamii ya vijijini katika uwajibikaji wa masuala ya ardhi ya kijiji.

Alisema kuwa kwa ufadhili wa shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (USAID) kupitia shirika la PELUM Tanzania wanaendesha midahalo katika wilaya mbili za Mufindi na Kilolo mkoani Iringa.

Kwa upande wake Afisa Mradi kutoka mtandao wa Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali yanayofanya kazi na wakulima na wafugaji wadogo nchini Tanzania (PELUM Tanzania) Angolile Rayson alisema, asilimia kubwa ya migogoro yote ya ardhi wilayani Kilolo mkoani Iringa, inatokana na ugomvi wa mipaka katika maeneo ya vijijini.

Rayson alisema kuwa midahalo inayofanywa katika wilaya hizo inalenga kutafuta mambo yakufanya ili kupunguza malalamiko ya migogoro ya ardhi.

Alisema kuwa Kwa ufadhili wa shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (USAID), mtandao huo ulitoa mafunzo ya haki za ardhi na utawala katika vijiji vyote vya mradi.

Alisema kuwa ili kuhakikisha wananchi wanakabiliana na changamoto hiyo shirika lake lilitoa elimu, na kuimarisha kamati za ardhi za vijiji na mabaraza ya ardhi ya vijiji ili yaweze kutatua migogoro pindi inapojitokeza kwenye maeneo yao.

Rayson alisema mafunzo hayo ya haki za ardhi na utawala yanalenga kuwaongezea wananchi wa wilaya hizo uelewa juu ya sheria za ardhi, haki za ardhi kwa wanawake na makundi maalum pamoja na utatuzi wa migogoro ya ardhi.
Afisa Mradi wa PELUM Tanzania huyo alisema shirika lake limeamua kufanya kazi hiyo kwa lengo la kusaidia kukuza uelewa wa wananchi juu ya ya haki zao kwa masuala yahusuyo ardhi na mbinu za kukabiliana nayo ili kupunguza tatizo hilo nchini.

Alisema kwa sasa mradi huo unatekelezwa katika vijiji 30 vilivyopo katika wilaya sita za mikoa mitatu ya Tanzania bara ambayo ni Morogoro, Dodoma na Iringa.

Hata hivyo, Afisa Mipango Miji na Vijiji Wilaya ya Kilolo, Bernard Kajembe alisema kuwa halmashauri ya wilaya kilolo ina vijiji 30 vilivyo na mpango wa matumizi bora ya ardhi kati ya vijiji 95 vya wilaya hiyo.

Alisema kuwa kwa shirikiana na shirika la Pelum Tanzania halmashauri hiyo wanaanda mpango wakuongoza vijiji vingine kupelekewa mpango huo wa matumizi bora ya ardhi ili kupunguza migogoro ya ardhi wilayani humo.

WAZIRI NCHEMBA AZUKA IDARA YA NIDA



Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza kikao chake na Menejimenti ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) wakati alipofanya ziara ya kikazi Makao Makuu ya NIDA, Kinondoni, jijini Dar es Salaam leo. Mwigulu aliwaambia waandishi wa habari kuwa, NIDA itaanza kutoa namba za utambulisho kwa wananchi wote kuanzia mwezi Desemba mwaka huu, ambao wamesajiliwa kupitia mpango wa usajili wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Andrew Massawe.


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Andrew Massawe (watano kushoto) akimuelezea jambo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba (katikati) wakati Waziri huyo alipotembelea Makao Makuu ya Mamlaka hiyo, Kinondoni, jijini Dar es Salaam leo. Kiongozi huyo wa NIDA katika hotuba yake fupi kwa Waziri Mwigulu, alisema kuwa, NIDA itaanza kutoa namba za utambulisho kwa wananchi wote kuanzia mwezi Desemba mwaka huu, ambao wananchi hao wamesajiliwa kupitia mpango wa usajili wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). 



Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba (kushoto) akimsikiliza Kaimu Mkurugenzi wa Mifumo ya Kompyuta (TEHAMA) wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Mohamed Khamis (wapili kushoto) alipokuwa akielezea jinsi wanavyosajili taarifa mbalimbali za waombaji wa vitambulisho. Waziri Mwigulu alitembelea Kituo hicho cha Usajili na kujifunza kazi mbalimbali zinazofanywa na NIDA, jijini Dar es Salaam leo. Watatu kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Andrew Massawe. 



Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Andrew Massawe (wapili kushoto-mbele) akimsindikiza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba (kushoto mstari wa mbele) mara baada ya Waziri huyo kumaliza ziara yake ya kutembelea ofisi za NIDA Makao Makuu na ofisi zake za usajili wa taarifa mbalimbali za waombaji wa vitambulisho, zilizopo jijini Dar es Salaam. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

HATIMAYE MPEMBA WA MAGUFULI ABURUZWA MAHAKAMANI,NI YULE JANGILI WA MENO YA TEMBO



Hatimaye Vinara wanaodaiwa kujihusisha na mtandao wa kukusanya, kuuza vipande 50 vya meno ya tembo, vyenye thamani ya Sh. milioni 392.8 wamepandishwa katika mahakamani wakikabiliwa na mashtaka manne ya kuhujumu uchumi akiwamo, Yusuf Ali maarufu kama Shehe ama "Mpemba" (35).

Mbali na "Mpemba", washtakiwa wengine n mfanyabiashara mkazi wa Mrimba, Mkoani Morogoro, Charles Mrutu maarufu Mangi Mapikipiki ama Mangi Mpare (37), wakazi wa Dar es Salaam, Benedict Kungwa (40) Jumanne Chima maarufu Jizzo ama JK (30), Pius Kulagwa (46) na Dereva wa Vikindu, Pwani Ahmed Nyagongo (33).

Washtakiwa wote walisomewa mashtaka yao leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.Wakili wa Serikali Paul Kadushi, alidai kuwa kati ya Januari, mwaka 2014 na Oktoba, mwaka huu maeneo tofauti Mkoani Dar es Salaam, Morogoro, Iringa, Tanga na Mtwara washtakiwa wakiwa na wenzao ambao bado hawajashtakiwa mahakamani, walijihusisha na matukio ya uhalifu.

Ilidaiwa pia, washtakiwa walijihusisha kukusanya, kuuza vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola za Kimarekani, 180,000 (sawa na Sh. 392,817,600) mali ya Serikali ya Tanzania, bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Upande huo wa Jamhuri ulidai katika shtaka la pili, Oktoba 26, mwaka huu eneo la Mbagala Zakhem Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, washtakiwa walikutwa na vipande 10 vya meno ya tembo vikiwa na uzito wa kilo 13.85 vyenye thamani ya Dola za Kimarekani, 30,000 (sawa na Sh. 65,469,600) mali ya Serikali ya Tanzania, bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Shtaka la tatu na la nne, ilidaiwa kuwa kati ya Oktoba 27 na 29, mwaka huu na eneo la Tabata Kisukulu, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, washtakiwa walikutwa na vipande 40 vya meno ya tembo vikiwa na uzito wa kilo 69.56 vyenye thamani ya Dola za Kimarekani 150,000 (sawa na Sh. 327,348,000) mali ya Serikali ya Tanzania, bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Kadushi alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kwamba Jamhuri inaandaa nyaraka mbalimbali ikiwamo maelezo ya mashahidi pamoja na vilelezo kwa ajili ya kuwasilisha taarifa katika Mahakama Maalum ya kesi za Kuhujumu Uchumi na Rushwa (mafisadi).

Hakimu Simba alisema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama yake haina mamlaka ya kusikiliza kesi za kuhujumu uchumi.

Kesi hiyo itatajwa Desemba Mosi, mwaka huu na washtakiwa wamepelekwa mahabusu.

POMBE FEKI ZA VIROBA ZALITESA TAIFA,WAZIRI WA MAGUFULI AKIFUMA KIWANDA BUBU



Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla, akiwa ameongzana na timu ya Serikali yenye wataalamu na wanausalama wameendesha operesheni kali ya kusaka viroba feki na pombe nyingine haramu katika maeneo ya Jiji la Dar es Salaam na kufanikiwa kukama shehena kubwa ya bidhaa hizo feki na haramu kwenye maeneo hayo.


Katika operesheni hiyo, pia wamefanikiwa kukibaini kiwanda bubu kinachotengeneza kinywaji aina ya konyagi na Smirnoff feki maeneo ya Sinza Jijini Dar es Salaam. 

Kiwanda hicho kinatengeneza vinywaji hivyo kwa kutumia ‘spirit’ ambayo inachanganywa na ‘gongo’; spirit, gongo, chupa tupu na zilizojazwa, vizibo, vifungashio vimekamatwa.


Kwa hatua hiyo Jeshi la Polisi linawashikilia watu wawili ambao inasemekana wanafanya kazi pamoja na bwana Yusuf Abdul Kalambo, ambaye anatafutwa na polisi mpaka sasa kwa tuhuma za kuendesha shughuli hizo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla akiwa ameshika vifuniko vya bidhaa za pombe feki katika moja ya kiwanda bubu cha kutengeneza pombe hizo aina ya Konyagi. katika zoezi hilo eneo la Sinza

LOWASSA ATOA SABABU YA KUTOKUWEPO KWENYE MSIBA WA SITTA NA MUNGAI



Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ametoa ufafanuzi kuhusu mjadala ulioibuka kwenye mitandao ya kijamii baada ya kutoonekana kwenye misiba ya aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta na waziri wa Elimu wa zamani, Joseph Mungai.

Sitta alifariki Novemba 7 mwaka huu nchini Ujerumani alipokuwa ameenda kutibiwa maradhi ya tezi dume ambapo siku iliyofuata alifariki Mungai.

Lowassa amesema kuwa hakuweza kuhudhuria kwakuwa alikuwa nchini Afrika Kusini akimuuguza mdogo wake, Bahati Lowassa.

“Mdogo wangu Bahati Lowassa ni ofisa ubalozi nchini Afrika Kusini, alikuwa anaumwa na alikuwa amelazwa. Kwa siku zote nilikuwa huko kumuangalia. Nisingeacha kuhudhuria misiba hiyo,”Lowassa 

Mwanasiasa huyo ameongeza kuwa alikuwa pamoja na waombolezaji kwa kutuma salamu zake za rambirambi kwa familia ya Sitta kupitia vyombo vya habari pamoja na kumtumia mwanasheria wake kuwasilisha salamu zake za rambirambi kwa familia ya Mungai.

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...