Sunday, 20 December 2015

HOSPITALI ZAAGIZWA KUTENGENEZA MFUMO WA MALIPO WA KIELEKTRONIKI



Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dkt. Hamisi Kigwangalla akifurahi jambo na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sokoine ya Mkoa wa Lindi, Dkt. Evaristo Kasanga (kulia) wakati wa ziara ya kushtukiza aliyofanya mwishoni mwa juma mkoa wa Lindi.(Picha zote na Zainul Mzige wa Modewjiblog)

Na Mwandishi wetu, Mtwara

NAIBU Waziri katika Wizari wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla ameagiza kubadilishwa kwa mifumo ya utawala, malipo na uendeshaji katika katika hospitali nchini ili kuleta ufanisi na tija.

Akizungumza katika ziara yake ya kujifunza kuona katika hali ya kawaida huwa zinatolewaje katika hospitali za wilaya na mikoa alisema kukosekana kwa mifumo bora ya malipo na motisha kumedumaza utumishi.

Ziara yake hiyo ambayo aliifanya katika hospitali ya mkoa wa Lindi ya Sokoine na Ile ya Mtwara ya Ligula ililenga kuona masuala mbalimbali yanayohusiana na utoaji huduma ili kuwa na nafasi ya kutengeneza hali bora zaidi kimkakati.

Alisema tatizo la upungufu wa dawa na hata raslimali watu linasababishwa na kukosekana kwa mfumo waukusanyaji mapato ulio sahihi na wenye salama ambao utawezesha pia kutoa motisha mbalimbali kwa watumishi ili kuwavutia kufanyakazi katika mikoa ya pembezoni.

Aidha alisema malipo yanayofanyika katika hospitali hizo yanatakiwa kuwa ya kielektroniki kwa kuwa imethibitishwa kila kunapokuwapo na mfumo wa malipo kielektroniki unaboresha mapato na hatimaye kuboresha ufanisi katika uendeshaji wa hospitali pamoja na kuwapo kwa huduma bora za dawa.

Pia ameagiza kuharakishwa kwa mfumo wa malipo kielektroniki kwa wateja wa Bima ili mchango wao usaidie kwa haraka utoaji wa huduma ndani ya hospitali.

Hata hivyo Naibu Waziri huyo alisema aliridhishwa na utendaji katika hospitali ya Sokoine na Ligula na kusema ufanisi wao unatokana na kuwapo kwa mipango inayowezesha kazi kufanywa.

Alisema hospitali ya Sokoine imeanzisha utaratibu wa mawasiliano ambao unawezesha daktari mahali popote pale kuitwa huku kila mmoja akijua kwamba daktari ameitwa eneo Fulani.

Alitaka hospitali nyingine nchini hasa za rufaa kuangalia mfumo wa mawasiliano ya ndani wa Hospitali ya Sokoine ili kuleta ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Pia alipongeza utendaji wa hospitali ya Ligula na kusema kwamba kutokana na ufanisi wao na huduma nzuri ndio maana hata wananchi wa nchi jirani wanafika katika hospitali hiyo kupata huduma.

Alisema kama kusingelikuwa na huduma bora wananchi hao wasingelivuka kuja kutafuta huduma Ligula.

Hata hivyo Naibu Waziri huyo alitaka kuwapo na utaratibu wa kudhibiti hali hiyo na kusema kwamba ni matumaini yake kuwa wataalamu wataketi pamoja na kutafuta namna ya kufanya katika mazingira hayo ya pia kuhudumia raia wa nchi jirani.

Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Ligula ya mkoa wa Mtwara, Dkt. Shaibu Maarifa, alisema kwamba pamoja na huduma wanazotoa wanakabiliwa na changamoto kadha hasa wodi ya wanawake na wajawazito.

Alisema kutokana na ongezeko la watu katika mji wa Mtwara kutokana na kuwapo kwa fursa kubwa za uchumi wa gesi na kiwanda cha saruji cha Dangote, wafanyakazi wamekuwa wakifika na familia zao na hivyo kwa sasa wodi hiyo haitoshi.

Hata hivyo alisema hali ingekuwa mbaya zaidi kama kituo cha afya cha Lipombe kisingesaidiana na hospitali hiyo.

Alisema wodi ya watoto kwa sasa inafanyiwa ukarabati na benki ya Eco na wana mkakati mwingine wa kuomba msaada wa kuondoa ufinyu wa wodi ya wanawake.

Alisema anashukuru Katibu Tawala wa mkoa wa Mtwara, Alfred Luwanda na Mkuu wa mkoa wameshafika katika hospitali hiyo na wameahidi kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba matatizo yake yanatatuliwa na kukidhi hospitali ya rufaa.

Kuhusu upatikanaji wa dawa alisema kwamba hospitali hiyo wa sasa ina akiba ya kutosha baada ya serikali kuipelekea sh milioni 80 na tayari wameshazilipa kwa Bohari ya Dawa (MSD).

Aidha alisema dawa za bima afya zipo na kwamba hawatarajii tatizo kwa kuwa wamekubaliana na mamlaka husika kukitokea upungufu watatumia hata fedha za bima kwa ajili ya kupunguza upungufu wa dawa.

Hata hivyo alisema kwamba wanakabiliwa na uhaba wa madaktari bingwa kwani kwa sasa wana dakatri bingwa wa mifupa na wanawake.


Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dkt. Hamisi Kigwangalla akipewa maelezo na Kaimu Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Sokoine ya Mkoa wa Lindi, Damasiana Msalla alipotembelea wodi ya wazazi na kuridhishwa na huduma za hospitalini hiyo wakati wa ziara ya kushtukiza aliyoifanya mwishoni mwa juma mkoani Lindi.


Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sokoine ya Mkoa wa Lindi, Dkt. Evaristo Kasanga akizungumza jambo na Eleuteri Mangi, Afisa kutoka Idara ya Habari -MAELEZO jijini Dar es Salaam.


Hospitali ya Sokoine ya Mkoa wa Lindi imetwaa kombe la mshindi wa pili kwa utoaji wa huduma bora Tanzania kwa mwaka 2015.


Jedwali linaloonesha baadhi ya gharama za matibabu katika huduma zinazotolewa hospitali ya Sokoine ya Mkoa wa Lindi.


Ujumbe wa watoa huduma kwa wateja wanaofika kupata huduma hospitali ya Sokoine ya Mkoa wa Lindi.


Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dkt. Hamisi Kigwangalla (katikati) akiongozana na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Ligula ya mkoa wa Mtwara, Dkt. Shaibu Maarifa (kushoto) pamoja na Daktari wa zamu kitengo cha dharura hospitalini hapo, Dkt. Ester Tumwanga kuelekea wodi za wagonjwa wakati wa ziara ya kushtukiza aliyofanya mwishoni mwa juma mkoani humo.


Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dkt. Hamisi Kigwangalla akiwa kwenye chumba cha dharura katika Hospitali ya Ligula ya mkoa wa Mtwara. Kushoto ni Daktari wa zamu kitengo cha dharura hospitalini hapo, Dkt. Ester Tumwanga.


Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dkt. Hamisi Kigwangalla akitoka kwenye wodi ya wazazi Hospitali ya Ligula ya mkoa wa Mtwara wakati wa ziara ya kushtukiza aliyofanya mwishoni mwa juma mkoani humo. Aliefuatana nae ni Mganga Mkuu wa Hospitali ya Ligula ya mkoa wa Mtwara, Dkt. Shaibu Maarifa.


MAHAKAMA YAFUTA KESI YA KUPINGA UBUNGE WA KUBENEA



MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imefuta kesi ya madai ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Ubungo.

Kesi hiyo ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea wa jimbo hilo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Didas Masaburi dhidi ya mbunge wa jimbo hilo, Saed Kubenea (CHADEMA).

Uamuzi wa maombi ya kufuta kesi hiyo uliwasilishwa mahakamani hapo juzi na wakili wa Dk. Masaburi, Clement Kihoko mbele ya Jaji Lugano Mwandambo.
Wakili Kihoko alisema kuwa mteja wake hana nia ya kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo ya kupinga matokeo.
Baada ya kuwasilisha maombi hayo, Jaji Mwandambo alisema mahakama imepokea maombi hayo ya kuifuta kesi hiyo.

GHARAMA

Baada ya jaji kukubali ombi hilo, Wakili Kihoko aliiomba mahakama kuwapunguzia gharama za uendeshwaji wa kesi ya msingi pamoja na fidia ya usumbufu.
Hata hivyo, Wakili wa Kubenea, Nyaronyo Kicheere, alisema licha ya upande wa utetezi kuomba punguzo hilo, lakini wanapaswa kulipa gharama hizo.

Kutokana na hali hiyo, kuliibuka mvutano wa sheria, jambo lililomlazimu Jaji Mwandambo kuahirisha kesi hiyo kwa muda mfupi, aweze kupitia hoja hizo kabla ya kurudi mahakamani.
Baada ya kurudi, Jaji Mwandambo alisema katika kesi ya msingi mdai anatakiwa kulipa asilimia 50 ya gharama zote za uendeshaji wa kesi hiyo.
Alisema katika maombi ya punguzo la uendeshaji wa kesi hiyo, kila upande utalipia gharama zake.

KUBENEA ANENA
Akizungumza baada ya kutoka mahakamani, Kubenea aliwashukuru wanachama wa Chadema kumsindikiza mahakamani wakati kesi hiyo ikiendelea.
Hata hivyo, alisema kitendo cha Dk. Masaburi kufuta kesi hiyo kinaonyesha wazi kuwa yeye ni mshindi na ataliongoza jimbo hilo katika miaka mitano.
“Wagombea wengine waliofungua kesi kama ya Dk. Masaburi wakati hawana uhakika wa kushinda wanapaswa kuzifuta ili waendelee na kazi nyingine,” alisema Kubenea.

Dk. Masaburi alifungua kesi hiyo namba 8 /2015 kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu kwa mbunge wa Ubungo, Kubenea akidai kuwa yeye na mawakala wake hawakuruhusiwa kuona vifaa vya kupigia kura kama ilivyofanyika kwa Kubenea na mawakala wake.
Vilevile alidai Kubenea alitoa rushwa ya jenereta katika Hospitali ya Mavurunza iliyopo Kimara, zawadi ya meza ya mchezo wa pool kwa vijana wa Makuburi na kujenga barabara ya Matete huko Kimara akiwashawishi kumchagua.

Dk. Masaburi pia alimlalamikia msimamizi kukataa kuhakiki kwa mara ya pili matokeo yake ikiwamo na watu kadhaa wa maeneo ya Mizizini, Mianzini, Kilimahewa, Mizambarauni, Shule ya Mugabe na Kanuni, kutokupiga kura.
Pamoja na Kubenea, washtakiwa wengine katika kesi hiyo walikuwa ni Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Ubungo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mawakili wengine kwa upande wa Kubenea walikuwa Tundu Lissu, Mabere Marando, Peter Kibatala, Method Kimomogolo na Frederick Kihwelo. Chanzo: MTANZANIA

MAGAZETINI LEO JUMATATU

WAZIRI UMMY MWALIMU AVAMIA HOSPITALI YA RUFAA YA BOMBO MKOANI TANGA, KUKAGUA UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA



Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu akizungumza na mmoja wa wahudumu wa afya (jina lake halikuweza kupatikana kiurahisi) wa dirisha la dawa katika Hospitali ya rufaa ya Bombo mkoani Tanga alipofanya ziara ya kushtukiza mchana wa leo Disemba 20, 2015.

-Atoa wiki mbili wawe wamefunga mashine ya kukusanya mapato kwa njia ya Kielektroniki ili kudhitibiti upotevu wa mapato yanayotokana na wananchi kuchangia huduma za afya.


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu akizungumza na mmoja wa wakina mama anayemhudumia mwanae katika wodi ya watoto Hospitali ya rufaa ya Bombo mkoani Tanga alipofanya ziara ya kushtukiza leo mchana Disemba 20, 2015.


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu akimsikiliza mmoja wa akina mama aliyelazwa kwenye wodi ya wazazi wakati wa ziara ya kushtikiza aliyoifanya mchana wa leo Desemba 20, 2015 katika Hospitali ya rufaa ya Bombo mkoani Tanga.


Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga (RMO), Dkt. Clement Marceli akimwelezea changamoto wanazokabiliana nazo katika Hospitali ya rufaa ya Bombo mkoani Tanga Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu (hayupo pichani).


Daktari aliyekuwa kwenye mafunzo, Dkt. Zuberi (Medical Intern) akitoa maelezo ya namna wanavyohudumia wananchi wanaofika hospitalini hapo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu (kulia) aliyefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya rufaa ya Bombo, mkoani Tanga mchana wa leo Desemba 20, 2015 ambapo Waziri huyo alikutana na changamoto utoro wa madktari wa zamu kutokuwepo kwenye kituo chao cha kazi katika Hospitali ya rufaa ya Bombo, mkoani Tanga.



Mratibu wa Hospitali ya Rufaa ya Bombo, mkoani Tanga kutoka Idara ya Tiba, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Ibrahimu Maduhu (mwenye tai) akitoa maelezo kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu namna wanavyokabiliana na changamoto ya kuzuia vifo vya mama na mtoto katika hospitali hiyo wakati wa ziara ya kushtukiza iliyofanywa na Mh. Ummy Mwalimu katika wodi ya wazazi leo mchana Disemba 20, 2015.


Baadhi ya madaktari waliokuwa mafunzoni wakizungumza na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu aliyefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo, mkoani Tanga mchana wa leo Disemba 20, 2015.


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu akipitia orodha ya mahudhurio ya zamu za Madaktari na Wauguzi ambao wengi hawakuwepo kazini wakati wa ziara yake ya kushtukiza katika Hospitali ya rufaa ya Bombo, mkoani Tanga aliyoifanya leo mchana Disemba 20, 2015.







WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...