Rais Jakaya Kikwete akihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo jioni huku Spika wa Bunge hilo Anna Makinda (kulia) akifuatilia kwa umakini mkubwa. (Picha kwa Hisani ya Ikulu)
HOTUBA YA MHESHIMIWA DR. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUAGANA NA BUNGE NA KULIVUNJA BUNGE LA KUMI LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, UKUMBI WA BUNGE, DODOMA TAREHE 9 JULAI, 2015.
Mheshimiwa Spika;
Tunayo kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kutujalia uzima na kutuwezesha kuishuhudia siku hii adhimu katika historia ya Bunge letu na nchi yetu. Hatimaye siku ya kuvunja Bunge la Kumi imewadia ili kuwezesha hatua husika za mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ziweze kutekelezwa.
Nakushukuru sana Mheshimiwa Spika kwa kunipatia nafasi hii ya kulihutubia Bunge lako tukufu ili niweze kutimiza wajibu wangu huo wa msingi Kikatiba. Lakini, shukrani zangu kubwa ni kwa uongozi wako mahiri na shupavu. Umeliongoza Bunge vizuri. Najua haikuwa kazi rahisi. Penye wengi pana mengi. Lakini kwa uhodari mkubwa umeweza kulifikisha jahazi bandarini salama salmini. Hakika wewe ni nahodha makini na jemedari hodari, uliyethibitisha uhodari na umakini wako katika uwanja wa medani. Wewe ndiwe mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huu wa juu kabisa katika mhimili huu wa kutunga sheria na umeidhihirishia dunia kuwa wanawake wakipewa nafasi wanaweza.
Mheshimiwa Spika;
Niruhusu pia nitoe shukrani na pongezi zangu za dhati kwa Waheshimiwa Wabunge kwa kazi kubwa na nzuri mliyoifanya. Mmetimiza ipasavyo wajibu wao wa Kikatiba wa Kutunga Sheria na kusimamia Serikali. Nawashukuru kwa ushirikiano wenu na msaada wenu. Ni ukweli ulio wazi kuwa bila ya ninyi Wabunge wetu na Bunge hili, tusingeweza kupata mafaniko na maendeleo tuliyoyapata. Mmejijengea, nyinyi wenyewe na Bunge letu heshima kubwa mbele ya wananchi. Mmeitendea haki demokrasia ya Tanzania na kuliletea heshima kubwa Bunge letu nchini, kikanda na kimataifa.
Mheshimiwa Spika;
Tarehe 30 Desemba 2005 nilipozindua Bunge la Tisa nilielezea mtazamo wangu kuhusu nchi yetu na kutaja majukumu ya msingi na vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Nne. Nilisema tutatekeleza wajibu wetu na vipaumbele hivyo kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya. Tarehe 16 Julai, 2010 wakati wa kuvunja Bunge hilo nilielezea mafanikio tuliyopata na changamoto zilizotukabili katika kipindi hicho. Tarehe 28 Novemba, 2010 wakati wa kuzindua Bunge hili la Kumi niliainisha vipaumbele vya Serikali ya Chama cha Mapinduzi katika kipindi changu cha pili cha uongozi wa nchi yetu na kuahidi kuvitekeleza kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi. Kama ilivyo ada, leo tunafikia mwisho wa uhai wa Bunge la Kumi, naomba kutumia fursa hii kutoa mrejesho wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali na yale mambo ambayo tuliahidi na kupanga kufanya.