Na Gustav Chahe, Iringa
Jumla ya watuhumiwa wanane (8) ambao walitakiwa kupelekwa mahakamani kwa sababu za ubadhilifu wa pesa za mradi wa kijiji cha Madege umeingia dosari na wanakijiji kuutupia uongozi lawama za kushindwa kufanya hivyo. Zaidi ya shilingi milioni ishirini na moja (21m/-) za mradi huo ambao unaendeshwa kwa ufadhili wa Districts Agricultural Development Programme Support (DADS), yaani mpango wa kilimo wilayani, kutoka Denmark ulitiwa dosari na baadhi ya wanakijiji walioamua kujinyakulia fedha kinyemela na kuzitia mifukoni mwao.
Kijiji hicho kilipata bahati ya ufadhili wa mashine mbili zenye vinu vya kukoboa na kusaga kwa ajili ya maendeleo ya kijiji hicho licha ya kuwa kinakabiliwa na changamoto mbalimbali za kila aina ambazo zinahitaji nguvu kubwa itumike ili kujikwamua nazo.
Hasara hiyo inatokana na usimamizi mbovu wa wale waliopewa dhamana na kijiji kusimamia ikiwa ni pamoja na kutokuwa na na mwongozo wa uendeshaji na kuzitumia mashine hizo kama mali zao binafsi kwa ajili ya maslahi yao. Kwa kutochukuliwa hatua yoyote watuhumiwa hao kunatokana na ama kula njama moja na viongozi hao au kwa kile kinachosadikiwa na wengi kuwa ni hali ya kulindana ili kuepusha kuumbuana pindi watakapo kuwa kizimbani kwa ajili ya kutolea maelezo juu ya ubadhilifu huo. Itakumbukwa kuwa mmoja wa watuhumiwa alipohojiwa na mwandishi hapo katika makala ya awali alieleza kuwa haogopi kwenda mahakamani kwa kuwa kule ndiko atakakotolea maelezo ya ukweli na uhakika.
Bw. Elenasi Kikoti ambaye ni miongoni mwa watuhumiwa alidiriki kusema hivyo kwa mwandishi kwa kile alichosema hawezi kumwambia mtu yeyote siri aliyo nayo hadi kitakapoeleweka mahakamani hiko kwani akiongea mapema anaweza akageuziwa ubaya. “Ukweli mwandishi mimi siwezi ni katoa siri niliyonayo sasa hivi ili tutakapofika mahakamani ndiko nitakako toa siri yangu na kuzungumza ukweli kutokana na mambo ninayoyajua kuhusiana na mradi huu na mengine ambayo si ya mradi huu, lakini yanahusiana na maendeleo ya kijiji” alisema Bw. Kikoti.
Kwa mujibu wa ripoti ya tume iliyoundwa kwa ajili ya uchunguzi wa mradi huo, lilikuwa na orodha ya watuhumiwa ambao wanahusika moja kwa moja kujibu tuhuma na kustahili uadabishwa juu ya ubadhilifu wa pesa hizo. Ripoti hiyo imeorodheshwa majina ya Santina Msuva, Zamda Mtenga, Waride Sechambo, Elenasi Kikoti, Jasimini Kikoti pamoja na Boazi Kadinda, Athumani Kisima na Elisha Mhile. Mradi huo ulianza tangu mwaka 2006 ambao ulilenga kukinufaisha kijiji hicho chenye wakazi 2,225 pamoja na maeneo jirani ambao hutegemea kilimo katika kujipatia mahitaji yao ya kila siku na kuwajibika katika shughuli mbalimbali za maendeleo yao binafsi, kijiji hata kwa ajili ya maendeleo ya kitaifa kwa ujumla.
Aidha, Lesamu Msuva naye anaingizwa katika tuhuma hizo kwa kushindwa kuwajibika katika tatizo hilo wakati wa uongozi wake alipokuwa Diwani katika Kata hiyo katika kipindi cha awamu ya kwanza ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete. Mheshimiwa huyo anaingizwa katika kundi hilo kwa kile kinachodaiwa ufisadi kwake lilikuwa ni jambo la kawaida kwani aliogopa kuwakoromea wenzake kwa kuwa hata yeye wanakula sahani moja. Kama isemwavyo “mtoto umleavyo, ndivyo akuavyo”, kutokumuadabisha fisadi ni kuna maanisha kuwa hali hii ni ya kawaida kwa kuwa hakuna aliye safi wa kumuondoa mwenzake au wa kumkaripia na kumchukulia hatua. Hii ni kwa sababu ya usemi usemwao “ndege wenye mabawa yanayofanana, huruka pamoja”, ndivyo ilivyo hata kwa watu wa namna hiyo kulindana kwa ili wasiumbuane, lakini pindi inapotokea mmoja ameumbuka huwa inakuwa tafrani kubwa kwa maswahiba hao.
Awali akiongea na mwandishi wa habari hizi, Afisa Mtendaji wa kijiji hicho Bw. Elijus Kikoti alisema kuwa watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote utaratibu utakapokuwa umekamilika. Kadiri siku zinavyozidi kwenda hali ya kijiji inazidi kuwa mbaya kutokana na watu kutojitokeza kwa uwingi katika kutumia nguvu zao katika maendeleo ya kijiji hususani katika michango, na kujitoa pale wanapotakiwa kutumia nguvu zao.
Ikiwa viongozi wa kijiji hicho walikanusha madai ya wanakijiji kuwepo na hali ya kuogopana na viongozi kula sambamba na watu wanaotia hasara maendeleo ya kijiji hicho, hali inazidi kuonekana wazi kwa tuhuma hizo. Kiongozi mmoja ambaye jina tunalo, alipohojiwa na mwandishi wa makala haya juu ya kujihusisha na wanaosadikiwa kuwa ni wabadhilifu wa miradi ya maendeleo ya kijiji, alieleza kuwa wao hawatakuwa wa kwanza kujihusisha na watu kama hao wakati wapo wengi wanaofanya hivyo. “Siwezi kukubali au kukata, watanzania wa leo siyo wajinga kiasi kwamba wanaweza kudanganywa kirahisi. Najua watakuwa wanaongea wanachokijua. Kama ni hivyo, hatutakuwa wa kwanza sisi kufanya hivyo kwa sababu hata ukiangalia jinsi nchi inavyokwenda tunasikia kabisa hata ngazi za juu wanafanya hivyo sembuse na sisi ambaye ni wadogo kabisa. Kumbuka mwandishi kuna usemi ambao husemwa “mtoto wa nyoka ni nyoka tu” alieleza kiongozi huyo.
Kiongozi huyo ambaye aliomba jina lake lisiandikwe alieleza waziwazi kuwa mpango huo kautatimia endapo safu ya uongozi uliopo haitafanyiwa marekebisho kwani haiwezekani watu wanaokula pamoja wakatafutana ubaya. “Ninaomba unilinde jina langu ili nikwambie ukweli. Ninakwambia, kama watuhumiwa hawa watapelekwa mahakamani tutaona. Ninasema hivi kwa sababu ninajua; miongoni mwetu tunakula sahani moja na watuhumiwa kwa hiyo mpango wa kuwapeleka watuhumiwa mahakamani utabaki maneno tu hadi utakapopotea tu hewani kwa sababu si rahisi wakafanya usaliti wanaoijua siri yote” alisema.
Mpango wa kuwapeleka watuhumiwa wa ubadhilifu wa fedha za mradi wa DADS wa kijiji cha Madege mahakamani umeota mabawa na kuwaacha watuhumiwa wakitesa kwa zamu kijijini hapo kwa raha zao. Watuhumiwa hao imeshindikana kupelekwa mahakamani kutokana na udhaifu wa uongozi wa kijiji hicho kuingiza udugu na urafiki badala ya kuwajibika katika nafasi zao za kiutendaji katika kuwahudumia wananchi.
Awali wananchi waliilalamikia serikali ya kijiji hicho kuwachukulia watuhumiwa kama ndugu zao na kuwakingia kifua ili suala liweze kupotea bila maelezo na kuwaacha wananchi gizani bila kujua kinachoendelea. Mradi huo ulitiwa dosari na baadhi ya wanakijiji hicho walioamua kujinyakulia fedha kinyemela na kuzisweka wanakokujua wao na kuwaacha wanakijiji wakihaha bila kupata majibu huku wakipoteza nguvu zao kwa ajili ya maendeleo ya kijiji.
Itakumbukwa awali wananchi walidai kuwepo na hali ya kubebana ambako ni sababu kubwa inayosababisha kutowafikisha watuhumiwa hao mahakamani. Maelezo ya viongozi wa kijiji yalionekana kwenda tofauti na kauli za wananchi kwa kile walichokieleza kuwa hawezi kumuogopa mtu yeyote kwa namna yoyote ile. Hali inazidi kuwa mbaya kutokana na mashine hizo kusimama badala ya kuhudumia wanakijiji huku wanakijiji wakibaki na mahangaiko yasiyokuwa na majibu na viongozi wao wakiendelea kubaki kimya. Bado wanakijiji wanaendelea kulalamika ili haki iweze kutendeka na sheria iweze kuchukua mkondo wake dhidi ya watuhumiwa hao vinginevyo hali si shwari. Wakizungumza na mwandishi wa makala haya kwa nyakati tofauti, wanakijiji wanaulalamikia uongozi wa kijiji hicho kuwa wanafanya kazi kwa upendeleo huku wengine wakiumia kwa ajili ya maendekeo ya kijiji. “Ndugu mwandishi, sisi wanakijiji tupo gizani hadi sasa kuona viongozi wetu wanakaa kimya bila kutuelekeza ni nini kinaendelea kwa watuhumiwa hao wanaotutesa sisi wengine” anasema mwanakijiji mmoja.
Pia anasema ni bora kutolea maelezo kama wanashindwa badala ya kukaa kimya kwani wapo wanakijiji ambao wanaweza wakalifanya hilo kwa ufanisi kulingana na uchungu wao kwa kijiji na nguvu zao wanazozipoteza kwa ajili ya maendeleo ya kijiji hicho. “Kama wanashindwa kufanya kazi na kuwapeleka watuhumiwa hao mahakamani watueleze ili sisi wanakijiji tujue la kufanya; tunaweza tukawateua watu ambao tunawaamini walisimamie suala hilo kuwapeleka mahakamani” anasema mwanakijiji huyo.
Naye katibu wa kamati ya uchunguzi wa mradi huo Bw. Felix Kayage anaeleza kuwa, tatizo ni porojo nyingi kuliko uwajibikaji na ndiyo maana maendeleo ya kijiji yanazidi kudumaa. “Ukweli ni kwamba porojo ni nyinyi kuliko uwajibikaji na ndiyo maana tunashindwa kufanya kazi za msingi; kama uwajibikaji ungekuwa wa kifanisi, watu kama hao wasingekuwa wanafumbiwa macho kwa muda wote huo na kusabasha hasara kuendelea kujitokeza zaidi” anasema Bw. Kayage. Taarifa za kuaminika zilizolifika gazeti hili zinasema, moja ya mambo ambayo yanakwamisha maendeleo katika kijiji hicho ni kuwepo kwa undugu zaidi kuliko uwajibikaji wa viongozi katika nafasi zao kwa kutenda haki. “Ndugu mwandishi, hiki kijiji hakiwezi kuendelea kamwe kutokana na viongozi kuendekeza undugu na urafiki badala ya kuwajibika katika nafasi zao. Tabia hii ndiyo inayotumaliza sisi wananchi kila kunapokucha kwa kuwa hata anayeonekana kwenda kinyume na utaratibu wetu akiowa ni rafiki wa kiongozi au ndugu wa kiongozi, hawezi kuadabishwa” kinasema chanzo hicho. Katika maelezo ya wanakijiji waliowengi, wanakijiji wanazidi kukata tamaa siku hadi siku kutokana udhaifu walionao viongozi wao kiutendaji na kuwajibika katika malalamiko na ushauri wao kwa ajili ya ufanisi bora.
Wednesday, 4 May 2011
Subscribe to:
Posts (Atom)
WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...
Na Friday Simbaya, Mufindi Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...
-
KIKUNDI cha Upendo ni kikundi cha kina mama 20 walioamua kujiunga kwa pamoja na kuanz...
-
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini MIEMBE hulimwa karibu katika nchi zote zilizoko kwenye ukanda wa joto, na hasa tropiki. Nchini ...
-
Habari ndugu msomaji wetu wa blog, Natumaini unaendelea vyema. Leo tutaanza kujifunza kilimo cha bora cha nyanya, na tutaanza kufahamu vit...