Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Lupefu, Lugarawa wakiwa darasani na Mwalimu Mary Mhagama huku wakiwa wamebanana saba kwenye dawati moja lenye uwezo wa watoto watatu. |
WANAFUNZI katika Shule ya Msingi ya Lupefu iliyoko Kata ya Lugarawa wilayani Ludewa, mkoani Iringa wako hatarini kukatika miguu na viungo vingine vya mwili kutokana na kuliwa na funza mikono na miguu yao kunakosabishwa na uhaba wa madawati ambapo sasa wanafunzi saba wanalazimika kukalia dawati moja.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bi. Aprudensia Lugome amekiri kuwepo kwa matatizo hayo na kuongeza kuwa hali hiyo inatokana na ukata wa fedha unaoikabili shule yake pamoja na uelewa na mwamko mdogo wa wananchi juu ya elimu.
Lugome alisema hulazimika kila wakati kununua pini madukani kwa fedha zake na kuwaita wazazi wa wanafunzi wenye mafunza kufika shuleni kushiriki kuwatoa funza watoto wao hata hivyo hufika wachache.
Aidha aliongeza kuwa uchakavu wa majengo na ukosefu wa vitabu vya kujifunzia kunatokana nakusahaulika kwa shule ya Lupefu iliyoko upande wa kusini magharibi katika ya kata ya Lugarawa Ludewa.
Alisema kuwa shule hiyo ilianzishwa mwaka 1978 na kwamba hadi sasa ina jumla ya wanafunzi 545, madawati 149, vyumba 10 vya madarasa kati ya hivyo vyenye ubora vikiwa vitatu, walimu 15 lakini walio wengi wakiwa na matatizo ya kiafya.
Kuhusu utoro kwa wanafunzi mwalimu Lugome alimwambia mwandishi wetu kuwa watoto wengi wanatoka umbali mrefu wengine kilomita 6 hasa katika milima ya Luholomela na Msango na kwamba umbali huo husababisha wachoke na kuishia vichakani inakuwa vigumu kwa walimu na wazazi kugundua hali hiyo.
Kwa upande wa vyoo mkuu huyo alisema kuwa vyoo vyote vilivyopo ni vya muda tu na kwamba kwa sasa anajenga matundu 12 ya choo cha wanawake kutokana na fedha za faini kwa wazazi wa watoto wenye funza.
Alisema pamoja na hali hiyo watoto wamekuwa wakianguka hovyo na kupoteza fahamu shuleni hapo lakini cha kushangaza wakati mwingine huzinduka baada ya muda mfupi wakipelekwa hospitalini, hatimaye huendelea na shughuli kama kawaida.
Alizitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili shule yake kuwa ni pamoja na ukosefu wa fedha za kuendeshea shule ambapo hulazimika kufanya vibarua kwa walimu na watu wengine sanjari na kuuza kuni na matete tunapohitaji kununua mahitaji ya shule.
Amewataka wazazi kuwekeza katika elimu na kufuatilia kwa karibu maendeleo ya watoto wao. Lakini akaishauri serikali kwenda na wakati kwa kutoa mafunzo kwa walimu hasa wanapobadili sera mpya ya elimu.
Serikali haijatoa mwongozo mpya namna ya kuendesha shule hasa baada ya MEM kuonekana inalegalega kwa kutopatikana kwa fedha mashuleni na sasa shule nyingi zinaendeshwa kwa kusuasua.