KANISA LA BAPTIST SINDE
Na Friday Simbaya, Mbeya
“Nilizaliwa katika familia ya kipagani ambapo baba yangu mzazi alikuwa ni msaidizi wa chifu ambao waliitwa ‘Ifumu’, habari za dini na elimu kwake zilikuwa ni mwiko…”
Hayo yalikuwa ni maneno ya Mchungaji Raphael Mwasifiga wa Kanisa la Baptist la Kanani, Makunguru Sinde, Mwanjelwa mkoani Mbeya.
Mchungaji Mwasifiga alizaliwa mwaka 1953 katika kijiji cha Lukule Kiwira akiwa ni mtoto wa saba na wa mwisho katika familia ya Mzee Mwasifiga.
Alisema kuwa alipenda sana kusoma shule na kujifunza dini lakini haikuwa kazi rahisi kutokana na baba yake kuona vitu kama hivyo ni vya kihuni.
“Wakati ni kiwa mtoto nimechunga sana ng’ombe kijijini kwetu na baadaye niliamua kwenda shule na nilisoma mpaka darasa la saba mwaka 1968,” alisema Mch. Mwasifiga.
Alisema kuwa baada ya kumaliza elimu ya msingi alikwenda kuishi na dada yake mjini Mbeya ndipo alipoanza kujishughulisha na masuala ya dini na baadaye kumpokea Bwana Yesu.
Alisema kuwa kabla hajaja mjini Mbeya kuishi na dada yake, aliwahi kushiriki mkutano mkubwa wa injili uliondaliwa na kanisa la KKKT huko Masebe Tukuyu, Mwakaleli ambao ulifanyika kwa siku nne na ndipo aliposhukiwa na roho mtakatifu na kujikuta akiwa muinjilisti.
Alisema kuwa wazazi wake waliposikia ameokoka kitendo kicho kuliwachukiza sana.
Baba yake alikuwa anaona masuala ya dini na elimu kwake kama ni usanii ndio maana hakuona haja ya kuwapeleka watoto shuleni, alisema.
Baada ya kuona kuwa baba yake hakuwa na mpango wakuwapeleka shule ndipo alipoamua kwenda shule mwenyewe.
Mchungaji Mwasifiga alisoma katika Shule ya misheni ya Igogwe katika ‘Bush school’ hadi darasa la saba huko wilayani Rungwe Tukuyu, mkoani Mbeya.
Alisema kuwa baada ya baba yake kufariki mnamo mwaka 1964 alikuja kuishi mjini Mbeya kwa dada yake Mbeya maeneo ya Majengo.
Alisema kuwa katika watoto saba yeye pekee ndiye aliyesoma lakini dada zake wote hawakuwahi kuhudhuria hata darasa moja.
Alisema alipofika mjini Mbeya alipenda sana kwenda kanisani ndipo alipogundua kipaji chake cha uchungaji kupitia kwa Mchungaji mmoja Mwansodobe wa Kanisa la Baptist Majengo, ambapo akampokea Bwana Yesu na hatimaye kubatizwa kwa maji mengi.
Alisema alienda kusoma katika Chuo cha biblia tukuyu ambalo ni tawi la Arusha Bible College kwa miaka minne na nusu.
Alisema kuwa baada ya kumpokea Yesu aliamua kuwa muinjilisiti wa kujitolea kwa kuhubiri neno la Mungu nyumba kwa nyumba.
Alisema alikuwa anatembea kwa miguu kutangaza injili ya Yesu katika maeneo mbalimbali kutoka Uyole mpaka Mwakaleli katika miaka 1970 na 1972.
Alisema alifanyakazi ya kuhubiri na baadaye akaanza kutafutakazi kwa ajili ya kuoa.
Mnamo mwaka 1970 aliacha kazi pale Chuo cha Kilimo Uyole mjini Mbeya ambapo ni kuwa kama mtunza stoo (storekeeper) wakati huo chuo hicho kilikuwa na wazungu wawili na jengo moja tu, na kazi yake ilikuwa ya kutunza maziwa, mayai na kuuza kabeji.
“Nilikuwa nimeajiliwa sehemu mbalimbali kama vile kampuni ya Simu na kampuni mmoja ya kichina iliokuwa inajenga reli ya TAZARA na shirika la umeme la TANESCO,” aliongeza.
Alisema kuwa baada ya kufanyakazi kwa muda mrefu aliamua kuoa mke anaitwaye Kisa Mwasifiga.
Mwaka 1979 nilienda Chuo cha Biblia cha Tukuyu kwa miaka minne baada ya kumaliza chuo aliendelea na uinjilishaji kuwa kuhubiri mitaani, alisema.
Alisema kuwa baada ya kufanya kazi ya Mungu mitaani aliamua kwenda kuomba darasa katika Shule ya Msingi Sinde na Rais Mwinyi alipoingia madarani alipiga marufuku watu kutumia majengo ya shule kuhubiria neno la Mungu.
Alisema kuwa baada ya kufukuzwa pale shuleni ndipo alipoamua kuanzisha kanisa lake akiwa na waumini wanane tu lakini leo kanisa linafurika.
Mchungaji Mwasifiga alisema alinunua viploti viwili kwa shilingi elfu 33 wakati huo kutoka kwa wenyeji kwa ajili ya kujenga kanisa mwaka 1992.
Alisema kabla ya kuanzisha kanisa alikodi lipagale moja ambalo walitumia kama kanisa kwa takribani miezi sita huku akiendelea na ujenzi wa kanisa.
Alisema kuwa walianza kujenga kanisa mwaka 1992 na familia yake kwa kushirikiana na waumini wachache waliokuwepo.
“Tulipo eneo la kujenga kanisa tuanaza mara moja kufyatua matofali na kuanza ujenzi mara moja huku nikipiga mikutano ya nguvu katika eneo la kanisa…” aliongeza Mchungaji Mwasifiga.
Alisema kuwa katika waumini wale na walikuwepo mafundi ujenzi wawili ambao walikuwa wanasaidiana nao kujenga ambapo mafunzi wakiinua kuta wao kazi yao ilikuwa kukazia.
Alisema kuwa walipomaliza kujenga kanisa hilo katika maeneo ya Makunguru Sinde, Mwanjelwa alitokea mzungu mmoja aitwaye Rafubo akawasaidia vigae kwa ajili ya kuezeka kanizsa lakini kwa bahati mbaya vigae vile vilikuwa vibovu vilianza kudondoka.
Alisema kuwa baada ya kuona kuwa vigae vile ni vibovu waliamua kuezeka kwa bati na mpaka sasa kanisa hilo linaendelea kupanuliwa na wanampango wa kujenga ghorofa moja ili waumini wasikae nje wakati wa kusali.
Alisema kuwa Kanisa la Kanani limepitia katika hatua mbalimbali za ujenzi na kwa sasa wameanza kulipanua ilikujenga ghorofa moja na wamenunua pia vyombo vya muziki kwa ajili ya kumtukuza Mungu.
Alisema wakati anafanya kazi ya Mungu alitokea Mchungaji Mpeli Mwaisumbe wa Kanisa la Daily Bread life Ministry lililopo mjini Iringa mkoani Iringa.
Alisema kuwa Mchungaji Mpeli alikuwa ametoka kusoma masuala ya kichungaji na kupewa kanisa moja pale Mabatini mjini Mbeya kabla ya kuhamia Iringa ambapo sasa ana kanisa lake la Daily Bread Life Ministry.
“Mchungaji Mpelia lipotoka chuo hakuwa na uzoefu wakuhubiri neno la Mungu kwa hiyo aliamua kuungana na mimi katika Kanisa la Baptist ili kujifunza zaidi…,” alisema Mch. Mwasifiga.
Shirika la Daily Bread Life ambalo linaongozwa na Mchungaji Mpeli Mwasumbe lina kituo cha kulelea watoto yatima cha ‘Daily Bread Life Children's Home’ chenye watoto 40 kilichoanzishwa mwaka 2005 kupitia Daily Bread Life Ministries.
Aidha, Mchungaji Mwasifiga alisema kuwa amefundisha watumishi wengi na wengine wameamua kuanzisha makanisa yao wakitokea mikononi mwake.
Mchungaji Mwasifiga amekua mchungaji katika Jumuiya ya Wabaptist Mbeya nakushika nyazifu mbalimbali za uongozi na kwa sasa ni mdhamini mkuu wa ‘Baptist Convention of Tanzania-BCT.’
Mchungaji Mwasifiga amekuwa mchungaji kwa zaidi ya miaka 34 na kwa sasa ameamua kustaafu kwa hiari na atabakia kuwa mshauriwa wa Kanisa la Baptist la Kanani Mbeya, Makunguru Sinde maeneo ya Mwanjelwa.
Alisema kuwa kanisa lake limefanyikiwa kusomesha wachungaji wanne ambao ni mchungaji Mwapongo ambaye ni mkuu wajimbo la Baptist Mbeya, Mwalusamba, Mwambona na Kawema na wengine ni wasichana walioinuka kuwa wachungaji.
Alisema kuwa kutokana afya yake kutokuwa nzuri ameamua kupumzika ambapo tarehe 28.08.2016 ndio tarehe yake maalum ya kustaafu.
Alisema kuwa haikuwa kazi rahisi kwake hadi kufikia hapo alipo kwani, alipitia katika changamoto nyingi ikiwemo kuugua magonjwa ya ajabu na pengine kulala nje kwa sababu yakukosa mahali pakulala wakati akifanya kazi ya Mungu.