Saturday, 13 August 2011

DKT MFUTAKAMBA: ZAIDI YA BILIONI 6 KUBORESHA USAFIRI WA MELI ZIWA NYASA,V ICTORIA NA TANGANYIKA



LUDEWA             
SERIKALI imetenga zaidi ya shilingi bilion 6 kwa ajili ya kuboresha usafiri wa Meli katika maziwa matatu nchini likiwemo Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa ambalo ni ziwa pekee lenye kero na changamoto kwa wananchi wa Ludewa, Songea na Mbeya.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi Dkt Athumani Mfutakamba alipotembelea Kata ya Masasi na Manda Wilayani Ludewa kujionea mwenyewe eneo kitakapojengwa kiwanja cha ndege katika kijiji cha Sagalu kama njia ya kuvutia wawekezaji kufika na kuwekeza Wilayani humo.
Dkt Mfutakamba alisema kuwa ujenzi wa uwanja wa ndege Sagalu Wilayani Ludewa utasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi na kufungua milango ya kimaendeleo zaidi wilayani humo kutokana na kuwa na utajiri wa madini ya chuma na makaa ya mawe na dhahabu.
Hata hivyo waziri huyo aliahidi kuwa ujenzi wa uwanja huo muhimu utaanza mara baada ya wataalam wa viwanja vya ndege kufika na kulifanyia uchunguzi wa kina eneo hilo.
“Eneo nimeliona linafaa lakini kama serikali sasa tunaiachia jukumu hili Mamlaka ya viwanja vya ndege nchini ili kuangalia uwezekano wa kuufufua uwanja huu na kuuboresha sanjari na uwanja wa ndege Njombe kama njia ya kupanua wigo wa uchumi katika mikoa ya kusini.”” Alisema Mfutakamba.
Mfutakamba aliainisha kuwa fedha hizo kwa upande wa Ziwa Nyasa zitatumika kuboresha usafiri wa meli na kujenga magati na bandari katika mwambao wote wa Ziwa Nyasa ambako hadi sasa hakuna bandari ya uhakika.
Aliongeza kuwa wananchi wilayani Ludewa wanaendelea kuyalinda na kuyatazama madini kwa macho huku wenyewe wakikabiliana na umaskini wa kipato unaosababishwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa miundombinu hafifu, kukosekana kwa viwanja vya ndege ndani ya wilaya hiyo ambapo utajiri ulioko umegeuka mateso kwa wananchi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wilayani humo wamesema miradi ya Mchuchuma na Liganga ni moja kati ya miradi mikubwa nchini lakini wakaishangaa serikali kusuasua kuanza utekelezaji.
Walisema kama miradi ya makaa ya mawe ya ketewaka, mchuchuma na chuma cha magangamatitu na Liganga itaanza vijana wengi watapata ajira pamoja na Taifa kuondokana na mgao wa umeme kwa sababu mradi huo peke yake unaweza kuzalisha megawati 600 hadi 1000.
Pamoja na mradi huo kuwapatia vijana ajira lakini pia utapunguza umaskini uliokithiri miongoni mwa wananchi kwa kutoa fursa mbalimbali kama sekta ya biashara kutokana na ongezeko kubwa la watu wanaotarajia kuja Ludewa kufanyakazi mgodini.
Eneo la Sagalu linalotarajiwa kujengwa uwanja wa ndege wilayani Ludewa awali katika miaka ya sabini liliwahi kutumika na Jeshi la Wananchi wa Tanzania ya Ulinzi na Usalama kipindi cha utawala wa Ngwazi Kamuzu Banda Rais wa kwanza wa Malawi, aliyejiita wa Muyaya alipojaribu kuchukua ardhi ya Tanzania upande wa Ziwa Nyasa na kusema ni eneo lake.
                             MWISHO

DIWANI LUDEWA AMKANA DC MKUTANONI, AGEUKA BUBU KUJIBU MASWALI LIKIWEMO LA KUMFUKUZA MWANDISHI WA HABARI




Na Friday Simbaya,
Ludewa
DIWANI wa Kata ya Ludewa ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludew, Bi Monica Mchiro juzi alimkana hadharani Mkuu wa Wilaya hiyo Bi Georgina Bundala kutokana na mkuu huyo kutokuweka bayana kilichotokea kati ya wananchi na watafiti wa madini walioingia na mitambo na kuanza shughuli katika Kata ya Iwela bila taarifa kwa madiwani na kuzua hofu na mkanganyiko kwa wananchi.
Bi Monica alifikia hatua hiyo ya kuwaambia wananchi ukweli baada ya Naibu Kamishna wa Madini Kanda ya Mbeya Bw. John Shija kuweka wazi Sheria za Madini na jinsi walivyotekeleza baada ya kutoa leseni ya utafiti katika kata ya Iwela na hatimaye wananchi kugundua kuwa tatizo lilikuwa katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi.
Bi. Monica pamoja na wapigakura wake walikuwa wametega masikio na kutegemea kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo Bi Georgina Bundala angetoa ufafanuzi juu ya utata uliokuwepo kati ya wananchi na wachimbaji madini waliokuwa wameingia na mitambo katika kata hiyo na kuzua utata jambo lililopelekea madiwani wote pamoja na wabunge kufanya ziara ya kushtukiza na kuiingizia hasara halmashauri.
“Ndugu wananchi sisi madiwani wenu tulivyosikia mkanganyo kuhusu watafiti na wachimbaji hao walioko katika Kata ya Iwela tuliamua kufanya ziara ya kushtukiza, lakini tulikuta wahusika wana vibali vyote ikiwemo barua ya Mkuu wa Wilaya. Jambo hili lilituudhi sana kwani kama walikuwa wanajua kwanini wasituambie mpaka Halmashauri ikaingia gharama ya kuwasafirisha madiwani wote 35 bila sababu wangetuambia,” aling’aka Monica.
Awali, Bw. Shija aliwaambia wananchi kuwa baada ya watafiti hao kupewa leseni na kamishna wa Madini Kanda. “Tulimwandikia barua Mkuu wa Wilaya kuwatambulisha kwake ili utaratibu ufuatwe wa kuwafikisha hadi kwa walengwa kijijini.”
“Tukishatambulisha mtafiti au mchimbaji kwa Mkuu wa Wilaya husika siyo jukumu letu tena kufuatilia mamlaka nyingine, lakini sheria inasema kamishna akishatambulisha ugeni kwa Mkuu wa Wilaya ni jukumu lake kuwatambulisha kwa Mkurugenzi na yeye kuwapeleka na kuwatambulusha katika ngazi zote hadi ulipo mradi,”alibainisha Bw Shija.
Madiwani katika baraza kuu waliiomba ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri kumwita kamishna wa madini kanda ili akutane na madiwani hao ili na wao waweze kujiridhisha na kuwaondolea utata uliokuwepo, lakini wakashangaa kamishna huyo akitembezwa na Mkuu wa Wilaya katika baadhi ya Kata wakati Ludewa yote imefunikwa na madini.
Baada ya kamishna kufafanua na kueleza kwa uwazi kuhusu utaratibu ulitumika ndipo maswali yakaanza. “Mimi swali langu ni moja tu kwako Mkuu wa Wilaya naomba ujibu tujue wote kama kweli wewe unatenda kazi zako kwa haki utaratibu na sheria kwanini umemkataze mwandishi wa habari kufanyakazi yake katika mkutano huu wa hadhara,” aliuliza kwa jazba Bw Amani Chaula.
Swali ambalo lilimtesa na kumnyima raha Mkuu huyo na kushindwa kujibu jambo lilizua mashaka kwa wananchi.
“Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wao ni wapita njia tu wanafanya haya kwa maslahi yao binafsi ili baadaye tutakapokuwa tumeanza mvutano kati ya mwekezaji na wananchi wao watakuwa wameshahama,”alilalamika mzee Timoth Mtitu.
Monica aliwaambia wananchi kuwa utaratibu alioueleza Kamishna ni mzuri, lakini sijui kwanini haukufuatwa na viongozi wetu wa Wilaya halafu mbaya zaidi wakauchuna bila kutushirikisha madiwani wote na wabunge.
Monica, “madiwani hawakujua kama watafiti na wachimba madini walioko Iwela walipita na kupata baraka zote kutoka katika ofisi za Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi tungejua tusingekwenda ilikuwa ni aibu tupu tulipofika tulioneshwa vibali vyote ikiwemo barua ya Mkuu,” alisikitika Monica.
Bi Monica alisema Julai 14 mwaka huu madiwani na wabunge wawili walifanya ziara ya kushtukiza katika Kata ya Iwela kutokana na hofu iliyokuwepo kuwa baadhi ya vigogo  wamehusika kuwaleta watafiti na wachimbaji hao kinyemela kwa manufaa yao binafsi.
Kwa mujibu wa ratiba baadhi ya kata alizopelekwa kamishna wa madini kanda ya Mbeya kutoa elimu kwa wananchi ni pamoja na Manda, Iwela, Mkomang’ombe, Lugarawa na Mundindi tu badala ya wilaya nzima.
Mwisho

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...