LUDEWA
SERIKALI imetenga
zaidi ya shilingi bilion 6 kwa ajili ya kuboresha usafiri wa Meli katika maziwa
matatu nchini likiwemo Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa ambalo ni
ziwa pekee lenye kero na changamoto kwa wananchi wa Ludewa, Songea na Mbeya.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi Dkt Athumani Mfutakamba alipotembelea Kata ya Masasi
na Manda Wilayani Ludewa kujionea mwenyewe eneo kitakapojengwa kiwanja cha
ndege katika kijiji cha Sagalu kama njia ya kuvutia wawekezaji kufika na
kuwekeza Wilayani humo.
Dkt Mfutakamba
alisema kuwa ujenzi wa uwanja wa ndege Sagalu Wilayani Ludewa utasaidia kwa
kiasi kikubwa kukuza uchumi na kufungua milango ya kimaendeleo zaidi wilayani
humo kutokana na kuwa na utajiri wa madini ya chuma na makaa ya mawe na
dhahabu.
Hata hivyo waziri
huyo aliahidi kuwa ujenzi wa uwanja huo muhimu utaanza mara baada ya wataalam
wa viwanja vya ndege kufika na kulifanyia uchunguzi wa kina eneo hilo.
“Eneo nimeliona
linafaa lakini kama serikali sasa tunaiachia jukumu hili Mamlaka ya viwanja vya
ndege nchini ili kuangalia uwezekano wa kuufufua uwanja huu na kuuboresha
sanjari na uwanja wa ndege Njombe kama njia ya kupanua wigo wa uchumi katika
mikoa ya kusini.”” Alisema Mfutakamba.
Mfutakamba aliainisha
kuwa fedha hizo kwa upande wa Ziwa Nyasa zitatumika kuboresha usafiri wa meli
na kujenga magati na bandari katika mwambao wote wa Ziwa Nyasa ambako hadi sasa
hakuna bandari ya uhakika.
Aliongeza kuwa
wananchi wilayani Ludewa wanaendelea kuyalinda na kuyatazama madini kwa macho
huku wenyewe wakikabiliana na umaskini wa kipato unaosababishwa kwa kiasi
kikubwa na ukosefu wa miundombinu hafifu, kukosekana kwa viwanja vya ndege
ndani ya wilaya hiyo ambapo utajiri ulioko umegeuka mateso kwa wananchi.
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti wananchi wilayani humo wamesema miradi ya Mchuchuma na Liganga
ni moja kati ya miradi mikubwa nchini lakini wakaishangaa serikali kusuasua
kuanza utekelezaji.
Walisema kama miradi
ya makaa ya mawe ya ketewaka, mchuchuma na chuma cha magangamatitu na Liganga
itaanza vijana wengi watapata ajira pamoja na Taifa kuondokana na mgao wa umeme
kwa sababu mradi huo peke yake unaweza kuzalisha megawati 600 hadi 1000.
Pamoja na mradi huo
kuwapatia vijana ajira lakini pia utapunguza umaskini uliokithiri miongoni mwa
wananchi kwa kutoa fursa mbalimbali kama sekta ya biashara kutokana na ongezeko
kubwa la watu wanaotarajia kuja Ludewa kufanyakazi mgodini.
Eneo la Sagalu
linalotarajiwa kujengwa uwanja wa ndege wilayani Ludewa awali katika miaka ya
sabini liliwahi kutumika na Jeshi la Wananchi wa Tanzania ya Ulinzi na Usalama
kipindi cha utawala wa Ngwazi Kamuzu Banda Rais wa kwanza wa Malawi, aliyejiita
wa Muyaya alipojaribu kuchukua ardhi ya Tanzania upande wa Ziwa Nyasa na kusema
ni eneo lake.
MWISHO
No comments:
Post a Comment