Na Friday Simbaya,
Ludewa
DIWANI wa Kata ya Ludewa ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludew, Bi Monica Mchiro juzi alimkana hadharani Mkuu wa Wilaya hiyo Bi Georgina Bundala kutokana na mkuu huyo kutokuweka bayana kilichotokea kati ya wananchi na watafiti wa madini walioingia na mitambo na kuanza shughuli katika Kata ya Iwela bila taarifa kwa madiwani na kuzua hofu na mkanganyiko kwa wananchi.
Bi Monica alifikia hatua hiyo ya kuwaambia wananchi ukweli baada ya Naibu Kamishna wa Madini Kanda ya Mbeya Bw. John Shija kuweka wazi Sheria za Madini na jinsi walivyotekeleza baada ya kutoa leseni ya utafiti katika kata ya Iwela na hatimaye wananchi kugundua kuwa tatizo lilikuwa katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi.
Bi. Monica pamoja na wapigakura wake walikuwa wametega masikio na kutegemea kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo Bi Georgina Bundala angetoa ufafanuzi juu ya utata uliokuwepo kati ya wananchi na wachimbaji madini waliokuwa wameingia na mitambo katika kata hiyo na kuzua utata jambo lililopelekea madiwani wote pamoja na wabunge kufanya ziara ya kushtukiza na kuiingizia hasara halmashauri.
“Ndugu wananchi sisi madiwani wenu tulivyosikia mkanganyo kuhusu watafiti na wachimbaji hao walioko katika Kata ya Iwela tuliamua kufanya ziara ya kushtukiza, lakini tulikuta wahusika wana vibali vyote ikiwemo barua ya Mkuu wa Wilaya. Jambo hili lilituudhi sana kwani kama walikuwa wanajua kwanini wasituambie mpaka Halmashauri ikaingia gharama ya kuwasafirisha madiwani wote 35 bila sababu wangetuambia,” aling’aka Monica.
Awali, Bw. Shija aliwaambia wananchi kuwa baada ya watafiti hao kupewa leseni na kamishna wa Madini Kanda. “Tulimwandikia barua Mkuu wa Wilaya kuwatambulisha kwake ili utaratibu ufuatwe wa kuwafikisha hadi kwa walengwa kijijini.”
“Tukishatambulisha mtafiti au mchimbaji kwa Mkuu wa Wilaya husika siyo jukumu letu tena kufuatilia mamlaka nyingine, lakini sheria inasema kamishna akishatambulisha ugeni kwa Mkuu wa Wilaya ni jukumu lake kuwatambulisha kwa Mkurugenzi na yeye kuwapeleka na kuwatambulusha katika ngazi zote hadi ulipo mradi,”alibainisha Bw Shija.
Madiwani katika baraza kuu waliiomba ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri kumwita kamishna wa madini kanda ili akutane na madiwani hao ili na wao waweze kujiridhisha na kuwaondolea utata uliokuwepo, lakini wakashangaa kamishna huyo akitembezwa na Mkuu wa Wilaya katika baadhi ya Kata wakati Ludewa yote imefunikwa na madini.
Baada ya kamishna kufafanua na kueleza kwa uwazi kuhusu utaratibu ulitumika ndipo maswali yakaanza. “Mimi swali langu ni moja tu kwako Mkuu wa Wilaya naomba ujibu tujue wote kama kweli wewe unatenda kazi zako kwa haki utaratibu na sheria kwanini umemkataze mwandishi wa habari kufanyakazi yake katika mkutano huu wa hadhara,” aliuliza kwa jazba Bw Amani Chaula.
Swali ambalo lilimtesa na kumnyima raha Mkuu huyo na kushindwa kujibu jambo lilizua mashaka kwa wananchi.
“Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wao ni wapita njia tu wanafanya haya kwa maslahi yao binafsi ili baadaye tutakapokuwa tumeanza mvutano kati ya mwekezaji na wananchi wao watakuwa wameshahama,”alilalamika mzee Timoth Mtitu.
Monica aliwaambia wananchi kuwa utaratibu alioueleza Kamishna ni mzuri, lakini sijui kwanini haukufuatwa na viongozi wetu wa Wilaya halafu mbaya zaidi wakauchuna bila kutushirikisha madiwani wote na wabunge.
Monica, “madiwani hawakujua kama watafiti na wachimba madini walioko Iwela walipita na kupata baraka zote kutoka katika ofisi za Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi tungejua tusingekwenda ilikuwa ni aibu tupu tulipofika tulioneshwa vibali vyote ikiwemo barua ya Mkuu,” alisikitika Monica.
Bi Monica alisema Julai 14 mwaka huu madiwani na wabunge wawili walifanya ziara ya kushtukiza katika Kata ya Iwela kutokana na hofu iliyokuwepo kuwa baadhi ya vigogo wamehusika kuwaleta watafiti na wachimbaji hao kinyemela kwa manufaa yao binafsi.
Kwa mujibu wa ratiba baadhi ya kata alizopelekwa kamishna wa madini kanda ya Mbeya kutoa elimu kwa wananchi ni pamoja na Manda, Iwela, Mkomang’ombe, Lugarawa na Mundindi tu badala ya wilaya nzima.
Mwisho
No comments:
Post a Comment