Na Friday Simbaya, Songea
Mamia ya wakazi wa Peramiho wilayani Songea mkoani Ruvuma wamzika mfanyakazi wa kiwanda cha uchapishaji cha Peramiho (Peramiho Printing Press), Mzee Bernhard Mhagama (55) katika makaburi ya Lundusi leo (Alhamisi).
Mzee Mhagama ambaye pia alikuwa kiungo kikuu katika Kiwanda cha Uchapishaji cha Peramiho katika masuala ya kompyuta alifariki dunia tarehe 02.04.2013 baada ya kuanguka ghafla wakati wakielekea kijiji cha Lugarawa kwenye msiba wa mama yake mzazi, ambapo hata hivyo hawakuwahi mazishi.
Ibada ya Misa ya mazishi iliongozwa na Padri Benedict OSB ambaye pia ni Paroko msaidizi wa Parokia ya Peramiho kwa kushirikiana na Paroko wa Parokia ya Lugarawa – Njombe, Pd. Jordan Mwajombe.
Akiongea na Nipashe mdogo wa marehemu Beda Mhagama alisema kuwa baada ya kupata taarifa ya misba kwamba mama yao amefariki walifunga safari yeye na marehemu (Mzee Mhagama) pamoja na baadhi ya ndugu, lakini walipofika mjini Njombe kaka yake alizidiwa na kukimbizwa katika hospitali ya Kibena, Njombe na baadaye kupelekwa hospitali ya misheni ya Peramiho kwa matibabu zaidi kutokana na ugonjwa wa BP ya kupanda, ambapo hata hivyo haikuwezekana kuokoa maisha yake.
“Hapo awali marehemu mzee Mhagama alifiwa na baba mkwe wake,( yaani baba mzazi wa mke wake), ambapo msiba ulikuwa nyumbani kwake katika Mtaa wa Lipinyapinya Kata ya Peramiho, Wilaya ya Songea Vijijni mkoani Ruvuma, lakini kesho yake tena marehemu akapata taarifa ya kufiwa na mama yake mzazi huko Lugarawa, ndipo Jumapili tarehe 28.03.2013 tuliondoka na baadhi ya wanafamilia kuelekea Lugarawa kumzika mama yetu ndipo umauti ukamkuta,” alielezea mdogo wa marehemu.
Marehemu Bernhard Mhagama alizaliwa mwaka 1958 huko kijiji cha Lugarawa, Njombe. Alimaliza shule ya msingi mwaka 1974 ambapo baadaye alijiunga na ufundi uwashi huko Uwemba mwaka 1975 – 1976.
Mwaka 1978 alijiunga na Kiwanda cha uchapishaji cha Peramiho (Peramiho Printing Press), mwaka 1980 marehemu alifunga ndoa katika Kanisa la Kitawa la Abasia ya Peramiho. Marehemu ameacha mke na watoto nane (8), wa kiume wanne na wa kike wanne, na wajukuu watano.
Kabla ya kifo chake marehemu alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa BP ya kupanda tangu 2000 hadi mauti yalipomfika asubuhi ya tarehe 02.04.2013 katika hospitali ya Mtakatifu Joseph – Peramiho.
Wakati huohuo, mkuu wa kiwanda cha uchapishaji Peramiho Br. Sylvester Ndoga OSB, ambacho kinamilikiwa na Peramiho Benedictine Fathers, alimuelezea marehemu kama mtu aliyefanya kazi kwa moyo wote ambaye hakuwahi kuchelewa kazini, na pia alikuwa na ushirikiano mzuri na wafanyakazi wenzake.
Mwisho