Wednesday, 27 November 2013

TATIZO LA MIMBA KWA WANAFUNZI PERAMIHO TISHIO




Na Friday Simbaya, Songea

Asumpta Magunga mwenye miaka kumi na saba (17) wa Kijiji cha Peramiho, Wilaya ya Songea (V) mkoani Ruvuma amezaa mtoto asiyekuwa na ngozi tumboni, yaani amezaliwa na viungo vyote vya ndani vinaonekana wazi  kwa kitaalamu wanaita (congenital malfunction) katika Hospitali ya Mtakatifu Joseph Peramiho.
Magunga ambaye alikuwa ni mwanafunzi wa Kidato cha Pili Shule ya Sekondari Namihoro, willayani Songea Vijijini mkoani Ruvuma ni mkazi wa mtaa wa Lihangano katika kijiji cha Peramiho alijifungua mtoto bila ngozi ya tumboni, lakini bahati mbaya mtoto huyo hakuishi muda mrefu alifariki dunia Jumapili tarehe 24 Novemba mwaka huu.
Nilipopata taarifa kuhusu kuzaliwa kwa mtoto wa ajabu mwenye kuzaliwa na viungo vya ndani vikiwa nje nilichukuwa kamera ya ofisini na kukimbia mara moja hospitalini kupata picha na maelezo kidogo kuhusiana na tukio lenyewe.
Nilipofika pale hospitali nilikwenda moja kwa moja kwenye ofisi ya Muuguzi Mkuu, Romanus Mgimba ambaye naye akanielekeza niende wodi ya kinamama Chumba Namba Tatu (3), ambapo alilazwa mama huyo ndipo nikakutana na Muuguzi Mkunga, Odila Kapinga na aliyenionesha mtoto wa ajabu wa  jinsia ya kike aliyezaliwa na utumbo nje.
Nilitaka kupata maelezo ya kitaalam kuhusiana na tatizo hilo, lakini juhudi za kumuona daktari ili kuelezea tukio lenyewe ziligonga mwamba baada ya kuambiwa nisubiri mpaka hapo watakapokuwa na taarifa kamili.
Hata hivyo tatizo la mimba za utotoni hapa Peramiho linaendelea kukua siku hadi siku kama ambavyo wadau mbalimbali wanaelezea kwamba kila  kona upitapo utaona mabinti wenye umri chini ya miaka 19 wakiwa wamebeba watoto migongoni, ambapo chanzo chake kikielezwa kuwa ni umasikini pamoja na mmomonyoko wa maadili katika familia nyingi.
Katekista George Millinga ni katekista wa Parokia ya Peramiho ambaye pia ni mwalimu wa dini anayefundisha soma la dini katika shule za sekondari na taasisi mbalimbali za hapa Parokia ya Peramiho, Jimbo Kuu la Songea.
Amesema kuwa tatizo la mimba za utotoni Peramiho linaongezeka siku hadi siku, ambapo alielezea chanzo kikubwa ni umasikini na mmomonyoko wa maadili kwa familia nyingi za hapa Peramiho.
Amesema watu wengi  hapa Peramiho hawapendi kujishughulisha na kazi kwa kutegemea misaada mbalimbali kutoka mahali fulani na matokeo yake watu wanatumia kutatua umasikini kwa njia isio halali.
Vijana wengi wamekuwa mbali na Mungu kwa kutoshika maadili ya kidini na kupenda kuanza mapenzi katika umri mdogo badala ya kusubiri hadi hapo watakapofunga ndoa wakishakomaa, na zinaa au uasherati kidini ni dhambi.
“Tatizo kubwa ninavyojua mimi watu wengi wanatumia uasherati kwa kutatua matatizo yao ya umasikini, hawapendi kujituma kazi wanapenda zaidi kupata fedha kwa njia isio halali kwa kutegemea misaada kutoka sehemu na mapato yake ni  hizo mimba za utotoni…” amesema Kat. Millinga.
Amesema kitu kingine kinachochangia tatizo la mimba za utotoni ni wazazi wenyewe kwa sababu hawawafundishi watoto wao maadili mema na kuwa watoto wakirandaranda mitaani bila msaada wowote.
Kat. Miliinga ameshauri Serikali itoe adhabu kali kwa  mtu yeyote anayempa mimba mtoto mdogo na mwanafunzi kwa  sababu huko ni kuharibu taifa la baadaye na mtu kama huyo anastahili  apewe adhabu sawa na mauaji.
“Mtu anayempa mimba msichana mwenye umri mdogo afananishwe na mtu mwenye kosa la mauaji kwa  sababu anaharibu taifa la baadaye, anaharibu afya ya mtoto vile viungo vya uzazi havijakomaa sawa sawa,” amesema Kat. Millinga.
Ameshauri  walimu na wazazi wasichoke kukemea maovu kwa wanafunzi na kuwapa maadili mema na wazazi ili kupunguza tatizo la mimba za utotoni.

Ongezeko kubwa la mimba za utotoni Tanzania

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na idadi ya watu UNFPA limezindua ripoti yake na kuitaja Tanzania kama moja ya nchi ambazo zinakabiliwa na ongezeko kubwa la mimba za utotoni na hivyo kuwafanya wasichana wengi kukatiza masomo yao.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa hivi karibuni imeangazia hali ya idadi ya watu na kusema kuwa kati ya mimba milioni moja zinazotungwa nchini Tanzania, asilimia 23 ya mimba hizo zinawahusu wasichana walio chini ya umri wa miaka 19.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, idadi ya watoto wa kike wanaopata mimba bado ni kubwa na kwamba takwimu za sasa zinaonyesha kuwa kila kwenye wasichana 10, 4 kati yao wamepata mimba.
Baadhi ya mambo yaliyotajwa kusababisha hali hiyo ni pamoja na kuwepo kwa mila potofu ambazo zinawakandamiza na kuwabagua watoto wa kike. Jambo jingine lililoelezwa na ripoti hiyo ni kuendelea kuongezeka kwa ndoa za utotoni ambazo hutumika kama kigezo cha kujipatia mali kwa baadhi ya wazazi.
Alanna Armitage Mkurugenzi wa UNFPA mjini Geneva amesema mimba za utotoni huathiri afya, elimu na haki za mtoto wa kike. Ameongeza kuwa mtoto wa kike asiye na elimu atakuwa na ugumu kupata ajira na kujijengea maisha bora na familia yake.


 Caption
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Namihoro wilayani Songea vijijini, mkoani Ruvuma, Asumpta Magungu (17) mkazi wa Kijiji cha Peramiho akimuangulia mtoto wake huruma katika wodi ya kinamam Chumba Namba Tatu (3) Hospitali ya Mtakatifu Joseph Peramiho hivi karibuni. Picha ndogo ni sehemu ya mtoto huyu aliezaliwa bila ngozi ya tumboni. (Picha na Friday Simbaya)

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...