Na Friday Simbaya,
Ludewa
Wananchi wa
Kijiji cha Mlangali Kata ya Mlangali wilayani Ludewa, mkoani Iringa wameiomba
serikali iwafungulie zahanati yao waliyoijenga
kwa nguvu zao wenyewe ili waweze kupata
huduma ya afya jirani, kwa sasa
wanalazimika kutembea umbali mrefu kutafuta matibabu katika Kituo Cha Mlangali ambacho kipo zaidi ya kilometa nne.
Wakiongea na
Nipashe jana Mwenyekiti wa Kijiji cha Mlangali Bw. David Mtitu na Mtendaji wa Kijiji
(VEO) Bw. Leo Mlelwa kwa pamoja walisema
kuwa wananchi wa kijiji hicho wanapata shida sana kupata huduma ya afya
kutokana na kijiji chao kukosa zahanati,
wakati wana zahanati yao waliyoijenga kwa nguvu zao. Walisema kuwa zahanati yao
hipo tayari ,lakini hadi sasa haijafunguliwa.
“Pamoja na
kuitikia wito wa Serikali wa kutaka kila kijiji kuwa na zahanati na sisi kama wanakijiji
cha Mlangali tuliitikia wito huo na tukaamua kujenga zahanati yetu, lakini cha
kushangaza zaidi ni kwamba hadi sasa haijafungiliwa pamoja na kuwa kila kitu kimekamilika, ikiwa ni pamoja na
nyumba ya mganga,” walisema viongozi hao.
Walisema kuwa
kila kitu kimekalika mpaka nyumba ya mganga na choo, lakini cha cha ajabu ni
kwamba zahanati bado haijazinduliwa kwa
ajili ya kutoa huduma ya afya kwa mwanachi wa kijiji cha Mlangali, ili
kuwapunguzia wananchi adha ya kutembea mwendo mrefu kutafuta matibabu.
“Tuna mengi
ya kuzungumza, lakini kwa leo ngoja tuseme haya machache tu….. kuna kipindi
tunapata shida kuwasafirisha wagonjwa wetu hadi Kituo cha afya Mlangali ambacho
kipo umbali wa kilometa zaidi ya nne (4km), na pengine kabla ya kufika kituo
cha afya chenyewe mgonjwa anafia njiani. Kumbe kungekuwepo na zahanati jirani
matatizo kama haya yanapungua, ndiyo maana tunaomba serikali yetu iharakishe
kutufungulia zahanati yetu kwa sababu kila kitu kipo tayari mpaka nyumba ya
mganga pamoja na choo,” walisema viongozi hao.
Zahanati ya
Mlangali iliyopo Kijiji cha Mlangali ilianza rasmi kujengwa mwaka
2008 na kukamilika mwaka 2010 kwa
gharama ya shilingi 19,194,000/-, ambapo nguvu za wananchi zilikuwa ni shilingi
14,140,000/-, Halmashauri ya Ludewa ilichangia shilingi 3,800,000/- na pesa ya wahisani
ni shilingi 1,254,000/-.
Kijiji cha Mlangali
ni moja ya vijiji saba vya Kata ya Mlangali ambacho kina wakazi zaidi ya 2,360, vijijii vingine katika kata hiyo ni pamoja na Itunda,
Lufunbu, Ligumbilo, Masimbwe, Mkiu na Kiyombo. Kijiji cha Mlangali kina shule
mbili tu ambazo ni Shule ya Msingi ya Itunda na Shule ya Sekondari ya Ulayasi.
Kwa upande
wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ludewa (DMO), Dkt. Happiness Ndosi alisema kuwa ,
serikali tayari iko mbioni kuifungua zahanati hiyo ya Mlangali na taratibu zote
zimekamilika kilichobaki ni kupeleka
mganga na madawa. Alisema kuwa mganga tayari huyo, lakini wanasubiri taratibu zingine
zikamilike ili kuweza zahanati hiyo
kuanza kufanyakazi.
Alisema kuwa
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imetoa kibali cha kufunguliwa rasmi kwa Zahanati ya Mlangali, ambayo ilikamilika tangu
mwaka 2010.
“Wananchi
wa Kijiji cha Mlangali wasiwe na
wasiwasi kabisa kwa sababu mganga wa zahanati hiyo tayari na pesa tayari zipo kwa ajili ya madawa kutoka Bohari ya Madawa ya Serikali
(MSD),” alisema Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt. Ndosi.
Wakati huohuo,
Zahanati ya Kijiji cha Mawengi nayo pia inakabiliwa na uhaba wa nyumba ya
mganga pamoja na choo cha uhakika, na
kwa sasa zahanati hiyo inatumia choo cha muda.
Mwisho