Saturday, 19 March 2016

TOM MBOYA SAUTI YA WANYONGE ILIYOZIMIKA GHAFLA…!!!





Thomas Joseph Odhiambo Mboya (pichani), alikuwa ni mmoja wa waasisi wa Chama cha Kenya African National Union (Kanu)

Wakati anauawa, Tom Mboya, alikuwa ni Waziri wa Mipango ya Uchumi na Maendeleo. Pia alikuwa ni mwanasiasa aliyepewa nafasi kubwa ya kuja kuwa rais wa nchi hiyo baada ya Kenyatta.


Mboya alizaliwa Agosti 15, 1930 huko Kilima Mbogo karibu na Mji wa Thika katika maeneo ambayo wakati ule yalikuwa yanaitwa White Highlands.

Alisoma na kupata elimu ya juu, akaenda Uingereza na kurejea Kenya mwaka 1956 akafanya kazi na kujiunga na siasa. Wakati huo Waingereza walikuwa wanajaribu kulidhibiti wimbi la wapigania uhuru wa Mau Mau, waliokuwa wanataka ardhi yao na uhuru wa Kenya.

Aliajiriwa na Halmashauri ya Jiji la Nairobi, akajiunga na Chama cha Wafanyakazi cha African Staff Association na kuchaguliwa kuwa rais wa chama hicho ambacho kikaitwa Kenya Local Government Workers Union.

Aliingia katika bunge ambalo miongoni mwa wabunge 50, Waafrika walikuwa nane tu.

Katika medani ya kimataifa, akachaguliwa kuwa mwenyekiti wa All-African Peoples Conference nchini Ghana, ambao uliitishwa na Kwame Nkrumah. Wakati huo Mboya alikuwa na umri wa miaka 28 tu.

Mnamo1959, alianzisha mchakato wa kupeleka Waafrika kusoma nchini Marekani, ambapo wanafunzi 81 walihusika.

Juhudi hizo za Mboya zilimfanya Rais John Kennedy wa Marekani mwaka 1960, kujumuisha pia wanafunzi kutoka Uganda, Tanganyika (Tanzania) na Zanzibar, Rhodesia ya Kaskazini (ambayo sasa ni Zambia) Rhodesia ya Kusini (sasa ni Zimbabwe) na Nyasaland ambayo sasa ni Malawi.

Mradi huo uliwezesha wanafunzi 230 wa Afrika kupata masomo nchini Marekani mwaka 1960 ambapo mamia zaidi walifuatia mwaka 1961.

Yote hayo yalizidi kumpa Mboya umaarufu mkubwa machoni mwa umma na akazidi kushika nyadhifa za juu kila kukicha.

Ni katika Mtaa wa Independence Avenue (ambao sasa ni Moi Avenue), mchana wa Julai 5, 1969 ambapo Nashon Isaac Njenga Njoroge alimpiga risasi na kumuua akiwa anatoka katika duka moja la madawa.

Mboya, aliyekuwa na umri wa miaka 39, alikufa papo hapo.

Mboya aliacha mke (Pamela) na watoto watano. Alizikwa katika kaburi maalum kwenye Kisiwa cha Rusinga. Kaburi hilo lilijengwa mnamo mwaka 1970.

Pamela, ambaye baadaye alizaa mtoto mmoja aitwaye Tom Mboya Jr na kaka wa marehemu Tom Mboya aitwaye Alphonce Okuku, naye alikufa mwaka 2009 wakati akitibiwa huko Afrika Kusini.

MAGAZETI YA LEO JUMAMOSI
























WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...