Rais wa chama cha wakunga nchini (TAMA), Feddy Mwanga akimkaribisha Ofisa Mtendaji mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wakunga duniani, Frances Ganges (kulia) kuzungumza na wakunga nchini waliokusanyika kwenye mdahalo wa siku moja kuelekea sherehe za kilele cha maadhimisho ya siku ya Wakunga Duniani ambapo kitaifa imefanyika mjini Musoma mkoani Mara. Kushoto ni Kaimu Muuguzi mkuu wa serikali kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Ama Kasangala. (Picha zote na Zainul Mzige wa modewjiblog)
Na Mwandishi wetu, Musoma
Ofisa Mtendaji mkuu wa Shirikisho la Vyama vya wakunga duniani, Frances Ganges, ametoa wito wa wakunga na wauguzi kubadilisha uzoefu wa shughuli zao ili kuhakikisha taifa linaondokana na vifo vya wanawake wajawazito na watoto.
Akizungumza katika mdahalo kuelekea sherehe za kilele cha maadhimisho ya siku ya wakunga duniani, iliyofanyika kitaifa mkoani Mara, Ganges alisema kwamba ni wajibu wa wakunga kuhakikisha kwamba dunia ya kesho inakuwa bora na wanaweza kwa kushirikiana na kubadilishana uzoefu.
Alisema dunia inawategemea wauguzi kuendeleza kizazi cha binadamu na katika kufanya hivyo kuna changamoto nyingi zinazotokea changamoto ambazo zinaweza kumalizwa kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake katika eneo analofanyia kazi.
Aliutaja wajibu huo kama uongozi, uelimishaji na pia utendaji wa kazi wenye tija na busara.
Alisema nia ya siku ya wakunga ipo wazi ni kuleta ushirikiano kwa ajili ya kuleta dunia iliyo njema ya kesho.
Mtendaji huyo wa Shirikisho hilo lenye makao makuu yake nchini Uholanzi alisema kwamba wanafuraha kubwa kusikia mambo makubwa yanayofanywa na wakunga nchini Tanzania pamoja na changamoto zake zilizopo.
Alisema mafanikio yaliyopo ni matokeo ya ushirikiano na ufanyaji kazi wa pamoja.
Ofisa Mtendaji mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wakunga duniani, Frances Ganges akizungumza na Wakunga nchini Tanzania waliohudhuria kwenye mdahalo wa siku moja uliofanyika kwenye ukumbi wa Mara ofisi za Mkuu wa mkoa wa Mara mjini Musoma kuelekea kilele cha sherehe za maadhimisho ya siku ya Wakunga duniani kujadili changamoto zinazowakabili Wakunga nchini. Katikati ni Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA), Feddy Mwanga na Kushoto ni Kaimu Muuguzi Mkuu wa Serikalim kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Ama Kasangala.
Alisema katika hotuba yake hiyo kwamba wakunga wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha watoto wanazaliwa salama, wanawake wanakuwa salama na kizazi cha binadamu kinakuwa salama.