Mmiliki na mwendeshaji wa kipindi cha Tuwalinde Watoto Wetu, Janet Mwenda.
Na Rabi Hume, Modewjiblog
Kipindi cha Tuwalinde Watoto Wetu kilichokuwa kikirushwa na Clouds TV, Alhamisi ya wiki hii kinatarajiwa kuanza tena kuonekana kupitia Clouds TV Alhamisi ya Disemba 10, saa tatu kamili usiku.
Akizungumza na Dewjiblog, Mmiliki na mwendeshaji wa kipindi hicho, Janet Mwenda amesema kuwa kipindi cha Alhamisi hii kinatarajiwa kuja na kitu kipya tofauti na vile walivyokizoea kuonekana hapo awali na hivyo kuwataka watazamaji kukaa tayari kuona kipindi bora kuhusu watoto na changamoto wanazokutana nazo.
Amesema lengo la kipindi hicho ni kuwakumbusha wazazi na walezi majukumu yao kwa watoto wao na hatari wanazoweza kukutana nazo pindi wasiposimamiwa vizuri na watu wanaoishi nao na kupitia kipindi hicho wanaweza kuona maisha wanayokutana nayo watoto hao pindi wanapokuwa nje ya familia zinazowalea.
“Kuna mambo jamii inakuwa haiyaamini kama yanatokea na tunachofanya ni kujaribu kuionesha jamii ni mambo gani yanawatokea watoto wanapokuwa mtaani na tunachotaka ni wazazi watambue hatari hiyo na waweze kuwalea vizuri watoto awe wa kwako au wa mwenzako,” amesema Janet.
Akizungumzia kipindi cha Alhamisi hii, Janet amesema kipindi cha wiki hii kitakuwa kinamuhusu kijana wa miaka 16 aliyekuja Dar es Salaam kutafuta maisha baada ya kutoroka nyumbani kwao na kujiunga na makundi mabaya ya vijana ambayo yalipelekea kuanza kujiingiza katika vitendo vya kimapenzi na wanawake wanaofanya biashara ya kuuza mwili na kuwa katika hali ya hatari ya kupata magonjwa ya zinaa.
Kujua kilichofuata baada ya kujiingiza katika vitendo hivyo na hali aliyonayo sasa kijana huyo usikose kutazama kipindi hicho alhamisi hii, Disemba 10 kupitia Clouds Tv!!!
USIKOSEEE!!