Mbeya: Mkurugenzi na kiongozi wa taasisi ya dini ya Daily Bread Life Ministry Tanzania, Mchungaji James Mpeli Mwaisumbe amewasihi watanzania kumuombea Rais Dkt John Pombe Magufuli ili aweze kuliongoza taifa kwa haki, amani na upendo.
Alisema kuwa ili Tanzania iweze kusonga mbele, waislamu, wakristo,viongozi wa siasa, serikali na watanzania kwa ujumla lazima waliombee taifa na viongozi wake kwa Mungu ili kuweza kudumisha amani na mshikamano viliyopo.
Mchungaji Mpeli alisema hayo wakati wa sherehe ya kumuaga Mchungaji Raphael Mwasifiga wa Kanisa la Baptist, Kanani lililopo Sinde Makunguru, Mwanjelwa jijini Mbeya.
Mchungaji huyo mwalikwa alisema kuwa anavutiwa na kiongozi wa nchi kwa sababu ni mcha Mungu na katika maneo yake kumi anayozungumza hakosi kumtaja Mungu.
Alisema kuwa taifa ni kitu cha muhimu kuliko vya vyama siasa na kuwaomba wakristo, waislamu viongozi wa siasa na serikali kuliombea taifa ili amani na mshikamano ambayo havipatikani Afrika isipokuwa Tanzania viweze kudumu.
“Kiongozi mwenye hofu ya Mungu ni yule ambaye anajinyenyekeza na kujishusha kama Yesu Kristo alivyo jinyenyekeza msalabani,” alisema Mchungaji Mpeli.
Alisema kuwa Tanzania imekuwa ikisifiwa na mataifa mbalimbali kuwa ni nchi yenye amani duniani lakini amani, upendo na mshikamano viweze kudumu ni lazima viongozi wawe na hofu na kuwa wanyenyekevu kwa kuutafuta uso wa Mungu.
Aidha, Mchungaji Mpeli katika ibada maalumu ya kumuaga mchungaji mwenzake Raphael Mwasifiga, iliyofanyika tarehe 29.08.2016 alisoma neno la Mungu kutoka katika Kitabu cha 2 Mambo ya Nyakati 7: 14.
Neno la Mungu linasema hivi, “ ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.”
Kuhusu hali ya siasa nchini, Mchungaji Mpeli Mwaisumbe amevitaka vyama vya siasa vitangulize maslahi ya taifa mbele na vyama vya siasa baadaye ili kuepusha vurugu kutokea nchini.
Alisema kuwa vyama vya siasa vinatakiwa kukaa chini kutafuta suluhu ya mvutano unaoendelea kuhusu operesheni ya Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta) ili kuepusha vurugu kutokea nchini.
Mchungaji huyo alimuomba pia msajili wa vyama vya siasa nchini kuwa asichoke kukemea na kuvionya vyama vyote vya siasa bila upendeleo wowote.
Kwa upande wake, Mchungaji Mstaafu Raphael Mwasifiga wa Kanisa la Baptist Kanani la Makunguru Sinde, Mwanjelwa mkoani Mbeya alisema kuwa serikali na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wanatakiwa kukaa chini kutafuta suluhu ya mvutano unaoendelea kuhusu operesheni ya Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta) ili kuepusha vurugu kutokea nchini maandamano hayo yatakapofanyika.
Mchungaji huyo, alisema ili kuepuka machafuko yanayoweza kutokea wakati wa kutekeleza operesheni hiyo Septemba mosi, mwaka huu, huku Jeshi la Polisi likisema litauvunja Ukuta ni vyema pande zote mbili zikajadiliana na kupata muafaka.
"Hakuna jambo lililoshindikana mezani, tunaiomba serikali ikae mezani na viongozi wa Chadema ili kumaliza tofauti," alisema.
Mchungaji Mwasifiga alizaliwa mwaka 1953 katika kijiji cha Lukule Kiwira Tukuyu wilayani Rungwe, mkoani Mbeya akiwa ni mtoto wa saba na wa mwisho katika familia ya Mzee Mwasifiga.
Mchungaji Mwasifiga alikuwa mchungaji mwanzilishi wa Kanisa la Baptist Kanani Makunguru Sinde maeneo ya Mwanjelwa jijini mbeya tangu mwaka 1992 na alimshukuru Mungu kwa kumaliza salama.