Marekani na Korea Kaskazini zimeendelea kujibizana vikali, ambapo safari ya meli za kivita za Marekani ikiwemo meli yenye uwezo wa kubeba ndege za kivita ya Carl Vinson imeibua hisia kubwa na uwezekano wa Marekani kufanya shambulio la mapema kujaribu kulemaza mfumo wa kijeshi wa Korea Kaskazini.
Wakati taarifa hizo zikienea, imebainika kwamba meli hizo za kivita za Marekani hazikuwa zinaelekea upande wa Korea Kaskazini kama ilivyoripotiwa awali, bali zilikuwa zinaelekea eneo tofauti.
Awali iliripotiwa kuwa, Jeshi la wanamaji la Marekani lilikuwa likielekea Korea kama hatua ya kuionya Korea Kaskazini, ambapo Rais Trump pia alitangaza kwamba kundi kubwa la meli za kivita lilikuwa likitumwa eneo hilo, hivyo imebainika kuwa si kweli.
Hadi kufikia mwishoni mwa wiki, meli hizo zilikuwa zimesafiri mbali sana na rasi ya Korea na zilikuwa zinapitia mlango wa bahari wa Sunda kuingia katika Bahari ya Hindi.
Wakuu wa jeshi la wanamaji la Marekani katika Bahari ya Pasifiki walisema Jumanne kwamba walikuwa wamefutilia mbali safari ya meli hizo katika bandari ya Perth.
Kundi hilo la meli sasa "linaelekea Magharibi mwa Pasiki kama lilivyoamrishwa".
Bado haijabainika iwapo kulitokea sintofahamu katika mawasiliano au labla Marekani ilipotosha watu makusudi kujaribu kumtia wasiwasi kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un.
Aidha, Marekani imesema Korea Kaskazini ilipotekeleza jaribio la kombora ambalo lilifeli mwishoni mwa wiki ilikuwa na nia fulani ya kiuchokozi.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, James Mattis amesema Marekani inafanya kazi kwa karibu na China kukabiliana na Korea Kaskazini. Amesema kuwa jaribio hilo lililofanywa na Korea Kaskazini lilikuwa la kutojali na ilifanya hivyo kwa kuichokoza Marekani.
Aidha, Korea Kaskazini wamesema kuwa itafanya majaribio ya makombora kila wiki na pia ikaonya kwamba kutatokea vita kamili iwapo Marekani itaichukulia hatua za kijeshi.
“Iwapo Marekani wanapanga kutushambulia, tutajibu kwa shambulio la nyuklia kwa mtindo na njia yetu wenyewe,” amesema Naibu waziri wa mambo ya nje wa Korea Kaskazini, Han Song-ryol
Pande zote mbili zimekuwa zikijibizana vikali baada ya Korea Kaskazini kufanya jaribio hilo la makombora.
Bw Mattis alisema kwamba jaribio hilo la Jumapili halikuhusisha kombora linaloweza kuruka kutoka bara moja hadi jingine lakini bado lilikuwa ishara ya kutojali.
“Inadhihirisha ni kwa nini tunafanya kazi kwa karibu kwa sasa na Wachina…tunajaribu kudhibiti hali hii na lengo letu ni kumaliza silaha za nyuklia katika rasi ya Korea,” alisema.
Credit:BBC