Mashambulizi yaliyotokea jana katika mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels yameendelea kuakisiwa na kulaaniwa sana katika vyombo vya habari na duru za kimataifa.
Baada tu ya mashambulizi hayo yaliyolenga uwanja wa ndege wa Zaventem mjini Brussels na kituo cha treni ya chini kwa chini, Baraza la Usalama wa Taifa la Ubelgiji lilikutana na kujadili kadhia hiyo. Takwimu zinasema kuwa, hadi sasa watu wasiopungua 34 wameuawa katika mashambulizi hayo na wengine zaidi ya 190 kujeruhiwa. Kundi la kigaidi la Daesh limetangaza kuwa limehusika na mashambulizi hayo.
Mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea jana mjini Brussels yanafuatia yale yaliyotokea Paris, Ufaransa miezi ya Januari na Novemba mwaka jana. Mashambulizi hayo kwa mara nyingine tena yamepiga kengele ya hatari kwa viongozi wa masuala ya kisiasa na kiusalama juu ya tishio kubwa la makundi ya kigaidi na kitakfiri barani Ulaya.
Siku kadhaa zilizopita askari usalama wa Ubelgiji walimtia nguvuni Salah Abdulsalam ambaye inasemekana ni miongoni mwa wanapangaji wakuu wa mashambulizi ya mwaka jana mjini Paris. Hata hivyo mshirika wa gaidi huyo alitoroka; kwa msingi huo polisi ya Ubelgiji ilitahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea mashambulizi ya kigaidi.
Maafisa wa polisi ya Ubelgiji wanasema Abdulsalam alikuwa na mpango wa kutekeleza mashambulizi kadhaa ya kigaidi katika jiji la Brussels.
Mashambulizi ya jana nchini Ubelgiji yamezilazimisha nchi nyingine za Ulaya kupandisha juu daraja ya tahadhari ya usalama. Mashambulizi hayo ya kigaidi ambayo tunaweza kusema taathira zake kwa nchi ndogo ya Ubelgiji ni sawa na za tukio la Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani, yatapelekea kufanyika mabadiliko makubwa katika muundo wa vyombo vya upelelezi na usalama nchini humo na kuziathiri nchi nyingine za Ulaya.
Baada ya mashambulizi ya Paris mawaziri wa mambo ya ndani wa Ulaya walikutana mara kadhaa kupanga mikakati mipya ya kuzidisha usimamizi katika mipaka na raia wa nchi hizo. Lengo na mikutano hiyo ni kupunguza vitisho vya ugaidi hususan kutoka kwa raia wa nchi za Ulaya waliojiunga na makundi ya kigaidi ya kitakfiri katika nchi za Syria na Iraq na baada ya kurejea katika nchi zao sasa wanatekeleza mashambulizi ya mara kwa mara ya kigaidi. Pamoja na hayo inaonekana kuwa, hatua zilizochukuliwa na mawaziri wa mambo ya ndani wa nchi za Ulaya hazikutosha na magaidi hao wameendelea kutekeleza mashambulizi barani Ulaya.
Maafisa wa masuala ya usalama barani Ulaya wanasema, zaidi ya raia elfu tano wa nchi hizo wamejiunga na makundi ya kigaidi yanayopigana katika nchi za Iraq na Syria na baadhi yao tayari wamerejea katika nchi zao. Kurejea kwa magaidi hao ambao wengi wao bado ni wanachama wa makundi ya kigaidi kama lile la Daesh, kumefuatiwa na mashambulizi kadhaa makubwa ya kigadi barani Ulaya likiwemo lile la tarehe 13 Novemba lililofanywa na wanachama wa kundi la Daesh ambalo liliua watu zaidi ya 130.
Wakati huo huo Polisi ya Ulaya (Europol) ilisema hapo awali kuwa tathmini ya mazungumzo ya maafisa wa usalama wa bara hilo inaonesha kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa kutokea mashambulizi ya kigaidi wakati wowote ule katika nchi za bara hilo.
Pamoja na hayo yote hatupasi kusahau kwamba, watu wa Ulaya sasa wanavuna matunda ya mche walioupandikiza wenyewe huko Syria kwa kuyaunga mkono na kuyafadhili makundi ya kigaidi kama Daesh dhidi ya serikali halali ya Bashar Assad.
Baada ya mashambulizi ya Brussels inatazamiwa kuwa kutafanyika mabadiliko makubwa si katika taasisi na mikataba ya Ulaya pekee kama ule wa Schengen bali pia mazingira na masuala ya kijamii na mitandao ya intaneti itatawaliwa zaidi na anga ya kipolisi na kiusalama katika nchi za bara la Ulaya. (BARAKA NYAGENDA)