LUDEWA
MKUU wa Wilaya ya
Ludewa Bi. Georgina Bundala amepiga marufuku kwa muda usiojulikana kuchinja au
kula na kusafirisha nguruwe pamoja na mazao yake kama vile nyama, mifupa,
nywele na mazao ya kusindika kutokana na homa ya nguruwe kupiga hodi tena
wilayani humo.
Bi. Bundala alisema
endapo mfanyabiashara au mfugaji yeyote atabainika akisafirisha nguruwe kutoka
katika maeneo yaliyoathirika na kupeleka maeneo yasiyoathirika mtu huyo atakuwa
amekiuka agizo na hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Aidha amewaagiza
wataalamu wote wa kilimo na mifugo, maafisa watendaji kata na vijiji kusimamia
agizo hili ili kuwathibiti wale wote wasiokuwa waaminifu wanaosafirisha nyama
ya nguruwe kwa siri wakidhani wanajificha.
Akitoa taarifa na
takwimu za ugonjwa huo kwa Mkuu wa Wilaya, Daktari wa Mifugo wilayani Ludewa
Bw. Festo Mkomba alisema maambukizi mapya ya homa ya nguruwe yametokea katika
tarafa ya Mwambao wa Ziwa Nyasa na sasa yapo katika tarafa ya Mawengi.
Dr. Mkomba alisema tangu
ugonjwa huo uingie wilayani Ludewa tayari nguruwe 612 kati ya nguruwe 2,356
waliopo wilayani humo wameshakufa na kwamba Lumbila wamekufa 154, Lupingu 214,
Kilondo 148 na Mawengi 40 na kusema kasi hiyo ni kubwa sana kiuchumi.
Katika tangazo lake
kwa wananchi Bw. Festo Mkomba ambaye ni Daktari wa mifugo wilayani Ludewa
alisema kuanzia Septemba 20 mwaka huu Wilaya ya Ludewa itakuwa chini ya
karantini mpaka hapo itakapotangazwa vinginevyo kutokana na matukio ya homa ya
nguruwe kujitokeza tena wilayani Ludewa.
Awali, Bw. Marco
Mhagama mtaalamu wa mifugo alisema wafanyabiashara, wafugaji na walazi ndio
wanaosababisha kurudiarudia kwa ugonjwa huo kwani wamekuwa na tabia ya kupuuzia
maelekezo wanayopewa na wataalamu wa mifugo juu ya kukabiliana na homa ya
nguruwe.
Bw. Mhagama alisema
kuwa kimsingi na kitaalamu homa ya nguruwe haina madhara ya moja kwa moja
katika afya ya binadamu, lakini wananchi wengi wilayani Ludewa wanategemea
mifugo hiyo katika kuinua uchumi na kuongeza kipato chao.
“Februari mwaka huu
katantini kama hiyo iliwekwa baada ya ugonjwa huo kuua idadi kubwa ya nguruwe
na baadaye mwezi June tuliruhusu kuanza kuchinjwa na kula, lakini wananchi
wenyewe wamekuwa wazembe kwa kukosa uaminifu,” alisema mhagama.
Homa ya mafua ya
nguruwe siku zote imekuwa ikiingia wilayani Ludewa kupitia vijiji vilivyopo
kandokando ya Ziwa Nyasa na kwamba asili ya
ugonjwa huo ni kutoka nchi jirani ya Malawi kupitia wafanyabiashara wa Kyela,
hivyo kuna kila sababu ya serikali kuongeza nguvu ya ziada katika kuthibiti
homa hii katika maeneo hayo.