Saturday, 22 March 2014

ATAKAYETUKANA MATUSI HADHARANI KUPIGWA FAINI ELFU HAMSINI



Na Friday Simbaya, Songea
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mlimani katika Kijiji cha Peramiho ‘B’ wilayani Songea, mkoani Ruvuma, Bonventura Mhagama kwa kushirikiana na katibu wake, Asante Mbawa amesema  mwananchi  atakeyetukana matusi hadharani atatozwa faini ya shilingi elfu hamsini.
Alisema kuwa kumezuka tabia kwa baadhi ya watu kitongojini kwa makusudi wameamua kutoa matusi ya nguoni hadharani kwa kisingizio cha kulewa pombe.
Mwenyekiti huyo alisema hayo jana wakati wa mkutano wa kitongoji, ambapo alisisitiza kwamba ni wakati wa kutumia sheria ndogondogo kukomesha tabia ya watu kutukana matusi baada ya kutofautiana kauli.
“Ni lazima tuishi katika jamii inayozingatia maadili, mtu mzima unapoporomosha matusi hadharani unamfundisha ni nini mtoto?”  alihoji mwenyekiti huyo.
Alisema kitendo hicho katika kitongoji hakitavumilika kwa sasa kwa sababu sheria ndogondogo zitatumika kumshitaki mtu yeyote atakayetukana mwenzake ili mradi kuwepo na ushahidi.
Katika mambo mengine mwenyekiti wa kitongoji alitoa rai kwa  wananchi wa kitongoji hicho wawe makini na wageni wanaofika katika maeneo kwa kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarishwa katika kitongoji na kijiji kizima.
Kauli hiyo imetolewa baada yakuwepo tabia ya baadhi ya wananchi kufikiwa na wageni bila kutoa taarifa kwa balozi wa nyumba kumi au kwa mwenyekiti wa kitongoji.
Alisema kuwa ili kuhakikishakitongoji kinakuwepo na ulinzi na usalama lazima wageni wanapofika kitongojini kuwe na utaratibu wa kuwaandikisha wageni wa muda kwenye kitabu cha wageni cha kitongoji.
“Mgeni anafaida na hasara, mgeni mwingine anakuwa na nia njema na mwingine anaweza kuwa mhalifu kwa kuja kuchunguza mazingira ya kuiba kwa shirikiana na wenyeji,”alisema mwenyekiti.
Alisema kuwa kitabu cha wageni wanaofika kwa muda kipo kitongojini ni lazima wananchi watoe taarifa ya wageni wao ili kujua wageni wa ngapi wanaingia na kutoka.
Alisisitiza kuwa mtu yeyote anapofikiwa na mgeni ni lazima atoa taarifa kwa uongozi husika kwa kumsainisha kitabu cha wageni wa muda ilikujua mgeni amekuja kwa lengo gani.
“Kuna mambo mawili hapa unaweza kumpokea mgeni kisirisiri anaweza kuwa ni mgeni wa hasara au anaweza kufa ghafla nyumbani kwako utafanyaje? Kumbe ungelitoa taarifa inakuwa rahisi kwako,” alitoa angalizo.
Kwa upande wa mazingira, aliwaasa wananchi kuwa na tabia yakufanya usafi katika mazingira yao, kujenga vyoo bora, kuchimba shimo la taka pamoja na kuaacha tabia yakujisaidia porini  kuepuka magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu.
“Sisi tupo mlimani na wenzetu wapo bondeni, tunapojisaidia porini uchafu wote unateremka chini na kuchafua maji ya kunywa kwenye visima vya wenzetu kwa hiyo lazima tujenge vyoo bora na bafu ili kupunguza uchafuzi wa mazingira,” alisema Mhagama.
Aidha, Kitongoji cha Mlimani ni mmoja vitongoji saba vilivyopo katika Kijiji cha Peramiho ‘B’ katika Kata ya Peramiho, vitongoji vingine ni pamoja na Lipinyapinya, Namatanda, Mchangani, Madukani, Sekondari na Lihangano.
Kitongoji hicho kina wakazi zaidi 320 kwa taarifa iliyotolewa mkutanoni na Mwenyekiti wa Kitongoji, Bonventura Mhagama.
Katika hali isiyo ya kawaida mjumbe mmoja Sidomino Kita Gama alimaarufu Sido,’ pia balozi wa nyumba kumi (ten cell leader) ambaye  alinyosha mkono wakati wa  mkutano  kutaka kujua kwa nini taarifa ya mapato na matumizi ya kitongoji hicho hayajasomwa kwa miaka minne?
Kwa upande wake mwenyekiti huyo alikiri kutoitisha mikutano pamoja na kutowasomea wananchi mapato na matumizi kwa muda mrefu kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake na kuahidi kuitisha mkutano mwingine wakuwasomea mapato na matumizi mwezi wanne (Aprili 2014). 
Mwenyekiti huyo pamoja na mambo mengine aliwaomba radhi wajumbe wa mkutano kwa kupiga magoti mbele mkutano na  wajumbe wakamsamehe.
“Sababu mojawapo iliyosababisha kutoitisha mikutano ni pamoja shughuli za kilimo na wananchi wengi kutofika mikutanoni pindi inapoitishwa na wakati mwingine mkutano wanapoitishwa kamati mbalimbali huwazinakosekana kwa ajili ya kutoa taarifa husika,” alifafanua mwenyekiti.
“Kutokana na sababu ya wananchi wengi kutofika mkutanoni au kuchalewa kufika katika mikutano, tutajiwekea kanuni ya kuwatoza faini wajumbe wanaoshindwa kufika mkutanoni bila taarifa au kwa kuchelewa kufika mkutanoni kwa muda uliopangwa, watalipa faini kati ya shilingi mia tano na elfu moja,”aliongeza.
Wakati huohuo, Kitongoji cha Mlimani kimeunda mabaraza mawili ya wazee na vijana pamoja na kuunda vikundi mbalimbali ya vijana ili kuwaunganisha katika taasisi ya mikopo kuwawezesha kuendesha  biashara na kilimo na hatimaye  kuwa kwamua katika lindi ya umasikini.
Katika baraza huru la wazee walichaguliwa viongozi wakuliongoza baraza hilo, ambapo Nestory Mbena alichaguliwa kuwa mwenyekiti, Ester Haule alichaguliwa kushika nafasi ya katibu na mhasibu alichaguliwa Ponsiano Gama.
Kwa upande wa baraza la vijana, Sofia Ngonyani alichaguliwa kuwa mwenyekiti  na katibu wake alikuwa ni Malta Ndunguru.
“Serikali haiwezi kusaidia mtu mmojammoja, lakini tunapojiunga katika vikundi mbalimbali na kuvisajili, kutengeza katiba na kufungua akaunti benki ni rahisi serikali kutusaidia kwa kupitishia pesa kwenye akaunti hizo,” alielezea mwenyekiti.
Mwisho


WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...