Na Friday Simbaya, Ludewa
WAKATI Taifa likishehekea mafanikio ya kuudhibiti ugonjwa hatari wa Maralia kwa kugawa vyandarua kwa mama wajawazito na watoto walio na umri chini ya miaka mitano Mkoani Iringa bado vyandarua havitoshi, lakini vilivyopo vinatumika kujifunika kama blanketi kujikinga na baridi imefahamika.
Hayo yalithibitika hivi karibuni katika kijiji cha Mbwila Kata ya Luana Ludewa Mkoani Iringa wakati wa maadhimisho ya siku ya malaria kimkoa ambapo mkuu wa wilaya ya Ludewa Bi Georgina Bundalla alimwakilisha Mkuu wa Mkoa huo kama mgeni rasmi.
Desmola Salo (37) aliliambia gazeti hili kuwa vyandarua vinavyotolewa na serikali havitoshi. “” mimi mwenyewe pale nyumbani ninayo familia ya watoto watano, lakini tunacho chandarua kimoja tu ambacho tunakitumia mimi na mume wangu huku watoto wakilala bila chandarua.”” Alilalamika Bi Desmola
Kwa upande wake Bi Evelina Haule (65) na Pendo Kayombo wao walikiri kupokea vyandarua vyenye dawa kutoka kwa mawakala wa mabadiliko katika jamii lakini wao wakaweka bayana kuwa wanatumia vyandarua hivyo kwa kujifunika nje ya shuka kama blanketi kwa kuwa hawajui matumizi vyandarua hivyo.
Bi Georgina Bundalla Mkuu wa Wilaya ya Ludewa aliwataka wananchi kuacha mara moja tabia ya kuamini na kuhusisha ushirikina na ugonjwa wa malaria kwa sababu wanapoteza muda na nguvu nyingi kwa waganga wa kienyeji wakati dalili za malaria ziko wazi ni vema kwenda Hospitalini kupima kwanza kuliko kukimbilia ushirikina. Aliongeza Bundala
“Tunasema malaria haikubaliki kwa sababu inawezekana kuidhibitiwa. Kwa nini ukubali kitu ambacho kinakuletea madhara. Malaria kwanza ina tabia ya kupunguza damu, wengi wetu tuna tabia ya kuchelewa kwenda hospitali na kuwahi kwa mganga wa jadi ambako tunachanjwa na kupunguzwa damu tabia hiyo ife,” alikemea
Meneja wa PSI Kileo Optatus alimwambia mgeni rasmi kuwa malaria ni ugonjwa hatari ambao unaongoza duniani kila baada ya dakika tano hufariki dunia ambapo katika bara la Afrika hasa nchi zilizo chini ya jangwa la Sahara na kuongeza kuwa Tanzania ni nchi ya katika Afrika kwa vifo vinavyotokana na malaria.
“wananchi wa Mbwila na Ludewa kwa ujumla tukishikiana na wadau wengine mbalimbali kwa kuzingatia kanuni zinazotolewa na wizara ya Afya kwa kutumia vyandarua vyenye dawa kila siku kwa mwaka mzima tutafanikiwa kuutokomeza ugonjwa huu wa malaria.”” Alisisitiza Bw Kileo
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Bw Happines Ndosi alimwambia mgeni rasmi kuwa ugonjwa huu ni hatari hasa katika makundi maalumu kama wajawazito na watoto waliopo chini ya miaka mitano na kwa Kitaifa maadhimisho haya yalifanyika mkoani Arusha kimkoa maadhisho haya yalifanyika wilayani Ludewa na kiwilaya yalifanyika kijiji cha Mbwila.
Mratibu wa malaria mkoa wa Iringa Bi Linda Chatila akitoa takwimu za ugonjwa wa malaria ailimwambia mgeni rasmi kuwa ugomjwa wa malaria unaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa nje yaani (OPD) na wale wanaolazwa katika mkoa.
Bi Linda alisema mwaka 2009 malaria iliongoza wagonjwa wa nje chini ya miaka mitano walikuwa asilimia 34.8 ya wagonjwa wote wa umri huo, pia kati ya wagonjwa wote waliolazwa umri chini ya miaka mitano malaria isiyokali iliongoza kwa asilimia 36.6 ya wagonjwa wote waliolazwa katika umri huu. Aidha ugonjwa wa malaria kali uliongoza kwa vifo kwa asilimia 19.5 ya vifo vyote vilivyotokea katika wagonjwa wa kulazwa wenye umri chi ya miaka mitano.
Alisema kwa wagonjwa wa nje wenye umri wa zaidi ya miaka mitano ugonjwa wa malaria ulichukua nafasi ya kwanza sawa na asilimia 24.8 ya wagonjwa wote wa umri huu takwimu hizi zinaonesha kuwa tatizo la malaria bado linaongezeka ingawa jitihada mbalimbali zimefanywa ili kudhibiti tatizo hili.
Wadau wengine wanao jishughulisha na mapambano dhidi ya malaria katika Nyanja mbalimbali mkoani wa Iringa ni pamoja na PSI (T), Chama cha Msalaba mwekundu, Meda, Tagurode, na maajenti wa kuleta mabadiliko katika jamii ambao shughuli zao ni pamoja na kusambaza vyandarua.
Friday, 6 May 2011
ASASI NYINGI NCHINI ZIMO HATARINI KUFA
MASHIRIKA yasiyokuwa ya kiserikali (NGOs) yamo hatarini kufunga milango ya ofisi zao kutokana na viongozi wengi wa mashirika hayo kukosa kabisa utaalamu wa kuandika miradi mbalimbali kwa ajili ya huduma za kijamii na badala yake yanasubiri wafadhili wenyewe wajitokeze jambo ambalo ni gumu sana kwa wafadhili kufanya hivyo imefahamika.
Hayo yalijitokeza jana katika semina ya siku tano ya kuwajengea uwezo viongozi wa mashirika hayo yasiyo ya kiserikali wilayani Ludewa iliyofanyika katika ukumbi wa MTC Mlangali na kuandaliwa na Ludewa Non Governmental Umbrella (LUNGOU) chini ya ufadhili wa The Foundation for civil society ya jijini Dar es salaam.
Pamoja na kuyajengea uwezo mashirika hayo juu ya uandaaji na uandishi wa miradi ya kijamii LUNGOU pia ili iliendesha semina ya ufahamu juu ya utawala bora ndani ya mashirika hayo na katika watumishi na wafanyakazi na watendaji ndani ya serikali na vyombo vya umma.
Akifungua semina hiyo Afisa maendeleo ya jamii wilayani Ludewa Bw. William Malima aliwataka viongozi hao wa mashirika yasiyo ya kiserikali kuacha tabia ya kusubiri wafadhiri waje kuwatafuta badala yake wayatumie mafunzo hayo kuwajengea uwezo wa kuandaa na kuandika wenyewe miradi ili kuwashawishi wafadhili kutoa fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali.
Bw. Malima alisema asasi nyingi za kiraia nchini zinakosa pesa kutokana na kutofahamu namna ya kundika maandiko ya miradi (project write up)hata zile chache zinazopata fedha bado zinakabiliwa na tatizo la utawala bora. Utawala bora ni pamoja na jinsi asasi inavyoendeshwa shughuli zake kwa njia ya vikao hasa kwa kukosa uwazi (Transparency) na uwajibikaji yaani (Accountability).
“Ndugu washiriki wa semina kuna umuhimu mkubwa wa kuandika miradi/maandiko ambayo malengo yake ni pamoja na kupata raslimali fedha, rasrimali mitambo (mashine) na vitendea kazi, rasriamali watu wenye ujuzi kama wataalamu ambao leo watatoa mafunzo namna ya kutayarisha na kushawishi wafadhili,”alisema Bw Malima.
Aidha, mgeni rasmi alisema asasi nyingi hushindwa kuandika miradi kwa kutojua ni miradi gani waandike, wakati gani na wapi wapeleke lakini wanasahau kuwa kwa sasa dunia inakabiliwa na matatizo kama ugonjwa wa Ukimwi, Umaskini uliokithiri hasa wa kipato, Uharibifu wa mazingira,Ukosefu wa utawala bora na Ukiukwaji wa haki za binadamu n.k.
Bw. Malima aliwataka washiriki na wadau wengine kwenda kuwaelimisha na kuhamasisha jamii, taasisi na vikundi viweze kuanzisha na kusajili asasi kwani katika Wilaya nzima ya Ludewa kuna asasi 38 tu zilizo hai wakati Tanzania yote hadi 2010 kulikuwa na asasi 6,000 idadi ambayo ni ndogo sana ukilinganisha na nchi ya Ufaransa yenye asasi 80,000 hadi sasa.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi Bw. Emanuel Kayombo mwenyekiti wa mwavuli wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali wilayani Ludewa aliwataka washiriki wa semina kushiriki vikamilifu mafunzo hayo kwani ndiyo ukombozi na uhai wa mashirika yao ama sivyo mashirika hayo yamohatarini kufutiwa usajili.
Bw. Kayombo aliwataka wanachama hao wa mtandao (LUNGOU) kutoa viingilio na michango yao ya kila mwaka ili kuweza kupata fedha za kuendeshea ofisi, na kuwataka viongozi ambao hawajasajili asasi zao kwa mwavuli wa mashirika ili kujua shughuli wanazofanya nia ikiwa ni kuepusha migongano ya kuandika miradi inayofanana kwa wafadhili na huduma zinazofanana.
Mkufunzi wa mafunzo hayo na mtaalam wa maandiko Bw Elwin Mligo kutoka Njombe aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa makini katika kuandika miradi hasa kutokuchanganya Dira ya shirika, Dhima na Maadili sanjari na kuzingatia mfumo wa mti wa matatizo, mti wa malengo, bo la mantiki na Bajeti bila kusahau visababishi,matatizo na madhara.
Mafunzo yaliyotolewa katika semina hiyo ni pamoja na upangaji na usimamizi wa miradi, uchambuzi wa ndani na nje ya azaki, uchambuzi wa wadau na tathmini ya mahitaji, utayarishaji wa malengo yenye kuzingatia matokeo, kupanga bajeti ya mradi uchambuzi na umuhimu wake, tathmini na ufuatiliaji,viashiria na utawala bora.
Hata hivyo, washiriki wa mafunzo hayo waliomba shirika la The Foundation For Civil society lilifadhili mafunzo hayo kuongeza ufadhili mwingine kwenye mwavuli wao ili kuweza kukamilisha mafunzo hayo kwani muda uliotumika hautishi kumaliza masomo yote jambo lililofanya kukatisha kutokana na ufinyu wa bajeti yenyewe.
MEI MOSI WAFANYAKAZI LUDEWA WAKERWA NA KIBURI NA KEJELI...
.Waajiri na Wakuu wa idara wakwepa kujitokeza kwenye sherehe hizo.
MAADHIMISHO ya sherehe za mei mosi yanayofanyika kila mwaka duniani kote yamewachefua wafanyakazi nchini hususani Wilayani Ludewa kutokana na viongozi na baadhi ya wakuu wa idara kupuuza na kuchelewesha maslahi na stahili za wafanyakazi wa kada za chini.
Akisoma risala kwa niaba ya wafanyakazi wote mwenyekiti wa shirikisho la vyama huru vya wafanyakazi Wilayani Ludewa Mkoani Njombe Bw Joseph Thomas Mvanga alisema waajili wanakatisha tamaa wafanyakazi wao na kusababisha kufanyakazi chini ya kiwango.
Bw Mvanga alizitaja kero hizo kuwa ni pamoja na kuchelewesha mishahara yao ya kila mwezi, kutopandishwa vyeo kwa wakati, mazingira mabaya ya kufanyia kazi, viongozi na waajili kutoa lugha chafu na kejeli kwa wafanyakazi wa kada ya chini, wastaafu kucheleweshewa mafao yao kunapelekea wastaafu waatarajiwa kukata tama na kuingiwa na hofu kila wanapokaribia kustaafu hasa wanapoona mateso wanayopata waliotangulia.
Naye mwenyekiti wa chama cha walimu (CWT) Wilaya ya Ludewa mwalimu William Kunyanja Akimkarisha mgeni rasmi Bw John Mahali ambaye ni katibu tawala wilaya ya Ludewa alisema kero za wafanyakazi zitatuliwe kwa ushirikiano ili kuondoa wasiwasi na kujenga uaminifu baina ya mwajiri na mwajiriwa.
“Inasikitisha sana kuona kila mwaka mei mosi wafanyakazi wanawasilisha kero na malalamiko yao lakini serikali imeziba masikio kama vile haisikii hii inaondoa maana ya maadhimisho haya kwa sababu matatizo kila mwaka tunatoa kero lakini hazitekelezwi”” alilalamika Bw Kunyanja
Alimwambia mgeni rasmi kuwa kupuuzia kunakofanywa na waajili kunaongeza msongo wa mawazo na mheuko kwa watumishi wenye uhitaji wa huduma kutoka kwa viongozi wao na kuitaka serikali kuchukua hatua na kushughulikia kero kwa wakati bila mizengwe na kwamba kwa kufanya hivyo rushwa na uzembe kazini vitakwisha.
Akijibu risala hiyo ya watumishi Bw John Mahali katibu tawala wa wilaya ya Ludewa (DAS)ambaye alimwakilisha Mkuu wa wilaya hiyo aliyekwenda kuhudhria maadhimisho ya mei iliyofanyika kimkoa wilayani mfindi alikiri kuzitambua kero hizo na kusema kuwa zinahitaji ushirikiano katika kuzitatua.
Hata hivyo aliahidi kuzishughulikia kero hizo lakini akawaambia waajili na wakuu wa idara wachache waliohudhuria sherehe hiyo kuwa mei mosi ijayo wawe wamezishughulikia kero hizo. Na kwamba siyo busara kila mwaka wafanyakazi kulalamikia mambo yaleyale.
Hata hivyo Bw Mahali alisikitishwa na tabia mbaya iliyooneshwa na wakuu wa idara katika Halmashauri hiyo na waajili kwa kutohudhuria na kutoshiriki vyema katika viwanja yalipofanyika maadhimisho ya sherehe hizo za mei mosi zilizofanyika kiwilaya katika kata ya Ludewa.
“Katika sherehe kama hizi inatakiwa wakuu wa idara na waajili wawepo wenyewe hapa na kusikiliza kero za watumishi waliochini yao kwa sababu yapo mambo yanayowahusu wao na matatizo mengi yapo chini ya uwezo wao kwa sababu wao ndio wanaoshinda na watumishi hao.” Alisema Bw Mahali
Hata hivyo aliwaagiza waandaaji wa maadhimisho hayo kuwashirikisha waajili wengine wa kutoka katika sekta binafsi kwa sababu mfanyakazi siyo wa serikalini tu na kwamba siyo vizuri kuwatenga watu binafsi na kuwataka waajili kuacha tabia ya kusema njoo kesho hiyo hali imepitwa na wakati.
WASOMALI 87 KIZIMBANI KWA KUINGIA NCHINI BILA KIBALI
WAKIMBIZI 87 wa kabila la wahadia kutoka nchini Ethiopia wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi wilayani Ludewa kwa kosa la kuingia nchini kwa makusudi bila ya kibali chochote huku wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Waethiopia hao ambao idadi yao kubwa ni wakristo na muislamu mmoja walikamatwa huko mwambao wa ziwa Nyasa katika kijiji cha Ngelenge Manda wakiwa wanajaribu kuvuka ziwa kwenda nchi jirani ya Malawi ambako wanakwenda kuomba hifadhi kutokana na kukimbia machafuko ya kisiasa nchini kwao.
Akisoma mashtaka mbele ya Hakimu mkazi wa mahakama ya Wilaya ya Ludewa Emanuel Mwambeta (DM) mwendesha mashtaka mratibu msaidizi wa polisi ambaye ni Mkuu wa upelelezi wilaya ya Ludewa ASP Thomas Mtikatika aliiambia mahakama hiyo kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo April 13 mwaka majira ya tano asubuhi huko Ngelenge Manda mwambao wa ziwa Nyasa.
Bw Mtikatika aliendelea kuiambia mahakama hiyo kuwa wakimbizi hao wamevunja sheria chini ya kifungu na 31 (1) (i) sheria namba 7 ya uhamiaji ya mwaka 1995 na kwamba kama watapatikana na hatia sheria itazingatiwa ikiwa ni pamoja na kurejeshwa nchini kwao.
Naye Bw Ali Abeid ambaye yuko kitengo cha sheria doria na uchunguzi katika idara ya uhamiaji wilayani Njombe aliongeza kuwa kwa mujibu wa sheria wanaweza kuhukumiwa chini ya kifungu na 31 au kwa mamlaka ya waziri anaweza kutumia kifungu na 14 kinampa mamlaka waziri kumrudisha mhamiaji haramu alikotoka.
Wao dhamira yao ni kwenda Afrika kusini kupitia Malawi na kwamba vipenyo vya kwenda nchi za kusini viko vitatu ambavyo ni Wilaya ya Kyela, Ludewa mkoa wa Iringa na Mbambabay mkoani Ruvuma maeneo hayo ndiyo yanayo sumbua. Hata hivyo washtakiwa wote walikiri kosa na sasa wanasubiri kurudishwa nchini kwao.
Alisema mikakati iliyopo ni kuzima mtandao wa mawakala wanaojihusisha na biashara hiyo ya kuwasafirisha wakimbizi hao haramu kwa manufaa binafsi, kesi hiyo imesikilizwa tena Mei 2 mwaka huu kwa kutekeleza amri kuridishwa kwao kwa mujibu wa mamlaka ya waziri wa mambo ya ndani ya nchi.
“”Awali wahamiaji haramu idadi yao ilikuwa 88, lakini mmoja alifariki dunia April 9 mwaka huu katika kundi la kwanza kutokana na kuugua malaria, kaharisha na kubadili hali ya hewa.”” Alisema Bw Alli
Katika kesi nyingine kijana Jackson Luoga (15) amehukumiwa kifungo kwenda jela mia miwili kwa kosa la kuiba kuku wenye thamani ya shilingi 45,000.
Subscribe to:
Posts (Atom)
WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...
Na Friday Simbaya, Mufindi Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...
-
KIKUNDI cha Upendo ni kikundi cha kina mama 20 walioamua kujiunga kwa pamoja na kuanz...
-
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini MIEMBE hulimwa karibu katika nchi zote zilizoko kwenye ukanda wa joto, na hasa tropiki. Nchini ...
-
The most deadly form of tuberculosis is one that lies in wait inside the body for years, attacking at the first sign of weakness. Abou...