Katika kufikia malengo ya mradi wa ‘Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili, unaotekelezwa mkoani Iringa; Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) imeanza mchakato wa kuziwezesha serikali za vijiji kuandaa sheria ndogo zitakazo waongoza katika usimamizi wa maliasili na mazingira.
Sheria hizo zitasaidia kupunguza uharibifu wa rasilimali misitu na wanyamapori ambazo zipo katika hatari ya kutoweka kutokana na uvunaji haramu.
Kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi katika wilaya za Iringa na Mufindi, mkoani Iringa; LEAT ilifanya utafiti juu ya kiwango cha ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili, pamoja na mambo mengine katika utafiti huo LEAT ilibaini kuwa baadhi ya vijiji havikuwa na sheria ndogo ambazo zingetumika kusimamia maliasili na mazingira. Kutokana na hali hiyo LEAT imeanza mchakato wa kuziwezesha serikali za vijiji kuandaa sheria hizo.
Vijiji vitakavyo wezeshwa katika awamu ya kwanza ni vijiji vya Mbweleli, Kinyika na Kinyali kwa wilaya ya Iringa. Vijiji hivi hakiwahi kuwa na sheria ndogo ambazo zingetumika kusimamia maliasili licha ya kuwa na misitu ya asili ya vijiji. LEAT iliziongoza serikali za vijiji na wananchi katika kuunda sheria ndogo za usimamizi wa maliasili.
Wananchi na viongozi wa serikali za vijiji walitoa mapendekezo ya muundo wa sheria hizo, na wote kwa pamoja walikubaliana kuwa LEAT ichapishe sheria hizo na zimepangwa kuwasilishwa kuanzia mwezi Julai, 2016 kwenye mikutano mikuu ya vijiji, ili wananchi wengi wapate fursa ya kuzijadili na kuzipitisha.
Kwa wilaya ya Mufindi, vijiji vitakavyo fikiwa katika awamu ya kwanza ni Kibada, Ludilo na Ikangamwani. Vijiji hivi vina na sheria ndogo zinazo waongoza katika usimamizi wa maliasili, lakini sheria hizo zilikuwa na mapungufu.
LEAT, serikali za vijiji pamoja na wananchi walipitia sheria hizo na waligundua mapungufu. Wananchi na viongozi wa serikali walioshiriki katika mchakato huo walitoa mapendekezo ya maboresho ya sheria.
Sheria hizo zitawasilishwa katika mikutano mikuu ya vijiji kuanzia mwezi Julai, 2016 ili wananchi wengi wapate fursa ya kuzijadili, kuzifahamu na kuzipitisha.
Malengo ya mradi wa ‘Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili, ni kujenga utamaduni wa wananchi kushiriki katika usimamizi wa maliasili, kuzijengea uwezo jamii za wenyeji katika kuziwajibisha na kuzisimamia taasisi za serikali zenye majukumu ya kuhifadhi na kusimamia maliasili. Mradi pia umelenga kukuza ufanisi katika utekelezaji na usimamizi wa sera na sheria muhimu zinazo husika katika usimamizi wa maliasili, mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi.
Kwa kuwa rasilimali zilizolengwa zinapatikana vijijini, LEAT iliona vyema kuwa lazima vijiji hivyo viwe na sheria ndogo zitakazo waongoza katika kusimamia kikamilifu maliasili zilizopo katika maeneo yao.
LEAT imekwisha toa mafunzo ya usimamizi wa maliasili kwa wananchi, kamati za maliasili, mazingira, ardhi, maendeleo ya jamii na fedha. Viongozi wa serikali za vijiji, Madiwani na Maafisa maliasili na ardhi, nao wamepatiwa mafunzo hayo. Makundi hayo yote yamejifunza sera na sheria zinazotumika katika usimamizi wa maliasili.
Pia wamejifunza majukumu ya taasisi na idara za serikali zinazohusika katika usimamizi wa maliasili. Zaidi makundi hayo yalijifunza mfumo wa Ufuatiliaji Uwajibikaji Jamii, ilikuongeza ufanisi na utawala bora katika kutoa huduma za jamii.
Mradi wa ‘Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili’ unatekelezwa na LEAT katika vijiji 32 vya wilaya za Iringa na Mufindi, mkoani Iringa. Mradi umefadhiliwa na Watu wa Marekani kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID).