MGOMBEA nafasi ya Uenyekiti katika Klabu ya soka ya Lipuli Fc 'Wanapaluhengo, Abinery Mrema (kushoto) amewaahidi wanachama na wapenzi wa soka mkoani hapa atahakikisha timu hiyo inamiliki uwanja wa mazoezi endapo atachaguliwa.
Wagombea wengine ni Ramadhani Mahani na Nuhu Muyinga.
Akizungumza na wanahabari SIMBAYABLOG leo, Mrema alisema kuwa timu ya Lipuli ambayo kwa sasa iko ligi kuu Tanzania Bara haina budi kuondokana na viwanja vya kuazima kwa ajili ya kufanyia mazoezi hivyo atahakikisha timu hiyo inapata uwanja wake.
Alisema kuwa licha ya kuwa uwanja wa mazoezi atahakikisha inawekeza katika vitega uchumi ambavyo ni kuwa na kiwanja kwa ajili ya uwekezaji, kuwa na chuo cha mafunzo kwa watoto, na kuhakikisha timu hiyo inapata usafiri wa uhakika.
Aliongeza kuwa atahakikisha wanafungua matawi ya timu ya Lipuli nchi nzima na nje ya nchi ambapo watachangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa timu ya Lipuli .
"Nitahakikisha timu ya Lipuli inakuwa na matawi mengi ndani na nje ya nchi na nitahakikisha nawashawishi wadau wakubwa wa ndani na nje kuweza kuisaidia timu yetu ili iweze kufanya vizuri katika ligi" alisema
Mrema alisema kuwa endapo wanachama watampatia ridhaa ya kuongoza timu ya Lipuli Fc atahakikisha wanafanya mikutano ya mara kwa mara na wadau kuwaelezea maendeleo ya timu na changamoto zake kwa lengo la kupata ufumbuzi.
Aliongeza kuwa atahakikisha Lipuli inafaidika na nembo ya timu katika kwa kuingia mikataba yenye maslahi kwa timu hasa katika uuzwaji wa vifaa vya timu kama Jezi.
Uchaguzi wa nafasi mbalimbali za uongozi wa timu ya Lipuli unatarajiwa kufanyika Julai 23 mwaka kwa nafasi za Uenyekiti, Makamu na ujumbe wa kamati.