Habari ndugu msomaji wetu wa blog, Natumaini unaendelea vyema. Leo tutaanza kujifunza kilimo cha bora cha nyanya, na tutaanza kufahamu vitu vya msingi kwanza, na natumaini ukimaliza mfululizo wa makala hizi utakua mkulima hodari wa nyanya. Kila kitu lazima kiwe na msingi imara, karibu tujifunze wote:
Utangulizi:
Nyanya ni zao la mboga ambalo hulimwa sehemu nyingi duniani kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na pia kama zao la biashara. Inahisiwa kuwa asili ya nyanya ni nchi ya Peru/Equador huko Amerika ya Kusini. Mmea huu ulianza kuzalishwa kama zao katika nchi ya Mexico na baadaye kusambaa katika nchi nyingine za ulimwengu.
Uzalishaji wa nyanya duniani na hapa Tanzania
Nchi zinazolima nyanya kwa wingi duniani ni pamoja na USA, Italia na Mexico. Kwa upande wa Africa nchi zinazo lima ni kama; Malawi, Zambia na Botswana.
Zao hili hulimwa pia katika nchi za Africa Mashariki, ikiwemo Kenya, uganda na Tanzania.
Zao la nyanya linalimwa karibu maeneo yote ya Tanzania. Uzalishaji wa nyanya ni mkubwa kuliko mazao mengine ya mbogamboga yanayolimwa hapa Tanzania, uzalishaji wa nyanya kwa mwaka ni jumla ya tani 129,578 ikiwakilisha asalimia 51 ya mazao yote ya mboga. Kwa mujibu wa Wizara ya kilimo ya Tanzania maeneo yanalolima sana nyanya ni pamoja na Mkoa wa Kilimanjaro (Hai, Moshi na Rombo), Arusha (Arumeru), Morogoro (Mgeta), Tanga (Lushoto), Mbeya (Mbeya vijijini) na Singida. Morogoro ndiyo inayoongoza kwa kilimo hichi ikiwa na wazalishaji wenye zaidi ya hekta 6,159 (ekari 15,398). Pamoja na kwamba eneo la uzalishaji linaongezeka kwenye maeneo mengi lakini uzalishaji wa nyanya bado ni mdogo sana.
Uzalishaji mdogo unasababishwa na kupungua kwa rutuba ya ardhi, upepo, joto, ukame. Sababu nyingine ni pamoja na ukosefu wa aina za nyanya zenye mavuno mengi amabazo zinahimili mazingira ya kwetu, wadudu, magonjwa na magugu.
Mazingira
Hali ya Hewa:
Nyanya hustawi vizuri zaidi kwenye mazingira ya joto la wastani kuanzia nyuzi joto 18-27 sentigreti. Mvua nyingi husababisha mlipuko wa magonjwa ya ukungu kama vile Baka jani chelewa n.k.)
Udongo:
Nyanya hustawi kwenye aina zote za udongo kuanzia udongo wa kichanga, mweupe wa tifutifu hadi udongo wa mfinyanzi, ili mradi uwe na mboji ya kutosha na usiosimamisha/tuamisha maji. Pia uwe na uchachu wa wastani yaani pH 6.0 - 7.0.
Aina za Nyanya
Kotokana na uchavushaji, nyanya zinagawanyika makundi mawaili:
1. OPV (Open Pollinated Variety) - Aina za kawaida. Mfano Tanya, Mwanga, Onyx n.k
2. Hybrid – Chotara: Hizi ni aina zenye mavuno, mengi, zilizoboreshwa zaidi. kati ya hizo zipo aina fupi,za kati na ndefu. Mfano Victory F1, Anna F1, Kipato F1, Monica F1, Kilele F1 n.k
Kutokana na tabia ya ukuaji, nyanya zinagawanyika katika makundi matatu:
1. Aina fupi (determinate) kwa mfano Tanya, Cal J, Mwanga, Onyx, Roma VF n.k. Hizi huweza kuvunwa mara 2 hadi 3.
2. Saizi ya Kati. – Hizi ni zile nyanya ndefu kaisi (sio ndefu sana), kitaalamu zinaitwa semi determinate varieties. Mfano wa nyanya aina hii ni Kipato F1. Aina hizi unaweza kuvuna mivuno 3 hadi 5
3. Aina ndefu ( intermediate) kwa mfano ANNA F1, Victory F1, Tebgeru 97. Aina hizi hufanya vizuri zaidi zinapopandwa ndani ya greenhouse. Uvunaji wake ni wa muda mrefu, kuanzia mivuno 5 na kuendelea, zipo ambazo zinavunwa hata zaidi ya miezi 6, yaani hiyo miezi 6 ni ya uvunaji tu.
Katika karne hii ya 21, nyanya zinazopendelewa kulimwa zaidi na wakulima, ni zile zinazoweza kuvumilia magonjwa, zinazo zaa sana, na zenye ganda gumu ili kufanikisha usafirishaji, na kuhifadhika kwa siku nyingi bila kuharibika mapema.
Kuandaa Kitalu cha Nyanya
Mambo muhimu ya kuzingatia:
• Kitalu kiwe karibu na maji ya kutosha na ya kudumu
• Kiwe sehemu iliyowazi na yenye udongo ulio na rutuba ya kutosha
• Eneo la kitalu kama ni kubwa liwe tambarare au na mwiinuko kidogo ili kuepuka maji yasituame kwenye kitalu, mtelemko ukiwa mkali sana nao sio mzuri kwani husababisha mmomonyoko wa udongo.
• Kitalu kiwe sehemu ambayo haikuwa na zao la nyanya au viazi mviringo (au mazao ya jamii ya nyanya k.m. mnavu, biringanya n.k.)
• Kiwe sehemu ambayo ni rahisi kupata huduma zote muhimu kwa urahisi, ikiwa ni pamoja na uhamishaji wa miche kwenda sehemu nyingine. Pia kurahisisha usambazaji wa miche kwenda sehemu nyingine.
Kuandaa Matuta ya Kusia Mbegu za Nyanya
Aina ya matuta:
– matuta ya makingo (sunken seed bed)
– matuta ya kunyanyulia udongo (raised seed bed)
– matuta ya kawaida (flat seed beds)
Mambo Muhimu ya Kuzingatia wakati wa Kuandaa Matuta
• Tuta liwe na upana kati ya sentimita 90-120, na urefu wowote, [ili mradi muhudumu anaweza kutoa huduma nyingine zote kitaluni bila kukanyaga miche].
• Kwatua/lima kina kirefu cha kutosha kiasi cha sentimita 15-20 ili mizizi iweze kusambaa vizuri ardhini.
• Choma takataka juu ya kitalu, au funika tuta kwa nailoni, majuma 4-8 ili kuua vimelea vya magonjwa na wadudu.
• Wakati wa kuandaa, kitalu, ongeza mbolea aina ya samadi/vunde au mboji kwenye udongo kisha kwatua ili ichanganyike vizuri na udongo.
• Changanya kiasi cha debe 1 hadi 2 kila baada ya mita moja (hatua moja) mraba.
• Tuta lisiwe na mabonde mabonde au mawe mawe ambayo yanaweza kuzuia usambaaji mzuri wa mbegu kwenye tuta, lisawazishwe vizuri ili kuhakikisha usambazaji mzuri wa mbegu na kuepuka mbegu kufukiwa chini mno kiasi ambacho hazitaota.
Faida na Hasara za Matuta yaliyotajwa hapo juu
1. Matuta ya kunyanyulia udongo (raised seed beds);
Faida:
– matuta ya namna hii huruhusu maji, hewa na mizizi kupenya kwenye udongo kwa urahisi zaidi.
– Mazao ya mizizi hupata nafasi ya kutosha kutanuka haraka zaidi
– Matuta haya hayatuamishi maji kama mengine, hivyo hutumika zaidi kwenye maeneo yanayokuwa na mvua mara kwa mara.
Hasara:
- Matuta ya namna hii yana sababisha sana mmomonyoko wa udongo kama hayakutengenezwa vizuri.
2. Matuta ya makingo (sunken seed beds):
Faida:
· matuta haya ni rahisi kutengeneza
· hutumika wakati wa kiangazi ili kuhifadhi maji na unyevu
· nyevu mdogo unaopatikana ardhini
· ni rahisi kumwagilia kwa kutumia maji ya mfereji au bomba
· huhifadhi unyevu nyevu kwenye ardhi kwa muda mrefu
· huzuia mmomonyoka wa ardhi
Hasara:
· Matuta ya aina hii hayawezi kutumika kwenye maeneo yenye mvua nyingi.
3. Matuta ya kawaida (flat seed beds):
Faida:
· ni rahisi sana kutengeneza kwani udongo ukisha kwatuliwa
· na kusambazwa mbegu huoteshwa
· ni rahisi kutumia eneo kubwa kuotesha mbegu
Hasara:
Matuta ya aina hii hayawezi kutumika kwenye maeneo yenye mvua nyingi.
Kusia Mbegu
• Hakikisha ubora na uotaji wa mbegu kabla ya kuzipanda kitaluni (germination test)
• Weka mistari kwenye tuta kulingana na ukubwa wa tuta, lakini mistari isiwe chini au zaidi ya sentimita 15-20 toka mstari hadi mstari
• Kina cha mistari kisiwe cha kutisha bali kiwe kati ya sentimita 1-2
• Matuta yapate maji ya kutosha siku moja kabla ya kusia mbegu. Ni vizuri kutumia chombo cha kumwagilia (watering can).
• Mbegu ziatikwe kwenye mistari na zisambazwe vizuri ili kufanikisha usambaaji mzuri wa mbegu kwenye tuta. Changanya mchanga laini na mbegu kisha sambaza kwenye mistari iliyoandaliwa kwenye tuta.
Mbegu zinaweza pia kuatikwa kwenye tuta bila mistari, lakini zisambazwe kwa uwiano mzuri kwenye tuta ili kupunguza msongamano. Msongamano husabisha magonjwa ya fangasi kama vile kinyausi (damping off) au ukungu (blight).
• Weka matandazo kiasi cha kutosha ambacho hakitazuia kuota kwa mbegu.
• Mara baada ya kuatika mbegu, mwagilia maji kiasi cha kutosha kulingana na unyevu nyevu ulioko ardhini
Mambo ya Kuzingatia baada ya kusia mbegu pamoja na Matunzo Kitaluni
• Mwagilia maji kwenye kitalu baada ya kuotesha kulingana na unyevu nyevu uliopo kwenye udongo.
• Miche yote ikisha ota, ondoa matandazo, kisha weka chanja ili kupunguza mionzi ya jua ambayo inaweza kuunguza miche michanga. (kipindi cha baridi si muhimu sana)
• Punguzia miche (thinning) ili ibakie kwenye nafasi ya kutosha. Hivyo miche ibakie kwenye umbali wa sentimita 2.5 - 4. Hii itapunguza magonjwa ya ulemavu na mnyauko, pia itasaidia kupata miche bora na yenye nguvu.
• Endelea kumwagilia hadi miche ifikie kimo kinachofaa kuhamishia shambani.
• Punguza kiwango cha umwagiliaji maji, siku chache kabla ya kuhamishia miche shambani, yaani siku 7-10.
Maandalizi ya Shamba la Nyanya
• Shamba la nyanya liandaliwe mwezi 1-2 kabla ya kupanda miche.
• Mara baada ya kulima choma nyasi juu ya udongo au ondoa magugu yote yanayoweza kuhifadhi wadudu na magonjwa ya nyanya.
• Siku moja au mbili kabla ya kuhamishia nyanya shambani, mwagilia sehemu iliyoandaliwa kwa ajili ya kuhamishia nyanya.
• Nafasi kati ya mche hadi mche ni wastani wa sentimita (50-60) x (50-75) kutegemeana na aina au hali ya hewa. Kama ni kipindi cha baridi ni vyema nyanya zikapandwa mbalimbali ili kuruhusu mzungungo wa hewa na kuzuia magonjwa ya fangasi.
Kanuni na Mbinu za kuhamisha miche toka Kitaluni kwenda shambani (Transplanting Rules)
• Mwagilia miche masaa machache kabla ya kuhamishia miche shambani ili wakati wa kung’oa miche mizizi ishikamane vizuri na udongo.
• Kabla ya kuhamisha miche, mashimo yawe yamekwisha andaliwa katika nafasi zinazo stahili huko shambani.
• Miche ihamishwe wakati wa jioni ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na jua.
• Kwa ujumla karibu mazao yote ya mboga mboga huwa tayari kuhamishiwa shambani yakiwa na majani kamili kati ya 2-6 pamoja na mizizi mingi iliyostawi vizuri.
• Mche lazima uwe na afya nzuri, uwe umenyooka vizuri, hivyo miche yote iliyonyongea au myembamba kupita kiasi isichukuliwe wakati wa kupeleka shambani.
• Ng’oa miche kwa uangalifu hasa pamoja na udongo wake kwa kutumia vifaa husika ili mizizi isidhurike.
• Miche ihamishiwe shambani mapema mara baada ya kung’olewa toka kitaluni.
• Wakati wa kuhamisha miche, uangalifu mkubwa utumike ili kutoharibu miche/mizizi.
Jinsi ya kupanda miche:
• Hamisha miche toka kitaluni pamoja na udongo wake
• Sambaza mizizi vizuri kwenye shimo bila kukunja.
• Fukia miche kina kile kile ambacho shina lilikuwa limefukiwa bustanini.
• Mwagilia maji ya kutosha kulingana na unyevunyevu uliopo kwenye udongo kasha weka matandazo na kivuli ili kupunguza uharibifu unaosababishwa na mionzi ya jua.
Mambo muhimu ya kuzingatia baada ya kuhamishia Miche Shambani
• Kagua shamba mara kwa mara ili kujua maendeleo au matatizo yaliyoko shambani mapema
• Hakikisha shamba ni safi wakati wote, palilia shamba na hakikisha magugu yote hasa yale ya jamii ya nyanya yamelimiwa chini.
• Ondoa mimea iliyoshambuliwa na magonjwa au ondoa sehemu zilizoshambuliwa, kisha zifukiwe chini au kuunguza moto.
• Punguza matawi na vikonyo ili kuongeza mwanga wa kutosha kwenye nyanya pamoja na kuruhusu mzunguko wa kutosha wa upepo na kusababisha mazingira magumu ya wadudu maadui kwenye nyanya, hasa wale wanaopenda kiza na magonjwa yanayopendelea unyevunyevu.
Utunzaji wa shamba la nyanya:
1. Uwekaji wa matandazo (Mulching)
Matandazo yanasaidia kufunika ardhi ili kutunza unyevunyevu, kuzuia magugu, pia matandazo yanasaidia kuzuia matunda ya nyanya yasigusane na udongo ambapo yanaweza kuoza. Matandazo yanaweza kua ya aina mbalimbali, kama vile majani makavu, nyasi au hata maranda yanayatokana na miti wakati wa upasuaji mbao (sawdust). Matandazo ya aina hii ni mzuri zaidi ya yale ya plastiki ambayo sio rahisi kuoza. Matandazo ya nyasi, maranda au majani yakioza yanakua mbolea nzuri na kurutubisha ardhi. Uwekaji wa matandazo una ufanisi kwenye kilimo cha eneo dogo, ila kwa maeneo makubwa, upatikanaji wa matandazo unakawa ni changamoto.
2. Kusimika miti ya kufungia mmea (Staking)
Uwekaji wa miti/mambo kwa ajili ya kusaidia mmea wa nyanya, kunasaidia nyanya zisianguke au kutambaa kwenye udongo kitu ambacho kinaweza kusababisha madhara kama magonjwa. Miti inapaswa kuwekwa wiki 2 hadi 3 baada ya upandikizaji wa miche.
Uwekaji wa miti unasaidia ukuaji wa nyanya na hivyo kupelekea kuzaa zaidi. Kwa aina ndefu za nyanya uwekaji miti hauepukiki ni lazima uweke miti ya kueleweka ambayo itaruhusu ukuaji mzuri, pia miti lazima iwe imara ili kuweza kustahimili mzigo wa nyanya pindi nyanya itakapokua imezaa vizuri. Kwa nyanya fupi (determinate) na saizi ya kati (semi determinate kwa mfano kipato F1) Tumia fito ndefu (mt 1.5) na nene (cm 4-5) pamoja na kamba ngumu hasa za katani au kudu.
Kwa nyanya ndefu ( indeterminate mfano victory F1, Anna F1) ni bora zaidi utumie nguzo nene/milunda urefu Mt 2.5 unene sm 10-12 pamoja na waya na kamba nzuri za kudu ( zitatengeneza umbo kama la njia ya umeme). zoezi lifanyike kabla ya mimea kuanza kuweka maua
3. Umwagiliaji
Nyanya hazivumilii ukame. Mavuno yanapungua kwa kiwango kikubwa endapo nyanya zitakosa maji. Ni muhimu kumwagilia mara kwa mara, hasa kama nyanya unalima kipindi cha kiangazi ambapo hakuna mvua. Kiwango cha maji ya umwagiliaji kinategemea aina ya udongo pamoja na hali ya hewa. Udongo wa mfinyazi umwagiliaji ufanyike mara 2 mpaka mara 3 kwa wiki. Udongo wa tifutifu na Kichanga, umwagiliaji ni Mara moja kwa siku. Umwagiliaji ufanyike asubuhi kwa maana mchana mmea ndio unahitaji maji. Zingatio Muhimu: Umwagiliaji ufanyike kutegemeana na Unyevunyevu wa udongo - Kama udongo una unyevunyevu wa kutosha, hakuna haja ya kumwagilia.
4. Udhibiti wa magugu (Palizi)
Palizi inapaswa kufanyika wiki 2 au 3 baada ya upandikizaji, ila pia inategemea na uotaji wa magugu katika eneo husika. Hakikisha shamba lako linakua safi bila magugu, maana magugu huvutia na kuficha wadudu na magonjwa. Magugu pia yana uwezo mkubwa wa kutumia virutubisho vilivyomo ardhini kuliko mazao, ndio maana magugu yanakua haraka kuliko mazao shambani. Hivyo hakikisha unafanya palizi mara 3 au 4 kulingana na kasi ya uotaji magugu.
5. Uwekaji wa mbolea
Mbolea ya kupandia huwekwa wakati wa kupandikiza, unaweka 5g kwenye shimo moja (gramu 5 ni sawa na kifuniko cha soda kimoja). Mbolea ya kupandia unaweza kutumia DAP, MAP, Minjingu n.k. Mbolea ya kukuzia unaweka wiki 2 au 3 baada ya kupandikiza. Ni vizuri mbolea inapowekwa shamba liwe safi, liwe halina magugu, kama kuna magugu fanya palizi kwanza. Mbolea ya kukuzia unaweza kutumia Urea, NPK n.k
6. Uvunaji na Utunzaji wa nyanya baada ya kuvuna
Nyanya ina maisha mafupi baada ya kuvunwa, ni rahisi kuharibika maana sehemu kubwa ya nyanya ni maji. Upotevu wa mavuno baada ya kuvuna inakadiriwa kua asilimia 5 hadi 50.
Upotevu wa mazao baada ya kuvunwa husababishwa hasa na utunzaji duni wa mazao hayo, njia duni za usafirishaji, pamoja na kuchelewa kuvuna. Kupunguza upotevu unashauriwa kuvuna kwa wakati nyanya zako. Maana nyanya zilizoiva sana, ni rahisi kuharibika wakati wa uvunaji na hata wakati wa kusafirisha maana ganda lake la nje linakua ni laini. Kama soko lako liko mbali vuna nyanya zikiwa ndio zimeanza kuonyesha dalili ya kuiva maana wakati huo nyanya inakua na ganda gumu hivyo kuweza kuvumilia mikikimikiki ya usafirishaji. Lakini pia nyanya itaweza kukaa muda mrefu zaidi bila kuharibika ikilinganishwa na ile iliyovunwa ikiwa imeiva sana. Ila pia zipo aina za nyanya zinazokaa muda mrefu wa hadi wiki 3 bila kuharibika kama zikitunzwa vizuri.
Wakati wa usafirishaji hakikisha unaweka nyanya kwenye vifungashio imara kama kreti ama boksi. Ukiweka kwenye mifuko ni rahisi nyanya kupondeka kutokana na mtikisiko pindi zisafirishwapo hasa kama barabara zenyewe ni za vijijini.
Masoko ya nyanya:
Kuna aina kadhaa za masoko ambapo nyanya zinaweza kuuzwa.
1. Kuna masoko yasiyo raami au masoko ya kawaida (informal markets) kama Kilombero, Arusha, Kariakoo Dar, soko kuu Morogoro, Buhongwa, Mwanza, na masoko mengine kama hayo yaliyotapakaa nchi nzima. Changamoto ya masoko haya unapitia msururu wa madalali, kila mmoja anataka naye apate. Masoko haya ndiyo yanatumia asilimia kubwa ya nyanya zinazozalishwa. Inakadiriwa kwamba zaidi ya Asilimia 80 ya nyanya zinazozalishwa zinauzwa kwenye masoko hayo.
2. Masoko ya kitaasisi (institutional markets) kama supa markets, mahotelini, hospitali, mashule n.k, Unaweza Kutafuta tenda za kupeleka (supply) nyanya kwenye masoko haya. Mfano kama kuna mahoteli unaweza kuyatembelea na kujua wanahitaji nyanya za aina gani, kiasi gani kwa siku au kwa wiki, wanapata wapi nyanya n.k. Kisha ukazalisha kulingana na mahitaji yao ikiwa mtakubaliana. Wapo wakulima wanaohudumia hayo masoko kwa mikataba au kwa kutokua na mikataba.
3. Masoko ya kiviwanda (Industrial markets) kama vile Darsh Industries maarufu kama REDGOLD ambao wako arusha , wao wanazalisha bidhaa nyingi zinazotokana na nyanya kama Tomato Sauce. Pia kipo kiwanda kinaitwa IVORI Iringa kinachotumia nyanya kama malighafi n.k
4. Masoko ya nje.
Aina hizo tatu za mwisho zinahitaji ubora wa hali ya juu, ndio maana wachache ndio wanaofaulu kuuza kwenye masoko hayo. Mfano masoko ya nje bidhaa yako lazima ikidhi vigezo vya kimataifa au vya nchi husika.
Bei za nyanya:
Bei za nyanya zinategemeana na misimu na aina ya soko. Kwenye masoko haya kawaida Bei ya nyanya mara nyingi inakua kubwa kuanzia mwezi Oktoba hadi mwezi Machi au hata Aprili. Kipindi cha kuanzia mwezi December uzalishaji unakua ni mdogo maana watu wachache ndio wanazalisha, maana kipindi hicho changamoto ni nyingi, kwanza maji ya umwagiliaji yanakua ni tatizo maana wazalishaji wengi wanategemea mvua. Hivyo wale wachache walioko kwenye vyanzo vya maji ndio wanaozalisha. Lakini pia kipindi hicho kuna changamoto kubwa ya wadudu na magonjwa, hii hupelekea mavuno kua madogo na gharama za utunzaji nazo ni kubwa. Kipindi hichi bei ya nyanya shambani ni Shs. 6,000 hadi 12,000 kwa ndoo ya lita 20. Bei ya sokoni hua ni Shilingi 9,000 hadi 25,000 kwa ujazo wa ndoo ya lita 20.
Msimu wa mwezi wa Aprili hadi Septemba bei ya nyanya inakua chini, maana uzalishaji ni mkubwa, maeneo mengi hali ya hewa ni nzuri kwa uzalishaji. Kipindi hichi bei ya nyanya ni 2,000 hadi 5,000 kwa ndoo ya lita 20.
Kwa mujibu wa TAHA, Bei ya Nyanya katika masoko mbalimbali kwa Leo Tarehe 13.12.2016 ni kama ifuatavyo:
Makambako: 25,000TSh./Kreti40Kg
Soweto: 30,000TSh./Tenga40Kg
Lushoto: 20,000TSh./Tenga40Kg
Arusha: 28,000TSh./Tenga40Kg
Kirumba: 20,000TSh./Kreti40Kg
Kongowea Kenya: 21,300TSh./Kreti40Kg
Kariakoo: 20,000TSh./Kreti40Kg
Morogoro: 30,000TSh./Tenga40Kg
Mwanakwerekwe ZnZ: 45,000TSh./Kreti40Kg
Dodoma: 60,000TSh./Tenga40Kg
Mombasa ZnZ: 50,000TSh./Kreti40Kg
Mtwara: 30,000TSh./Tenga40Kg
Hiyo ndio hali ya kwenye masoko ya kawaida. Kwa upande wa masoko rasmi (viwanda, mahoteli, masoko ya nje), hakuna mabadiliko makubwa ya bei kama ilivyo kwenye masoko hayo mengine, japo mabadiliko yapo.
Hata hivyo pamoja na hayo yote, ili uweze kupenya kwenye soko na kulifaidi soko lazima uwe mbunifu. Kumbuka mjasiriamali haishii tu kufuata soko, bali analitengeneza soko. Lazima uwe mdadisi, ufanye kwa utofauti. Lengo la kujifunza hapa ni kukupa msingi mzuri wa kua mbunifu. Nakuachia kanuni hizi tatu za kuliteka soko: Ya kwanza kua mbunifu, ya pili kua mbunifu na kanuni ya tatu nasema kua mbunifu. (credit: KILIMO BIASHARA)
Asante sana. Tukutane wakati mwingine