Saturday, 17 December 2016

MBUNGE KAFULILA ARUDI CHADEMA



Mbunge wa zamani wa Jimbo la Kigoma Kusini kwa tiketi ya Chama cha NCCR-Mageuzi, David Kafulila leo ametangaza kukihama chama hicho na kusema kuwa atajiunga na Chama cha Demokrasia na Manendeleo (CHADEMA).


Kafulila ambaye alijizolea umaarufu mkubwa katika bunge la kumi kwa kufichua hoja mbalimbali za ufisadi amesema kuwa ameshawasilisha barua ya kujiuzulu kwa uongozi wa chama hicho.


Akieleza sababu iliyomsukuma kujiunga na CHADEMA, Kafulila alinukuliwa akisema kuwa kikubwa ni kuhakikia wanaleta mabadiliko nchini Tanzania. 



"Ili kufanya safari kuwa fupi, kuondoa vikwazo vya huyu yuko chama hiki mwingine kile nimeamua kujiunga na CHADEMA ili kurahisisha uletaji mabadiliko katika nchi yetu sababu nimeona uhitaji huo," alisema Kafulila.


Katika uchaguzi uliopita Kafulila alipoteza jimbo la Kigoma Kusini ambalo lilikwenda wa Hasna Sudi Katunda Mwilima aliyekuwa akigombea kupitia Chama cha Mapinduzi.


MMILIKI WA JAMIIFORUM AENDELEA KUSOTA LUMANDE



Mwanzilishi na Mtendaji Mkuu wa Mtandao wa JamiiForums, Maxence Melo akiongozwa na Askari Polisi wakati alipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es salaam leo, kusomewa mashtaka yanayomkabili kama inavyosomeka hapa chini.



Mwanzilishi-mwenza na Mkurugenzi wa Kampuni ya Jamii Media, Maxence MeloMubyazi (40), leo amepelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana katika kesi moja kati ya tatu zinazomkabili ikiwamo ya kuzuia Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi na kuendesha mtandao wa Jamii Forum bila usajili.

Mapema leo asubuhi mshtakiwa huyo ambaye pia ni
mfanyabiashara na bosi wa mtandao huo, alifikishwa katika viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam mapema asubuhi.


Alipandishwa kizimbani saa 3:29 kusomewa mashtaka katika kesi yake ya kwanza mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Upande wa mashtaka uliongozwa na Wakili wa Serikali
Mwandamizi, Mohamed Salum akisaidiana na Wakili wa Serikali Mkuu, Yohanes Kalungula.

Wakili Salum alidai kuwa katika tarehe tofauti kati ya Aprili Mosi na Desemba 13, mwaka huu eneo la Mikocheni, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Jamii Media Ltd, inayoendesha mtandao wa kijamii wa Jamiiforums, akiwa anajua polisi wanafanya uchunguzi kutokana na taarifa zilizochapishwa katika mtandao huo, alishindwa kutoa taarifa. Ilidaiwa kuwa mshtakiwa alishindwa kutoa taarifa ambazo ziko chini yake huku akijua ni kosa.

Mshtakiwa alikana shtaka hilo, upande wa Jamhuri ulidaia kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, na haukuwa na pingamizi la dhamana hivyo uliomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Hakimu Simba alisema mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana kwa kuwa na wadhamini wawili wanaotoka taasisi zinazotambulika au serikalini, watakaotia saini hati ya dhamana ya Sh. Milioni 10 kila mmoja.

Mshtakiwa alitimiza masharti hayo dhidi ya kesi hiyo na imepangwa kutajwa Desemba 29, mwaka huu.

Katika kesi ya pili, mshtakiwa alisomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Godfrey Mwambapa. Wakili Salum alidai kuwa katika tarehe tofauti kati ya Mei 10 na Desemba 13, mwaka huu eneo la Mikocheni, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa kama Mkurugenzi wa Kampuni ya Jamii Media Ltd, inayoendesha mtandao wa kijamii wa Jamiiforums, huku akijua kwamba polisi wanafanya uchunguzi kuhusu taarifa zilizochapishwa katika mtandao wake, alishindwa kutoa taarifa hizo ambazo ziko chini yake. Mshakiwa alikana shtaka
hilo.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado
unaendelea na haukuwa na pingamizi la dhamana na uliomba tarehe ya kutajwa. Hata hivyo, mshtakiwa katika kesi hii alishindwa kutimiza masharti ya dhamana kwa kutokuwa na wadhamini na alirudishwa mahabusu hadi Desemba 29, mwaka huu kesi yake itakapotajwa.

Katika kesi ya tatu, mkurugenzi huyo alipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa.

Wakili Salum alidai kuwa katika tarehe tofauti, kati ya Desemba,mwaka 2011 na Desemba 13, mwaka huu eneo la Mikocheni, jijini Dar es Salaam,mshtakiwa akiwa kama mkurugenzi wa kampuni hiyo, aliendesha mtandao wa kijamii
ujulikanao kama Jamiiforums.com bila kuwa na usajili wa kuendesha mtandao huo.

Katika shtaka la pili, katika tarehe tofauti, kati ya Januari 26
na Desemba 13, mwaka huu eneo la Mikocheni, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa mkurugenzi wa kampuni hiyo inayoendesha mtandao wa kijamii wa Jamiiforums huku akijua kwamba polisi wanafanya uchunguzi kuhusu taarifa zilizochapishwa katika mtandao wake alishindwa kutoa taarifa hizo ambazo ziko chini yake.

Mshtakiwa alikana mashtaka hayo. Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Hakimu alisema mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana kwa kuwa na mashahidi wawili wanaotoka taasisi zinazotambulika watakaosaini hati ya dhamana ya Sh. Milioni Moja kila mmoja pamoja na mshtakiwa. Mshtakiwa alitimiza masharti hayo na kesi yake itatajwa Januari 16, mwaka 2017.



SERIKALI YAWATOA HUFU WANANCHI KUHUSU UGONJWA WA ZIKA,SOMA HAPO KUJUA



Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekanusha uwepo wa taarifa juu ya ugonjwa wa ZIKA hapa nchini.


Waziri wa Afya, Mh. Ummy Mwalimu pamoja na Naibu wake Dk. Hamisi Kigwangalla wakitolea ufafanuzi mbele ya waandishi wa Habari, wamesema wananchi wasiogope na wamewatoa hofu kwani taarifa zilizotolewa awali na kuripotiwa na vyombo vya habari walizonukuu kutoka NIMR hazina ukweli wowote na za kupuuzwa.


Aidha, kwa mujibu wa Kaimu Mkuu kitengo cha Mawasiliano Serikalini (Afya), Bi. Catherine Sungurakatika taarifa ya Waziri wa Afya, Mh. Ummy Mwalimu ilieleza: “Napenda kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa zilizoenea kwenye vyombo vya habari na mitandao ya jamii kuhusu uwepo wa ugonjwa wa Zika nchini.

Kama nilivyoeleza mnamo tarehe 31 Januari 2016, ugonjwa huu bado haujaingia nchini, na leo pia napenda kuwatoa hofu wananchi kuwa kwa sasa Tanzania haujathibitishwa kuwepo na ugonjwa wa Zika. Utafiti uliofanywa na NIMR, ulikuwa ni utafiti uliofanyika nchini wa kuchunguza ubora wa kipimo kipya cha kupima magonjwa ya zika na chikungunya.

Kwa utaratibu wa kitafiti, hii ni hatua ya awali tu ya kuangalia ubora na uwezo wa kipimo hicho.Matokeo haya bado yanahitaji kuchunguzwa kwa kina zaidi kupitia vipimo vilivyothibitishwa na Shirika la Afya Duniani.

Wizara itaendelea kushirikiana na Taasisi mbalimbali mbali ndani na nje ya nchi kuendelea na utafiti na ufuatiliaji wa kitaalamu ili kuzuia ugonjwa huu kuwepo Tanzania. Ufuatiliaji wa magonjwa ni endelevu katika sekta ya afya na tuna taratibu za utoaji taarifa wa magonjwa ya kuambukiza na hatari kama vile zika, ebola na mengineyo. Wizara yangu imeshaandaa mkakati wa Zika nchini, ambao unaelekeza utelezaji wa ufuatiliaji wa Zika.


WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...