Saturday, 6 August 2016

MSHINDI WA AIRTEL TRACE MUSIC STAR 2015 AZUNGUMZA NA VIJANA JIJINI MWANZA



Star wa Airtel Trace Music 2015, Mayunga Andrew Nalimi-MAYUNGA, akizungumza na #BMG kuhusiana na project yake ambayo anaifanya na star M-Rap.


Na George Binagi-GB Pazzo

Project inaitwa Across Lovers and Friend Music Tour ambayo Mayunga anaitumia kukutana na mashabiki zake na kuwapa burudani ikizingatiwa tangu atoke Marekani hakuwahi kufanya tour kama hiyo kwa ajili ya mashabiki zake.

Mayunga amesema Project hiyo imeanzia Mwanza na itaendelea katika mikoa mingine na hata nje ya nchi kama vile Kenya, Uganda, Malawi na Afrika Kusini.

Awali Mayunga pamoja na M-Rap kwa kushirikiana na Star Foundation na Kwanza Online na timu nzima ya Trace Music, waliweza kukutana na vijana Jijini Mwanza kwa ajili ya kuzungumza nao kuwahamasisha kutumia vipaji vyao ili kujikwamua kimaisha.


Mayunga akizungumza na BMG


Stella Mutta ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Star Foundation ya Jijini Mwanza, akizungumza na BMG


Petro Malongo ambaye ni mmoja wa Vijana waliohudhuria Inspiration Event ya hii leo


MAALIM SEIF AZUNGUMZA NA WAZANZIBARI BOSTON



Na Mwandishi wetu Boston 



Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, jana aliwasili Zanzibar akitokea Ughaibuni baada ya kukamilisha awamu ya pili ya ziara yake ya Mataifa mbalimbali Ulimwenguni.




Wazanzibari wakimsikiliza Maalim Seif (Picha na swahilivilla.Blog)




Katika awamu hiyo ya pili, Maalim Seif alitembelea Marekani na kupata nafasi ya kuzungumza na Wazanzibari katika jimbo la Massachusetts. Ifuatayo ni sehemu ya mwisho ya mfululizo wa makala zetu za "Maalim Seif azungumza na Wazanzibari Boston"



Akiwa mwishoni mwishoni mwa hotuba yake, Mwanasiasa huyo Mkongwe alikariri msimamo wa CUF wa kutoitambua serikali ya Zanzibar iliyoko madarakani kwa vile haikupata ridhaa ya wananchi, akisisitiza kuwa serikali hiyo pia haitambuliki Kimataifa.



"Hatuitambui serikali ya Dakta Shein, na hakuna taifa hata moja linaloitambua", alisisitiza.


Maalim Seif alielezea kwamba, wakati wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, wafanyazi wa serikali walikuwa wakipokea mishahara yao kwa wakati. Lakini matokeo ya serikali hiyo kugomewa na wanchi na kutengwa kimataifa, kumezidisha hali ya kiuchumi kuwa mbaya kiasi kwamba serikali inashindwa kuwalipa mishahara wafanyakazi wake kwa wakati.



"Tulifikia hatua nzuri, kiasi kwamba tarehe 22-23 watu walikuwa wameshapata mishahara yao. Sasa hali imezidi kuwa mbaya kiuchumi kiasi kwamba inafika mpaka tarehe 3 watu hawajalipwa", alisisitiza.



Kama Wahenga walivyosema: "Baada ya dhiki faraja", Maalim Seif naye aliwataka Wazanzibari kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha mpito, akiwahakikishia kuwa serikali iliyopo madarakani haitodumu.



".... Wananchi wavumiliye, na mwisho serikali hii itaondoka madarakani", alisihi, na kutamba: "Tutaendelea kufanya wajibu wetu na hatuchoki. Wala wasidhani kuwa tutarudi nyuma kwa kutukamata".



Aidha alikariri wito wake kwa jamii ya Kimataifa wa kuendelea kuibana serikali akisema: "Tunaiomba Jamii ya Kimataifa waendelee kuibana serikali........, na Inshallah itaondoka" alisema huku akijibiwa kwa kauli za "Amin"



Kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi. Kwa hivyo, kukhusu vitisho vilivyotolewa dhidi yake vya uwezekano wa kukamatwa, Maalim Seif aliyewahi kuwekwa gerezani kwa miaka kadhaa alisema kuwa kukamatwa kwake siyo mwisho wa harakati za Wazanzibari kudai haki yao, akisisitiza: "Kuna Maalim Seif zaidi ya mmoja" Aliongeza kwa kuwaonya viongozi wa Zanzibar dhidi ya kuchukuwa khatua kama hiyo kwa kusema: "....Washukuru sasa hivi kuna mtu ambaye angalau anaweza kusema na watu wakamsikiliza...."



Kukhusu suluhisho la mzozo wa sasa wa kisiasa Visiwani Zanzibar, Maalim Seif alitoa rai ya kuundwa kwa serikali ya mpito itakayosimamiwa na watu wanaoheshimika na ambao hawaelemei upande wowote wa kisiasa. Jukumu kubwa la serikali hiyo ya mpito litakuwa kufanya marekebisho ya sheria za uchaguzi visiwani humo: "Khaswa khaswa Tume ya Uchaguzi", aligogoteza.



Mahakama Ya Kimataifa:



Ni vizuri kukumbusha kuwa katika awamu yake hii ya pili ya ziara zake za Kimataifa, Maalim Seif na ujumbe aliofuatana nao walifika jijini The Hague, Uholanzi, na kufikisha malalamiko ya Wazanzibari.



Alipoulizwa iwapo hatua hiyo ina umuhimu wowote, hususan kwa vile viongozi wengi wa Kiafrika wamekuwa wakitoa wito wa kujitoa kwenye mkataba wa Kimataifa unaohusiana na mahakama hiyo, Maalim Seif alisema: "Azimio lenyewe halikupita kwenye Mkutano wa Kilele wa Umoja Wa Afrika uliopita"



"Tumejidhatiti kikweli kweli kwa hili, kama wanadhani tunatania, wasubiri", alisistiza na kuongeza: "Tumepata Wakili mahiri, na anasubiri tumpatie vielelezo zaidi tu..., kwa hivyo tuko 'serious' kwa hili" Akijibu swali kukhusu kile kilichoandikwa na baadhi ya magazeti ya Tanzania kuwa Mahaka hiyo ya Uhalifu (ICC) imeitaka CUF kukanusha madai yake, msaidizi wa Maalim Seif aliyefuatana naye kwenye mkutano huo Bwana Issa Kheri Hussein, alitupilia mbali uzushi huo na kusema kuwa hiyo ni propaganda tu.



Aidha alisema kuwa hizo ni mbinu za kuitafuta CUF itoe maelezo kukhusu kile kinachoendelea The Hague kwa vile bado watu hawajui khaswa kinachoendelea na madai yaliyomo katika shauri hilo.


N/WAZIRI JAFO: WATANZANIA WANAPASWA KUTHAMINI BIDHAA ZINAZOZALISHWA NCHINI


Naibu waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za mitaa TAMISEMI Jafo Suleiman Said akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mara baada ya kutembelea banda la Halmashauri hiyo.




Mgeni na Mwenyeji wakifurahi kufuatia maandalizi mazuri ya Maonesho ya Nane nane kanda ya kati.




Naibu waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za mitaa TAMISEMI Jafo Suleiman Said akisikiliza maelezo ya namna ya kulima kilimo na ufugaji wa kisasa




Na Mathias Canal, Dodoma

Watanzania wametakiwa kuthamini na kununua bidhaa zinazozalishwa nchini Tanzania hususani katika sekta ya Kilimo, Ufugaji na uvuvi kwani hakuna sababu ya kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi ilihali bidhaa hizo wanazoagiza zinazalishwa na watanzania wenzao.

Naibu waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za mitaa TAMISEMI Jafo Suleiman Said ameyasema hayo mara baada ya kutembelea baadhi ya mabanda katika maonyesho ya wakulima Nane nane Kanda ya kati Dodoma yanayofanyika katika uwanja wa Nzuguni huku kauli mbiu ya mwaka huu ikiwa ni "Kilimo, Mifugo na Uvuvi ni nguzo ya maendeleo, Kijana shiriki kikamilifu (Hapa Kazi Tu).

Jaffo amesema kuwa asilimia kubwa ya watanzania wamekuwa watumwa wa mambo ya kigeni, kuiga tamaduni mbalimbali ikiwemo matumizi ya bidhaa zinazotoka nje ya nchi wakati pia bidhaa hizo zinazalishwa nchini, huku akitolea mfano wa manunuzi ya viatu kutoka nchi mbalimbali wakati hapa nchini Jeshi la Magereza linatengeneza viatu bora vya ngozi tena kwa bei nafuu.

Sambamba na hayo pia Naibu Waziri huyo ameiagiza Mamlaka ya Ustawishaji Makao makuu Dodoma kusimamia vyema na kwenda na kasi kubwa katika utengenezaji wa stendi kubwa na ya kisasa ili kufanana na mji wa Dodoma ambapo pia hivi karibuni makao makuu ya serikali yatahamia mjini hapo.

Aidha ameongeza kuwa Maonesho hayo yanapaswa kuboreshwa ili maonyesho yajayo yawe ya kitaifa ambapo nchi mbalimbali zitapata fursa ya kutembelea na kuifanya Tanzania kujikomboa katika wimbi la umasikini.

Maonesho hayo yanahusisha Shughuli za wakulima, wafugaji wa mifugo, wafugaji wa nyuki, wavuvi, wana mazingira, wasindikaji wa bidhaa za mazao ya kilimo na mifugo, wizara taasisi/Makampuni ya umma, makampuni Binafsi, mabenki, taasisi za umma na za binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali.

Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya waandaaji wa Maonesho hayo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida Miraji Jumanne Mtaturu amesema kuwa maandalizi ya maonyesho hayo yametumia muda mfupi lakini kwa kiasi kikubwa yamekuwa bora na kuahidi kuwa na Maonesho yajayo kuwa bora zaidi katika kipindi kinachokuja.

Mtaturu amesema kuwa lengo mahususi la maonesho hayo ni utoaji wa elimu ya matumizi ya teknolojia mbalimbali kwa wadau wengi kwa muda mfupi ambapo watajifunza kwa njia ya kuona, kujadiliana na kuulizana maswali.

Ameongeza kuwa maeneo makuu ya mafunzo ni teknolojia za uzalishaji wenye tija wa mazao, mifugo na usindikaji wa bidhaa ili kuongeza thamani.

Dc Mtaturu amesema kuwa pia wadau watajionea na kujifunza huduma zitolewazo na serikali, Mashirika ya umma na binafsi, ambapo wafanya biashara wanayatumia maonesho hayo kwa kuuza bidhaa, kufahamiana na kuingia makubaliano.

Kwa upande wake Katibu wa maandalizi ya Maonesho hayo Aziza Rajabu Mumba amesema kuwa Wanatarajia kila mwananchi atakayetembelea maonesho hayo kwenda kutekeleza kwa vitendo anayojifunza katika eneo lake na kuwafundisha wengine ambao hawakupata fursa ya kuhudhuria kwenye Maonesho hayo.

Aidha amesema Malengo ya muda mrefu ni kuendeleza uwanja wa Nzuguni ufikie ubora na hadhi ya viwanja vya maonesho ya Kilimo Kimataifa na kuendelea kushawishi wadau mbalimbali kuwekeza ili kuufanya uwanja wa Nzuguni uwe kituo cha huduma cha Maonesho ya Kilimo nchini kama ilivyo kwa uwanja wa Mwalimu Nyerere Dar es salaam kwa maonesho ya Biashara.


KIJIJI CHA LUDILO WAPITISHA SHERIA NDOGO ZA USIMAMIZI WA MALIASILI









Wananchi wa kijiji cha Ludilo wilayani Mufindi, mkoani Iringa wamepitisha sheria ndogo ya usimamizi wa maliasili (misitu na wanyamapori) ilikukabiliana na kasi ya uharibifu wa rasilimali hizo.

Hatua hiyo ilifikiwa tarehe 4 Augusti, 2016 katika mkutano wa hadhara ambapo Diwani wa kata ya Mdabulo Mheshimiwa Henry Nyeho pamoja na Mwanasheria wa Wilaya ya Mufindi Leonard Jaka walihudhuria mkutano huo.


Sheria zilizopitishwa na wananchi hao ndio itakayotumika katika usimamizi wa maliasili.

Mchakato wa uboreshaji sheria ulianza mwezi Juni, 2016 ambapo Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) kwa kushirikiana na Mwanasheria wa Wilaya ya Mufindi pamoja na wananchi hao, kupitia mkutano wa hadhara waliangalia upya sheria zilizokuwa zikitumika kijijini hapo na kugundua kuwa zilikuwa na mapungufu. 


Wananchi wakiongozwa na Wanasheria kutoka LEAT na Mwanasheria wa Wilaya Mufindi walitoa mapendekezo ya maboresho na kuiruhusu timu ya LEAT kuchapisha sheria hizo mpya ambazo ziliwasilishwa tarehe 4 August 2016. 



Mtendaji wa kijiji cha Ludilo Martin Mwanule alisoma kipengele kimoja baada ya kingine kupitishwa na wananchi. 


Sheria hizo zinaelekeza haki na wajibu wa wananchi, serikali ya kijiji, kamati ya maliasili pamoja na timu ya Ufuatiliaji Uwajibikaji Jamii. Pia sheria zimefafanua adhabu zitakazotolewa kwa watu watakao kiuka sheria na kuharibu maliasili. 

Hii ni awamu ya kwanza ya kuzijengea uwezo serikali za vijiji wa kuunda sheria ndogo za kusimamia maliasili. 



Katika awamu hii vijiji vya Ludilo, Ikangamwani na Kibada kwa wilaya ya Mufindi. Kwa wilaya ya Iringa ni vijiji vya Mbweleli, Kinyika na Kinyali.


Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) inatekeleza mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili katika vijiji 32 vya wilaya za Iringa na Mufindi mkoani Iringa.

Mradi huu umefadhiliwa na Watu wa MArekani kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la MArekani (USAID). 

Lengo la mradi ni kuzijengea uwezo jamii zinazoishi karibu na rasilimali misitu na wanyamapori, iliwaweze kuzisimamia na kunufaika nazo. 

Mradi unatoa mafunzo ya sheria, sera, miongozo, kanuni na Ufuatiliaji uwajibikaji jamii kwa kamati za vijiji za maliasili na mazingira, uchumi, maji na matumizi ya ardhi. 

Pia mradi umetoa mafunzo kwa wananchi, madiwani na asasi za kiraia. Takriban wananchi 6500 watafikiwa na mafunzo hayo. 

Katika kutimiza azma ya kutoa elimu ya usimimizi wa maliasili kwa wananchi wengi, LEAT inatoa mafunzo kwa njia ya redio, sambamba na kutoa elimu kwa njia ya sanaa kupitia kikundi cha Sanaa Mashujaa kwa wilaya ya Iringa na kikundi cha Sanaa Mapogoro kwa wilaya ya Mufindi.





LHRC YAMPA MAPOKEZI MAKUBWA MWANAHARAKATI GELINE FUKO AKITOKEA MAREKANI




Geline Fuko (kushoto) akipokea maua kutoka kwa wafanyakazi wenzake wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC),ikiwa ni ishara ya kumpongeza baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam jana, akitokea Marekani alikokuwa akihudhuria mafunzo ya vijana wa kiafrika yaliyoandaliwa na Rais Obama. 






Na Dotto Mwaibale


SHANGWE ilitawala wakati mtanzania Geline Fuko alipo wasili Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) majira ya saa nne usiku jana Agosti 5, 2016 akitokea nchini Marekani alikohudhuria mafunzo ya viongozi vijana kutoka Bara la Afrika. 


Wafanyakaziwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ambao ni wafanyakazi wenzake wa Geline, familia ya Geline, ndugu na marafiki walitoa mapokezi ya kishujaa wa wanaharakati huyo aliyetajwa kuwa mfano wa kuigwa na Rais Obama.


Akizungumza na wanahabari, Geline alisema amefarijika na hakutarajia kama wazo lake la kuanzishwa kwa Kanzidata ya Katiba litakuwa wazo kubwa ambalolitakubalika mpaka na Rais Obama. 

Hata hivyo Geline alisema amefurahishwa na program hiyo ya Mandela Washington Fellowship kwani imewawezesha washiri kikujifunza mambo mengi na kupata uono mpana zaidi wakufanya mambo.


Geline iliwahimiza watanzania kutembelea Kanzidata hiyo iliyopo mtandaoni (http://katiba.humanrights.or.tz/) ili kuweza kuijua katiba yao na kuweza kujua haki zao kama watanzania. 

Mwisho alishukuru wa mapokezi makubwa ambayo pia hakuyatarajia.

Akitoa neno la shukurani kwa Geline kwa niaba ya LHRC, Mkurugenzi wa Fedha naUtawala-LHRC, Ezekiel Masanja amempongeza Geline kwa kuitoa kimasomaso LHRC na Tanzania kwa ujumla.

Geline Fuko amepata kutambulika baada ya Rais Obama kumtaja kama mfano wa kuigwa wa wanaharakati wa haki za binadamu wakati akizungumza Jumatano Agosti 3, 2016 katika kilele cha mpango wake wa kuwawezesha vijana wakiafrika unaojulikana kama Mandela Washington Fellowship. 


Rais Obama alimsifu mwanasheria huyo kutoka LHRC ambaye ni moja ya vijana 1000 waliokuwa jijini Washington kwa lengo la kujengewa uwezo ili kuweza kusaidia Maendeleo katika Nyanja zote za maisha katika nchi zao.

Rais Obama alisifu juhudi za Geline za kuibua wazo la kuanzisha kwamaraya kwanza Kanzidata ya Katiba nchini Tanzania kwa kutekeleza wazo hilo chiniya LHRC. 


Rais Obama alikaririwa akisema Marekani itaendelea kushikamana na wanaharakati kama Geline Fuko kutoka Tanzania. 


Geline ni mwanasheria na mwanaharakati wa haki za binadamu ambaye amefanikisha kuanzishwa kwa Kanzidata ya Katiba ya kwanza na yapekee nchini Tanzania inayowawezesha watanzania kusoma Katiba kupitia simu zao za mkononi”.


Programu ya Mandela Washington Fellowship yenye lengo la kuwa wezesha vijana wa Kiafrika katika Nyanja za kiuchumi, kisiasa, kiteknolojia na kijamii ilianzishwa na Rais Obama mwaka 2014. 

Programu hii hujumuisha vijana elfu moja (1000) kutoka nchi mbalimbali za Afrika ambao hugharamiwa na serikali ya Marekani kwenda jijini Washington kwa lengo la kujengewa uwezo zaidi.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kilianzisha Kanzidata ya Katiba mwaka mmoja uliopita mnamo Julai 15, 2015. 


Kupitia tovuti maalumu (http://katiba.humanrights.or.tz/) na simu za mkononi, watanzania wanaweza kusoma Katiba katika Kanzidata hiyo





WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...