BINADAMU anaelezwa kuwa ni kiumbe kilichochafuka na uchafu wa kutisha ambao anahitaji msaada kwa ajili ya kusafishwa.
Haya yamezungumzwa na Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania Mhashamu askofu Tarcisius Ngalalekumtwa alipokuwa akihubiri katika Mkesha wa Pasaka Parokia ya Bikira Maria Consolata - Mshindo Jimbo la Iringa.
Askofu Ngalalekumtwa ambaye pia ni askofu wa jimbo la Iringa alisema binadamu amejaa maovu ya kila aina ambayo yamekuwa kikwazo kwa wengine na kusema kuwa bila nguvu ya Mungu mwanadamu pekee hayawezi.
"Kristo amekuja kututoa katika uhuni, ufisadi, unyang'anyi na dhuruma. Maovu yetu tuliyo nayo yanatokana na ukaidi wetu na kiburi. Amebeba dhambi zetu akafa msalabani kwa ajili ya kutukomboa utumwani mwa shetani.
"Tumejipaka mavi, mikojo na uchafu wa kila aina. Tumejaa uchafu hata tumekuwa kinyaa, hatutamaniki kwa wengine. Sasa tumekombolewa kwa damu ya mwana kondoo" amesema.
Amesema mwanadamu ameingia mkataba wa urafiki na ibilisi na kumfanya kikaragosi wake kumtumikisha katika dhambi na kwamba muda wa kuufuta mkataba huo umefika.
Ameasa kuwa manyanyaso ya mwanadamu yanayotokana na ukaidi na kiburi kutopenda kutii maagizo ya Mungu kutenda mema.
Hata hivyo alisema mwanadamu ana deni kubwa kurudi kwa Mungu na kuachana na matendo yanayomchukiza Mungu kwa kuwapendeza wanadamu wenzake, kuachana na ufisadi na matendo yote yasiyo ya haki.
Katika Misa hiyo jumla ya watoto 74 wamepokea Sakramenti ya ubatizo.