Pichani ni Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala,Omary Ngumilamoto akifafanua jambo na waandishi wa habari (Picha na Maktaba)
NAIBU meya wa Manispaa ya Ilala,Omary Ngumilamoto amesema wataiondoa kwenye tenda Kampuni ya ujenzi wa Barabara Del-Monte katika manispaa hiyo baada ya kujiridhisha kampuni hiyo inafanya kazi chini ya kiwango ikiwemo kuchelewesha kumaliza kazi kwa wakati.Anaandika KAROLI VINSENT endelea nayo,
Kauli ya Ngumilamoto inakuja ikiwa ni tayari mkuu wa mkoa wa Dare s Salaam,Paul Makonda ambaye naye aliiagiza viongozi wote wa manispaa ya mkoa huo kutoipa tenda kampuni ya Del-Monte kutokana na kujenga barabara nyingi chini ya kiwango.
Ngumilamoto ambaye ni Diwani wa Kata ya Vingunguti kupitia chama cha Wananchi (CUF) ameyasema hayo leo wakati alipokuwa anafanya ziara na Kamati ya fedha ya Manispaa hiyo kwenye miradi mbali mbali iliyoanza kutekelezwa ili kujilidhisha juu ya ufanisi wake.
Amesema Kampuni hiyo ilipewa tenda ya kujenga barabara kutoka Mombasa hadi Mosha Baa kwa kiwango cha Lami ambayo inaurefu wa kilomotea 1.65 ambayo itagarimu Bilioni Sh 2.4 ambapo kwa sasa kampuni hiyo imepewa milioni 301,
“Hii Kampuni ya Del-monte tulishakamtaa kutokana na miradi mingi tunayompa kushindwa kumaliza miradi kwa wakati licha ya kupewa fedha lakini bado anatusumbua”amesema Ngumilamoto,
Ngumilamoto amesema Halmashauri hiyo ilishaingia Mkataba na kampuni hiyo hivyo hawezi kumkatisha mkataba wake,ila amedai kuwa Mkataba wake ukishamalizika hawataendelea nayo kampuni hiyo ikiwemo kuipa tenda tena katika Halmashauri hiyo.
Sanjari na hayo,pia Ngumilamoto amemtaka Kaimu Mhandisi wa Manispaa hiyo,Nyamagulula Masatu kuhakikisha anasimamia miradi huo uwe unakamilika kwa wakati na kuisimamia ipasavyo kutokana na kuwepo kwa miradi mingi ya Barabara kuharibika hata mwaka mmoja haujamilizika.
Kwa Upande wake Mhandisi Masatu alimuhakikishia Ngumilamoto kuwa ataisimamia mradi huo na kuhakikisha itaisha kwa wakati.
WAKATI wachambuzi wa masuala ya masuala ya kisiasa na kiuchumi wakielezea kuporomoka kwa uchumi na kuongezeka kwa ugumu wa maisha hapa nchini, Profesa Benno Ndulu, Gavana wa Benki Kuu amesema hali ya ukuaji wa uchumi ni ya kuridhisha, anaandika, Pendo Omary.
Prof. Ndulu amesema, takwimu kutoka Ofisi ya Taifa, katika robo ya kwanza ya mwaka 2016, ukuaji wa Pato la Taifa unakadiliwa kuongezeka kwa asilimia 5.5 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 5.7 kipindi kama hicho mwaka 2015.
Amezitaja shughuli zilizochangia ukuaji wa uchumi kwa kiasi kikubwa kuwa ni; kilimo, biashara, uchukuzi, sekta ya fedha na mawasiliano huku akieleza kuwa shughuli za kiuchumi zilizokua kwa kasi katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 ni sekta ya fedha (asilimia 13.5), mawasiliano (asilimia 13.4) na utawala wa umma (asilimia 10.2).
“Uzalishaji wa umeme nchini katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016 umeongezeka kwa asilimia 14.5 kufikia kWh milioni 3,454.2 ikilinganishwa na kWh milioni 3,016.7 katika kipindi kama hicho mwaka 2015,” amesema Prof. Ndulu.
Aidha amesema uzalishaji wa saruji katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 umeongezeka kwa asilimia 7 na kufikia tani elfu 725.4 ikilinganishwa na tani elfu 680.1. Hali hiyo imechangiwa na ongezeko la uzalishaji wa kampuni ya Dangote ambayo yenye uwezo wa kuzalisha tani 3 Milioni.
Kuhusu mfumuko wa bei, amesema “katika miezi sita ya kwanza ya mwaka 2016 umeshuka hadi kufikia asilimia 5.5 mwezi Juni 2016 na asilimia 4.9 mwezi Agosti 2016 kutoka asilimia 6.8 Desemba 2015.
“Wastani wa mfumuko wa bei usiojumuisha bei za vyakula na nishati ambao ni kiashiria sahihi zaidi cha utekelezaji wa sera ya fedha, umeendelea kubaki katika viwango vya chini wastani wa asilimia 2.8,” amesema Prof. Ndulu.
Amesema ongezeko la fedha taslimu, ambacho ni kipimo cha ukwasi kwenye uchumi limeendelea kubakia ndani ya malengo katika kipindi chote cha miezi sita ya kwanza ya mwaka 2016.
“Mikopo mingi kwa sekta binafsi ilielekezwa kwenye shughuli za biashara kwa wastani wa asilimia 19.0, uzalishaji wa viwandani wastani wa asilimia 10.6, uchukuzi na mawasiliano wastani wa asilimia 7.9 na shughuli za kilimo asilimia 7.8,” ameeleza Prof. Ndulu.
Pia amefafanua kuwa katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo ya mwaka 2016 Shilingi imekuwa ikibadilishwa kwa kati ya Sh. 2,180 hadi 2,190 kwa dola moja ya Marekani akisema kufikia mwezi Juni 2016, kulikuwa na jumla ya benki na taasisi za fedha zinazosimamiwa na Benki Kuu zipatazo 65 zenye matawi 739 nchini.
Kiwango cha mitaji kikilinganishwa na mali iliyowekwa kilikuwa asilimia 17.7 kikilinganishwa na kiwango cha chini kinachotakiwa kisheria cha asilimia 12.0.
Akizungumzia deni la taifa, Prof. Ndulu amesema deni la taifa limeendelea kuongezeka na kufikia dola za Kimarekani 20,851 Milioni mwisho wa mwezi Juni 2016 kutoka dola za Kimarekani 19,861 Milioni mwezi Desemba 2015.
“Asilimia 83.4 ya deni la nje ni deni la serikali na tasisi za umma. Pamoja na ongezeko hilo, takwimu zinaonyesha kuwa deni letu bado ni stahimilivu. Kwa mfano, deni la nje kwa thamani ya sasa ni karibu asilimia 20 ya pato la taifa, ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 50 ya pato la taifa.
Deni la ndani liliongezeka kufikia Sh. 10,038.4 bilioni mwishoni mwa mwezi Juni 2016 na kukopa Sh. 8,597.0 Bilioni mwezi Desemba 2015. Ongezeko hilo lilitokana na serikali kukopa kupitia dhamana na hati fungani kwa ajili ya kugharamia bajeti ya serikali kwa mwaka 2015/2016, ikilinganishwa na kupungua kwa misaada na mikopo kutoka nje,” amefafanua Prof. Ndulu.
Majambazi wapatao 10 juzi usiku walivamia magari mawili yaliyobeba wafanyabiashara waliokuwa wakitokea mnadani na kumuua kwa risasi, dereva aliyegoma kuwapa fedha na simu.
Dereva huyo, Chrispin Inyangwe (40) alipigwa risasi ya mgongoni alipojaribu kupambana nao.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana eneo la katikati ya vijiji vya Miula na Kalundi vilivyopo Kata ya Kipande wilayani Nkasi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema wafanyabiashara hao walikuwa wakitokea mnadani na walipofika eneo hilo walikuta mawe yamepangwa barabarani kuzuia magari.
Alisema baada ya kuona mawe hayo, magari hayo yalilazimika kusimama na ndipo majambazi hao waliokuwa na silaha za moto, mapanga na marungu walipoibuka na kufyatua risasi hewani na baadaye kutaka wafanyabiashara hao wasalimishe fedha na simu zao za mkononi.
Kamanda huyo alisema baadhi ya wafanyabiashara walisalimisha fedha na simu zao, na waliokataa walishambuliwa.
Inasemekana kwamba Inyangwe ambaye alikuwa dereva wa gari aina ya Mitsubishi Canter alikaidi kutoa fedha na kutaka kupambana nao, ndipo watu hao waliokuwa na bunduki aina ya SMG walipomfyatulia risasi iliyompata mgongoni na kufariki dunia papo hapo.
Kitendo hicho kiliwafanya wafanyabiashara wengine waliokuwa wakikataa kutoa fedha, kuzisalimisha sambamba na simu zao, ndipo majambazi hao walipowaachia na kukimbia.
Watu 19 waliojeruhiwa walipelekwa Hospitali ya Mkoa mjini Sumbawanga. Kamanda Kyando alisema majeruhi 12 waliruhusiwa kurejea nyumbani na wengine saba wanaendelea na matibabu na kwamba polisi wanaeendelea na msako wa watu hao.
JAMHURI ya Muungano wa Tanzania imempandisha kizimbani, Denis Temu, Mkazi wa Tabata Bima, jijini Dar es Salaam kwa madai ya kushabikia Ukuta, anaandika Faki Sosi.
Wakati Jamhuri ikiendelea kuwapandisha kizimbani watuhumiwa mbalimbali, Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ameendelea kushinda mahakamani kutetea watuhumiwa wa Ukuta.
Ukuta ni Umoja wa Kupinga Udikteta nchini, operesheni hiyo ilitangazwa na Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema-Taifa Julai mwaka huu kwa niaba ya Kamati Kuu ya chama hicho.
Operesheni hiyo ilipangwa kuanza kufanyika Septemba Mosi mwaka huu lakini viongozi wa dini, taasisi za kiraia na serikali ziliutaka uongozi wa Chadema kutofanya mikutano na maandamano chini ya Ukuta ili kuweka mazingira sawa ya mazungumzo na Rais John Magufuli.
Temu amepandishwa kizimbani leo kwa tuhuma za kuandika maneno yanayodaiwa kuwa ya uchochezi kwenye ukurasa wake wa kijamii wa ‘Facebook’ kuhusu Ukuta.
“Nipo tayari kwa Ukuta, naomba mnikabidhi askari 10, nikiwashindwa Mungu anihukumu.”
Kwenye kesi hiyo iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mshitakiwa huyo amefunguliwa kesi ya kulidhalilisha Jeshi la Polisi.
Akisoma shitaka hilo Salumu Mohammed, Wakili wa Serikali mbele ya Amillius Mchauru, Hakimu Mkazi Mkuu amedai kuwa, mtuhumiwa huyo aliandika maneno hayo kwenye ukurasa wake wa Facebook.
Mohammed amedai kuwa, mtuhumiwa anadaiwa kutenda kosa hilo tarehe 30 Agosti mwaka huu.
Kwenye kesi hiyo, Mohammed anawakilishwa na Tundu Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki.
Hata hivyo, Mohammed amekana shitaka hilo ambapo amedhaminiwa na wadhamini wawili kwa wadhamini kusaini hati ya Sh. 500,000 kila mmoja.
Upande wa Jamhuri umedai kwamba, upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea. Kesi hiyo itatajwa tena tarehe 12 Oktoba mwaka huu.
Mtuhumiwa huyo ni miongoni mwa vijana waliokamatwa na Jeshi la Polisi kabla ya Septemba Mosi.