naibu waziri wa ujenzi elias kwandikwa (wa pili kulia) akisalimiana na baadhi ya viongozi wa wilaya ya mufindi mkoani iringa kabla ya kukagua ukarabati wa barabara ya mafinga-igawa sehemu ya tazam unaotekelezwa na kampuni ya kichana ya CCECC kwa kiwango cha lami leo. (picha na friday simbaya)
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mheshimiwa Elias Kwandikwa (Mb), ametoa wito kwa wananchi na watumia barabara kuhakikisha wanatunza miundombiunu za barabara ili kupunguza matengenezo ya barabara ya mara kwa mara.
Kwandikwa ametoa wito huo mkoani Iringa wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Mafinga-Igawa yenye urefu wa KM 137.9 sehemu ya barabara kuu ya TANZAM.
Alisisitiza kuwa umuhimu wa kutunza miundombini ya barabara kutasaidia barabara hizo kutumika kwamuda mrefu na kuondoa malalamiko kwa wananchi na baadhi ya viongozi kuwa wanashindwa kufanya shughuli za maendeleo kwa kisingizio cha ubovu wa barabara.
Kuhusu barabara hiyo ya Mafinga-Igawa inayojengwa kufuatia agizo la Rais Dkt John Magufuli, Kwandikwa amemtaka mkandarasi kuhakikisha ujenzi huo unafanyika kwa kuzingatia viwango vya ubora uliopangwa kwa mujibu wa mkataba wake.
Kwa upande wake Meneja wa wakala wa barabara (TANROADS) mkoa wa Iringa Mhandisi Daniel Kindole, amemuhakikishia Naibu Waziri Kwandikwa kuwa serikali ya mkoa huo imejipanga kushirikiana na mkandarasi ili barabara hiyo ikamilike ndani ya muda uliopangwa.
Mhandisi Kindole alisema kuwa Wakala utawasimamia makandarasi wa kichana China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) ili kuhakikisha wanamaliza ujenzi huo kwa wakati baada ya changamoto ya tatizo la maji kupatiwa ufumbuzi.
Naibu Waziri Elias Kwandikwa, alikuwa katika ziara ya kikazi ya kukagua ujenzi wa barabara pamoja na miradi inayosimamiwana wakala ya majengo Tanzania (TBA).