Wednesday, 23 November 2011

KIKWETE AKATA MZIZI WA FITINA KUHUSU GARI LA WAGONJWA MLANGALI AWALI WANANCHI WALIJIPANGA BARABARANI KUKUMBUSHA AHADI YA RAIS, MADIWANI WAPIGWA MSHANGAO

Ludewa

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete jana alikata mzizi wa fitina kutokana na utata uliokuwepo kati ya wananchi na Baraza la Madiwani kuhusu gari la wagonjwa  Namba SM 9192 aliloahidi kwa Kituo cha Afya Mlangali mwaka 2008.
Dr. Kikwete alifikia hatua hiyo baada ya wananchi wa Kata ya Mlangali waliokuwa wamesimama barabarani kumlaki na alipowataka watoe shida zao wakamwambia kuwa wanashukuru kwa kutimiza ahadi ingawa wameipata jana wakati gari hilo lina zaidi ya miezi saba wilayani.
Wananchi wa Mlangali pamoja na mambo mengine walimwambia Rais kuwa katika Kata yao wanakabiliwa na mambo mengi ikiwemo maji safi, barabara, gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) na umeme.
Madiwani katika kikao chao cha Julai 15 mwaka huu walikubaliana kwa kauli moja kuchukua gari la kubebea wagonjwa (Ambullance) No. SM 4677 lililokuwa katika Hospitali ya Wilaya na kulipeleka Lupingu ili kuwahudumia wananchi wa Mwambao na gari SM 9192 lililotolewa na Rais kubakizwa wilayani huku, mbunge akiahidi kupeleka haraka gari jingine Mlangali.
Kutokana na utata huo wananchi wa Mlangali waliposikia ziara ya Rais waliamua kujipanga barabarani ili kudai haki yao kama alivyoowaahidi mwaka 2008 na siku moja kabla ya rais kufika walikabidhiwa gari kwa maandishi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa Matei Kongo kwa upande wake alisema kuwa gari SM 9192 lililetwa bila maelekezo ndiyo maana Baraza la Madiwani lililofanyika Julai 15 mwaka huu liliamua kwa kuzingatia vipaumbele na jiografia ya wilaya, lakini maelekezo ya rais ni sahihi tu aliongeza.
Katika barua yake kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Katibu Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ilielekeza kuwa gari lenye namba za usajiri SM 9192 lililokabidhiwa Aprili 01 mwaka huu ni kwa ajili ya kutekeleza ahadi ya Mh Rais wa Jamhuri ya Muungano na lilitolewa kwa ajili ya matumizi ya Kituo cha Afya cha Mlangali.
Diwani wa Kata ya Mlangali Bw. Rudolf Kacheche Chaula kwa upande wake alisema rais alitoa ahadi hiyo mwaka 2008 na gari hilo kufika wilayani Ludewa mwezi April mwaka huu, lakini limekabidhiwa Mlangali Novemba 11 mwaka huu takribani miezi saba limekaa nje.
Kacheche alisema yeye na wananchi wake wanamshukuru rais kwa maamuzi hayo, na kwamba hakuna sababu ya kutafuta mchawi kwa sababu aliyetoa ndiye aliye elekeza matumizi ya gari hilo ingawa hakuzuia gari hilo kutumika mahali popote ndani na nje ya Halmashauri.
Aliongeza kuwa baraza la madiwani lililokaa na kuelekeza gari la wagonjwa namba SM 9192 libaki katika Hospitali ya Wilaya na SM 4677 lipelekwe Lupingu lilizingatia jiografia ya wilaya na kwamba nia ilikuwa nzuri tu, lakini kwa kuwa aliyeleta ndiye aliyeelekeza vinginevyo inabidi tukubali.

DC LUDEWA, SITAYUMBISHWA NA WAWEKEZAJI WATAKAOVUNJA SHERIA ZA NCHI MCHUCHUMA NA LIGANGA.

Ludewa

MKUU wa Wilaya ya Ludewa mkoani Iringa Bi Georgina Bundala amekana kutoyumbishwa kwa namna yoyote ile na wawekezaji wataovunja sheria za nchi na zile zilizopo katika mikataba ya sheria ya madini ya Liganga na Mchuchuma.
Bi Georgina aliwaambia waandishi wa habari jana ofisini kwake ambao pamoja na mambo mengine walitaka kujua amejipanga vipi na nini msimamo wake kwa wawekezaji wenye tabia ya kuwayumbisha viongozi, hasa wakuu wa wilaya nchini waliopo ndani ya migodi kwa manufaa yao binafsi.
Aliongeza kuwa wawekezaji wengi nchini wanapokuja kuomba kuwekeza wanakuwa na nidhamu na kuonesha ushirikiano wenye kuleta ufanisi kwa nia nzuri ya kuchochea chachu ya kuwaletea maendeleo wananchi waishio maeneo ya migodi, lakini baadaye hugeuka na kuwafanya wananchi kuwa wakimbizi nchini mwao siko tayari kuwaonea aibu, alisisitiza.
“Sheria za nchi zipo wala sina haja ya kuumiza kichwa na kupoteza muda mtu yeyote atakayekiuka au kuvunja sheria kwa lengo la kuwanyanyasa wananchi tofauti na makubaliano yaliyomo ndani ya mkataba wake na serikali kwa niaba ya wananchi sheria itafuata mkondo wake,” alisisitiza Bundala.
Aidha, mkuu huyo amewataka wananchi wilayani humo kuongeza kasi ya kuwapeleka na kuwapatia vijana elimu ya kutosha hasa katika Nyanja ya ufundi stadi kwa nia ya kuliteka soko la ajira pindi madini hayo yatakapoanza kuchimbwa kufuatia serikali kutiliana na wawekezaji wa ndani na nje baada ya kushinda zabuni.
Kuhusu Chuo cha Ufundi VETA kilichotakiwa kujengwa katika maeneo ya kijiji cha Shaurimoyo Kata ya Lugarawa, Bi Georgina alisema kuna uwezekano mkubwa wa chuo hicho kujengwa katika Kata ya Ludewa Makao Makuu ya Wilaya ya Ludewa kutokana na sababu kuu nne.
Alizitaja baadhi ya sababu zitakazofanya chuo hicho kujengwa mjini kuwa ni pamoja na chuo hicho kuwa karibu na huduma muhimu kama vile benki, ili kuwa na urahisi wa kupata fedha, hospitali, mawasiliano, usalama na kuwa jirani na ofisi za utawala.
Kutokana na hali hiyo madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa wanatakiwa kukaa upya ili kubadili mihutasari na kupeleka kwenye kikao cha ushauri cha wilaya (DCC ) tayari kwa kupeleka mapendekezo kwenye kamati ya ushauri ya Mkoa (RCC) kwa hatua.
Hata hivyo mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi kuanza kujiandaa kwa kuchangamkia fursa zitakazotokana na uwekezaji kama vile matunda, mbogamboga, kujenga nyumba za kupangisha wageni wanaotarajia kuja wilayani Ludewa kwa shughuli mbalimbali.
Wataalamu na watafiti mbalimbali wa madini nchini wamegundua kuwa karibu ardhi yote ndani ya Wilaya ya Ludewa imegubikwa na madini kwa hiyo wananchi wasipojiandaa vema kuna hatari ya wao kuendelea kuwa maskini wa kipato huku wakiwaacha wageni wakinufaika na rasilimali hiyo.



LHRC, YAAMSHA MADIWANI LUDEWA, NI KUHUSU HAKI ZA BINADAMU NA WAJIBU ZAO.

Ludewa
 
HUKU Tanzania ikiadhimisha miaka Hamsini ya Uhuru madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa katika Mkoa Iringa bado wanabanwa na mfumo wa utawala na kushindwa kusimamia mali za umma.
Wakizungumza jana katika semina ya siku tatu kuhusu sheria za kazi, rushwa na utawala bora, haki za binadamu, Katiba, wajibu na maadili ya diwani, iliyoendeshwa na Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu walipongeza kituo hicho kwa kuwafumbua macho.
Madiwani hao walilalamikia mifumo na miongozo mibaya ya TAMISEMI inayoleta urasimu kwa nia ya kudhoofisha nafasi na hadhi ya madiwani kwa wananchi jambo linalopelekea kudharauliwa na watumishi wa Halmashauri.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa Bw. Emanuel Mlelwa ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mafunzo hayo alisema mafunzo haya yamekuja wakati mwafaka kwa madiwani hao kutokana na wengi wao kutokujua vyema sheria, maadili na wajibu zao.
Mlelwa aliwataka madiwani kuwa wasikivu kwani mafunzo hayo ni ukombozi kwao kwa kuwa semina elekezi walizopewa hazitoshi kuwa kitendea kazi kwao kwa sababu hazifafanui vyema mambo ya sheria.
Akimkaribisha mgeni rasmi Bi Edina Lushaka ambaye ni mwanasheria kutoka kituo cha sheria na haki za binadamu cha jijini Dar es Salaam alisema nia ya kutoa mafunzo haya ni kuwapa madiwani elimu kuhusu haki za binadamu katika maeneo yao.
Lushaka alimwambia mgeni rasmi kuwa madiwani wanapashwa kujua wajibu zao na maadili ikiwemo kudumisha uhusiano baina yao na watumishi wa Halmashauri kama kanuni ya 25 hadi 28 inavyobainisha.
“Diwani kama kiongozi ni mtoa maamuzi, msimamizi, mwajiri na mdhibiti wa shughuli za Halmashauri na kwamba siyo mtendaji, bali ni mwakilishi anayewajibika kwa wananchi wake,” aliongeza Bi. Edina Lushaka.
Naye Bahati Mwanu katika mada zake aliwaeleza madiwani maana ya Katiba na historia ya katiba ulimwenguni, historia ya katiba Tanzania, historia ya haki za binadamu, vizazi na sifa za haki za binadamu utetezi, ulinzi wa haki na faida za kuheshimu haki.
Bi. Manu aliwataka madiwani kujua misingi, taswira na malengo ya kanuni za maadili yao, sifa binafsi za diwani, tabia ya hadharani ya diwani, mali, mapato, madaraka kisiasa ikiwemo uwajibikaji, maslahi na kinga na rufaa kwa anayeona ameonewa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa Bw Matei Kongo akiungwa mkono na madiwani wake, alisema Serikali kupitia TAMISEMI imekuwa ikiwabana na kuwapa watumishi nafasi bila kuwa na sifa.
Kongo alisema watumishi wengi wamekuwa wakikaidi maelekezo ya madiwani kwa majigambo na kujivunia TAMISEMI na kwamba diwani hana mamlaka ya kuwafukuza kazi na kuongeza kuwa hili ni tatizo linalosababishwa na mifumo mibaya serikalini.
Diwani ni kiungo kati ya Halmashauri na vijiji na mitaa na mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya Kata na anapashwa kujua hali ya uchumi inayowakabili wananchi anaowaongoza, uboreshaji wa huduma na shughuli za maendeleo zinazoweza kuwakwamua katika dimbwi la umaskini.

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...