Ludewa
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya
Mrisho Kikwete jana alikata mzizi wa fitina kutokana na utata uliokuwepo
kati ya wananchi na Baraza la Madiwani kuhusu gari la wagonjwa Namba
SM 9192 aliloahidi kwa Kituo cha Afya Mlangali mwaka 2008.
Dr. Kikwete alifikia hatua hiyo baada ya wananchi wa
Kata ya Mlangali waliokuwa wamesimama barabarani kumlaki na alipowataka
watoe shida zao wakamwambia kuwa wanashukuru kwa kutimiza ahadi ingawa
wameipata jana wakati gari hilo lina zaidi ya miezi saba wilayani.
Wananchi wa Mlangali pamoja na mambo mengine
walimwambia Rais kuwa katika Kata yao wanakabiliwa na mambo mengi
ikiwemo maji safi, barabara, gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) na
umeme.
Madiwani katika kikao chao cha Julai 15 mwaka huu
walikubaliana kwa kauli moja kuchukua gari la kubebea wagonjwa
(Ambullance) No. SM 4677 lililokuwa katika Hospitali ya Wilaya na
kulipeleka Lupingu ili kuwahudumia wananchi wa Mwambao na gari SM 9192
lililotolewa na Rais kubakizwa wilayani huku, mbunge akiahidi kupeleka
haraka gari jingine Mlangali.
Kutokana na utata huo wananchi wa Mlangali waliposikia
ziara ya Rais waliamua kujipanga barabarani ili kudai haki yao kama
alivyoowaahidi mwaka 2008 na siku moja kabla ya rais kufika
walikabidhiwa gari kwa maandishi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa Matei
Kongo kwa upande wake alisema kuwa gari SM 9192 lililetwa bila maelekezo
ndiyo maana Baraza la Madiwani lililofanyika Julai 15 mwaka huu
liliamua kwa kuzingatia vipaumbele na jiografia ya wilaya, lakini
maelekezo ya rais ni sahihi tu aliongeza.
Katika barua yake kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Ludewa, Katibu Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
ilielekeza kuwa gari lenye namba za usajiri SM 9192 lililokabidhiwa
Aprili 01 mwaka huu ni kwa ajili ya kutekeleza ahadi ya Mh Rais wa
Jamhuri ya Muungano na lilitolewa kwa ajili ya matumizi ya Kituo cha
Afya cha Mlangali.
Diwani wa Kata ya Mlangali Bw. Rudolf Kacheche Chaula
kwa upande wake alisema rais alitoa ahadi hiyo mwaka 2008 na gari hilo
kufika wilayani Ludewa mwezi April mwaka huu, lakini limekabidhiwa
Mlangali Novemba 11 mwaka huu takribani miezi saba limekaa nje.
Kacheche alisema yeye na wananchi wake wanamshukuru
rais kwa maamuzi hayo, na kwamba hakuna sababu ya kutafuta mchawi kwa
sababu aliyetoa ndiye aliye elekeza matumizi ya gari hilo ingawa
hakuzuia gari hilo kutumika mahali popote ndani na nje ya Halmashauri.
Aliongeza kuwa baraza la madiwani lililokaa na
kuelekeza gari la wagonjwa namba SM 9192 libaki katika Hospitali ya
Wilaya na SM 4677 lipelekwe Lupingu lilizingatia jiografia ya wilaya na
kwamba nia ilikuwa nzuri tu, lakini kwa kuwa aliyeleta ndiye
aliyeelekeza vinginevyo inabidi tukubali.
No comments:
Post a Comment