Ludewa
MKUU wa Wilaya ya Ludewa mkoani Iringa Bi Georgina
Bundala amekana kutoyumbishwa kwa namna yoyote ile na wawekezaji
wataovunja sheria za nchi na zile zilizopo katika mikataba ya sheria ya
madini ya Liganga na Mchuchuma.
Bi Georgina aliwaambia waandishi wa habari jana
ofisini kwake ambao pamoja na mambo mengine walitaka kujua amejipanga
vipi na nini msimamo wake kwa wawekezaji wenye tabia ya kuwayumbisha
viongozi, hasa wakuu wa wilaya nchini waliopo ndani ya migodi kwa
manufaa yao binafsi.
Aliongeza kuwa wawekezaji wengi nchini wanapokuja
kuomba kuwekeza wanakuwa na nidhamu na kuonesha ushirikiano wenye kuleta
ufanisi kwa nia nzuri ya kuchochea chachu ya kuwaletea maendeleo
wananchi waishio maeneo ya migodi, lakini baadaye hugeuka na kuwafanya
wananchi kuwa wakimbizi nchini mwao siko tayari kuwaonea aibu,
alisisitiza.
“Sheria za nchi zipo wala sina haja ya kuumiza kichwa
na kupoteza muda mtu yeyote atakayekiuka au kuvunja sheria kwa lengo la
kuwanyanyasa wananchi tofauti na makubaliano yaliyomo ndani ya mkataba
wake na serikali kwa niaba ya wananchi sheria itafuata mkondo wake,”
alisisitiza Bundala.
Aidha, mkuu huyo amewataka wananchi wilayani humo
kuongeza kasi ya kuwapeleka na kuwapatia vijana elimu ya kutosha hasa
katika Nyanja ya ufundi stadi kwa nia ya kuliteka soko la ajira pindi
madini hayo yatakapoanza kuchimbwa kufuatia serikali kutiliana na
wawekezaji wa ndani na nje baada ya kushinda zabuni.
Kuhusu Chuo cha Ufundi VETA kilichotakiwa kujengwa
katika maeneo ya kijiji cha Shaurimoyo Kata ya Lugarawa, Bi Georgina
alisema kuna uwezekano mkubwa wa chuo hicho kujengwa katika Kata ya
Ludewa Makao Makuu ya Wilaya ya Ludewa kutokana na sababu kuu nne.
Alizitaja baadhi ya sababu zitakazofanya chuo hicho
kujengwa mjini kuwa ni pamoja na chuo hicho kuwa karibu na huduma muhimu
kama vile benki, ili kuwa na urahisi wa kupata fedha, hospitali,
mawasiliano, usalama na kuwa jirani na ofisi za utawala.
Kutokana na hali hiyo madiwani katika Halmashauri ya
Wilaya ya Ludewa wanatakiwa kukaa upya ili kubadili mihutasari na
kupeleka kwenye kikao cha ushauri cha wilaya (DCC ) tayari kwa kupeleka
mapendekezo kwenye kamati ya ushauri ya Mkoa (RCC) kwa hatua.
Hata hivyo mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi
kuanza kujiandaa kwa kuchangamkia fursa zitakazotokana na uwekezaji kama
vile matunda, mbogamboga, kujenga nyumba za kupangisha wageni
wanaotarajia kuja wilayani Ludewa kwa shughuli mbalimbali.
Wataalamu na watafiti mbalimbali wa madini nchini
wamegundua kuwa karibu ardhi yote ndani ya Wilaya ya Ludewa imegubikwa
na madini kwa hiyo wananchi wasipojiandaa vema kuna hatari ya wao
kuendelea kuwa maskini wa kipato huku wakiwaacha wageni wakinufaika na
rasilimali hiyo.
No comments:
Post a Comment