HUKU Tanzania ikiadhimisha miaka Hamsini ya Uhuru
madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa katika Mkoa Iringa bado
wanabanwa na mfumo wa utawala na kushindwa kusimamia mali za umma.
Wakizungumza jana katika semina ya siku tatu kuhusu
sheria za kazi, rushwa na utawala bora, haki za binadamu, Katiba, wajibu
na maadili ya diwani, iliyoendeshwa na Kituo Cha Sheria na Haki za
Binadamu walipongeza kituo hicho kwa kuwafumbua macho.
Madiwani hao walilalamikia mifumo na miongozo mibaya
ya TAMISEMI inayoleta urasimu kwa nia ya kudhoofisha nafasi na hadhi ya
madiwani kwa wananchi jambo linalopelekea kudharauliwa na watumishi wa
Halmashauri.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa
Bw. Emanuel Mlelwa ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa
mafunzo hayo alisema mafunzo haya yamekuja wakati mwafaka kwa madiwani
hao kutokana na wengi wao kutokujua vyema sheria, maadili na wajibu zao.
Mlelwa aliwataka madiwani kuwa wasikivu kwani mafunzo
hayo ni ukombozi kwao kwa kuwa semina elekezi walizopewa hazitoshi kuwa
kitendea kazi kwao kwa sababu hazifafanui vyema mambo ya sheria.
Akimkaribisha mgeni rasmi Bi Edina Lushaka ambaye ni
mwanasheria kutoka kituo cha sheria na haki za binadamu cha jijini Dar
es Salaam alisema nia ya kutoa mafunzo haya ni kuwapa madiwani elimu
kuhusu haki za binadamu katika maeneo yao.
Lushaka alimwambia mgeni rasmi kuwa madiwani
wanapashwa kujua wajibu zao na maadili ikiwemo kudumisha uhusiano baina
yao na watumishi wa Halmashauri kama kanuni ya 25 hadi 28
inavyobainisha.
“Diwani kama kiongozi ni mtoa maamuzi, msimamizi,
mwajiri na mdhibiti wa shughuli za Halmashauri na kwamba siyo mtendaji,
bali ni mwakilishi anayewajibika kwa wananchi wake,” aliongeza Bi. Edina
Lushaka.
Naye Bahati Mwanu katika mada zake aliwaeleza madiwani
maana ya Katiba na historia ya katiba ulimwenguni, historia ya katiba
Tanzania, historia ya haki za binadamu, vizazi na sifa za haki za
binadamu utetezi, ulinzi wa haki na faida za kuheshimu haki.
Bi. Manu aliwataka madiwani kujua misingi, taswira na
malengo ya kanuni za maadili yao, sifa binafsi za diwani, tabia ya
hadharani ya diwani, mali, mapato, madaraka kisiasa ikiwemo uwajibikaji,
maslahi na kinga na rufaa kwa anayeona ameonewa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa Bw Matei
Kongo akiungwa mkono na madiwani wake, alisema Serikali kupitia
TAMISEMI imekuwa ikiwabana na kuwapa watumishi nafasi bila kuwa na sifa.
Kongo alisema watumishi wengi wamekuwa wakikaidi
maelekezo ya madiwani kwa majigambo na kujivunia TAMISEMI na kwamba
diwani hana mamlaka ya kuwafukuza kazi na kuongeza kuwa hili ni tatizo
linalosababishwa na mifumo mibaya serikalini.
Diwani ni kiungo kati ya Halmashauri na vijiji na
mitaa na mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya Kata na anapashwa kujua
hali ya uchumi inayowakabili wananchi anaowaongoza, uboreshaji wa huduma
na shughuli za maendeleo zinazoweza kuwakwamua katika dimbwi la
umaskini.
No comments:
Post a Comment