MKOA wa Iringa umetekeleza agizo la Rais Dk John Magufuli kwa kufanikiwa kumaliza tatizo la upungufu wa madawati 29, 347 ambayo kati yake 26,046 ulikuwa ukizikabili shule za msingi 478 na 3,301 uliokuwa ukizikabili shule 107 za sekondari.
Akikabidhi sehemu ya madawati hayo katika hafla fupi iliyofanyika kwenye karakana ya chuo cha Ufundi Stadi (VETA) mjini Iringa jana, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza alisema mpaka jana madawati 21,304 yalikuwa yamekamilika na kusambazwa katika shule hizo.
“Hadi leo tuna madawati 21,304 yaliyokamilika huku madawati 8,163 kwa ajili ya shule za msingi na 1,264 kwa ajili ya shule za sekondari yakiendelea kutengenezwa katika karakana mbali mbali na fedha kwa ajili ya matengenezo hayo tayari zimelipwa,” alisema.
Alisema madawati yaliyochelewa kukamilika ndani ya muda uliopangwa yatakuwa yamekamilika ifikapo Julai 15, mwaka huu na yatasambazwa kwa shule hizo haraka iwezekanavyo.
“Yamechelewa kukamalika kwasababu mafundi waliopewa kuifanya kazi hiyo, walielemewa na kazi yenyewe iliyohitaji uharaka na umakini kwa pamoja,” alisema.
Alisema kazi ya kutengeneza madawati hayo imefanywa kupitia bajeti za halmashauri husika na michango ya wadau mbalimbali wa maendeleo wa mkoa wa Iringa walioko nje na ndani ya halmashauri husika.
“Nishukuru zoezi lililoagizwa na mheshimiwa rais limetekelezwa kutokana na mwitikio mzuri tulioupata kutoka kwa wadau wetu wa maendeleo,” alisema..
Alisema Rais Magufuli alitoa agizo kwa wakuu wote wa mikoa nchini kuhakikisha wanafunzi wote wanakaa katika madawati ifikapo Juni 30 mwaka huu.
Kwa kuzingatia agizo hilo, Masenza alisema alilazimika kuwashirikisha wakuu wake wa wilaya ambao kwa kushirikiana na wadau hao wamesaidia kumaliza upungufu huo.
Akizungumzia mchango wa mkoa katika kufanikisha agizo hilo la Rais, Masenza alisema kwa msaada wa wadau mbalimbali ofisi yake ilitengeneza madawati 700.
Masenza alisema kati ya madawati hayo, 200 ameyatoa kwa halmashauri ya manispaa ya Iringa, Mafinga Mji madawati 100, Iringa Vijijini madawati 100, Mufindi madawati 100 na Kilolo madawati 100.