Tuesday, 14 April 2015

SERIKALI YASEMA UJENZI WA KITUO CHA MAFUTA NDIUKA NI SALAMA



Mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza (mbele kulia) akitoa taarifa ya mkoa wa iringa ya mafanikio ya utekelezaji wa matokeo makubwa sasa (BRN) Julai, 2013 hadi kufikia Februari, 2015 wakati mkutano na waandishi wa habari jana. 


Serikali ya Mkoa wa Iringa imewatoa hofu wananchi kuhusu ujenzi wa kituo cha mafuta kinachojengwa eneo oevu (wetland) ya Mto Ruaha eneo la Ndiuka Ipogolo, Manispaa ya Iringa. 


Akitoa taarifa ya Mkoa wa Iringa ya mafanikio ya utekelezaji wa matokeo makubwa sasa (BRN) Julai, 2013 hadi kufikia Februari, 2015, kwa waandishi wa habari jana, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema kuwa ujenzi wa kituo hicho hautakuwa na adhari zozote za kimazingira.


Alisema kuwa uongozi wa mkoa ulipata taarifa kuwa ujenzi wa kituo cha mafuta (petrol station) ulikuwa unatarajiwa kuanza katika Kiwanja Namba 30/1 Kitalu “A” kilichopo eneo la Ndiuka Ipogolo katika Manispaa ya Iringa. 


Aidha, alisema kuwa ujenzi huo ulikwisha pata kibali cha ujenzi kutoka manispaa baada ya kampuni ya Puma Energy Tanzania Limited, inayojenga kituo hicho, kuwasilisha cheti cha tathmini ya mazingira.


Alisema kuwa baada ya kupata taarifa hizi, uongozi wa mkoa uliona ni muhimu kujiridhisha juu ya usalama wa wananchi, kutokana na kituo hiki kujengwa katika eneo oevu la mto ruaha, ambao maji yake yanatumiwa na wananchi wengi. 


Aidha, wadau walisema ujenzi wa kituo hicho kinaweza kuwa chanzo cha ajali za magari kwa kuwa kinajengwa jirani na barabara kuu ya TANZAM na ile inayopandisha mjini Iringa.


Hatua zilizochukuliwa na mkoa, tarehe 29/12/2014, mkuu wa mkoa alimwandikia barua Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira, Dkt. Binillith Mahenge (MB), kufika ili kusaidia kutoa ufafanuzi kuhusu ujenzi wa kituo hicho ikizingatiwa kuwa eneo hilo ni oevu.


“Waziri mara moja alimtuma Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC), Eng. B. T. Baya kufika mkoani na kukutana na uongozi wa mkoa na manispaa. Mkurugenzi mkuu wa NEMC akiambatana na wataalam wake alifika na kufanya kikao na uongozi wa mkoa na manispaa, ambapo maelezo ya kina yalitolewa juu ya mchakato wa kutoa cheti cha kuruhusu ujenzi wa kituo cha mafuta ulivyofanyika,” alisema mkuu wa mkoa.

Alisema kuwa baada ya maelezo ya mkurugenzi mkuu wa NEMC juu ya masharti aliyopewa mwekezaji (Puma Energy Tanzania Ltd) ili kuhakikisha ujenzi na uendeshaji wa kituo hauathiri mazingira, uongozi wa mkoa uliamua kiitishwe kikao cha wadau katika mradi huo ili NEMC pamoja na mwekezaji watoe ufafanuzi kwa hoja mbalimbali walizonazo wadau kuhusiana na ujenzi huo wa kituo.


Kikao cha wadau, tarehe 13/03/2015 wataalam wa NEMC pamoja na wamiliki wa kampuni ya Puma Energy Tanzania Limited walifika mkoani na kukutana na wadau, ambapo wadau walipata maelezo ya kina juu ya mchakato wa utoaji wa cheti cha tathmini ya athari kwa mazingira ulivyofanyika, na masharti yaliyowekwa ili kuhakikisha kuwa usalama wa maji na mazingira ya mto Ruaha, unazingatiwa. 


Alisema, uongozi wa mkoa, ukishirikisha wataalam na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, uongozi wa manispaa pamoja na wataalam, meneja na wataalam wa Tanroads, Iringa, wataalamu kutoka Bonde la Mto Rufiji, Mamlaka ya Maji mjini Iringa (IRUWASA), Mkurugenzi mkuu na wataalam wa NEMC na mwekezaji (Kampuni ya Puma Energy Tanzania Limited).


Katika kikao hicho wadau walipata nafasi ya kuhoji mambo mbalimbali waliyokuwa na wasiwasi nayo, hususan uchafuzi wa maji ya Mto Ruaha na hofu ya uwezekano wa kutokea ajali za magari katika barabara kuu ya Tanzam jirani na kituo hicho.


Kuhusu uchafuzi wa maji ya Mto Ruaha wadau walielezwa kuwa kwa kuzingatia eneo la kituo kuwa kwenye eneo oevu la mto ruaha, nemc waliagiza utafiti ufanywe ili kujua mwenendo wa maji katika eneo kinapojengwa kituo. 

Utafiti wa ki-haidrojia uliofanywa na Dr. Ibrahim Mjema wa Chuo cha Sua, ulithibitisha kuwa hakutakuwa na uchafuzi wa maji ya Mto Ruaha kutokana na mwenendo wa maji ya ardhini. 


Aidha, maji ya mvua yatakayotiririka yatadhibitiwa kwa kuongozwa kwenye mfereji unaoenda mtoni kabla ya kufika eneo la kituo. 


Alisema kuwa kituo kitajengwa nje ya eneo la Hifadhi ya barabara Kuu ya Tanzam na ile inayoingia mjini Iringa. 


Aidha, magari yanayoingia kituoni yataingia na kutokea katika barabara ya tanzam tu. Sharti hili litawezesha madereva wanaoingia au kutoka kituoni kuona kwa uwazi magari katika barabara kuu, kabla ya kuchepuka kuingia au kutoka kituoni.


“Baada ya wadau kuuliza na kufafanuliwa kwa kina hoja zote, wadau walielewa na kuridhika juu ya tahadhari zilizochukuliwa na masharti yaliyowekwa na NEMC kwa mwekezaji wakati wa ujenzi na uendeshaji wa kituo hicho,”Alielezea mkuu huyonwa mkoa. 


Maoni ya mkoa, kwa kuzingatia uchunguzi uliofanywa na mkoa pia ufafanuzi wa kina wa NEMC kwa wadau kuhusu ripoti ya tathmini ya athari kwa mazingira uliotolewa tarehe 11/03/2015, uongozi wa mkoa umeridhika na mradi huo kutokana na tahadhari zote zilizochukuliwa na zitakazoendelea kuchukuliwa na mwekezaji pia mamlaka zinazoshughulika na kudhibiti uharibifu wa mazingira.

MAGAZETI YA LEO APRIL 14













WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...